REA:Bado vijiji 1,005 umeme kufika Tanzania nzima

NA GODFREY NNKO

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umesema kuwa,ifikapo Juni 2024 wanatarajia kuhitimisha safari ya kupeleka umeme vijiji vyote nchini.

“Mwezi wa sita mwakani (2024), vijiji vyote tutakuwa tumevifikishia umeme, kwa hiyo tutakuwa tumekamilisha kabla ya lengo,kwa sababu tunapata sapoti kubwa kutoka serikalini na wadau wa maendeleo;
Hayo yamebainishwa leo Novemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo, Mhandisi Jones Olotu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,Mhandisi Hassan Saidy katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema, Tanzania Bara kuna vijiji 12,318 ambapo hadi kufikia leo vijiji 11,313 vimeunganishwa na umeme huku vijiji 1,005 vilivyobakia wakandarasi wapo kazini kukamilisha kazi ya kuunganisha na kuwasha umeme.

Mhandisi Olotu amesema, kati ya vitongoji vilivyopo nchini 64,760 tayari vitongoji 28,659 vimefikiwa na umeme.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao kazi hicho kati ya REA, wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa uratibu wa ofisi hiyo ambapo amesema, vikao hivyo vina umuhimu mkubwa kwani vinaupa umma fursa ya kutambua taasisi na mashirika yao yalipotoka, yalipo, yanapoelekea na mafanikio yake kwa ustawi bora wa Taifa.
 
Amefafanua kuwa, vitongoji 36,101 bado wapo mbioni kuvifikishia umeme kwa kuwa mipango tayari imeshaandaliwa.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Olotu amebainisha kuwa,mwaka 2030 malengo yao ni kuhakikisha kuwa, vitongoji vyote vimepata umeme nchini.

Amesema, miongoni mwa changamoto ambazo wanakabiliana nazo ni uharibifu wa miundombinu ikiwemo uharibifu wa nguzo kutokana na shughuli mbalimbali za wananchi katika maeno ambayo wanachoma moto ovyo.
Kutokana na changamoto hiyo, Mhandisi Olotu ameendelea kutoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele kuilinda miundombinu ya nishati ili iweze kuwanufaisha.

Vile vile amesema, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulianzishwa kwa Sheria ya Nishati Vijijini Na.8 ya mwaka 2005 na kuanza kazi rasmi mwezi Oktoba 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa iliyokuwa Sera ya Nishati ya mwaka 2003.

Aidha, Sheria ya Nishati Vijijini pamoja na kuanzisha wakala, pia imeanzisha Bodi ya Mfuko wa Nishati Vijijini.
“REA ni taasisi ya Serikali inayojitegemea ambayo ipo chini ya Wizara ya Nishati ikiwa na jumuku kubwa la kuhamasisha, kuratibu na kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa miradi ya nishati vijiji,”amesema Mhandisi Olotu.

Awali akizungumzia kuhusiana na vikao kazi hivyo ambavyo vinazikutanisha taasisi na mashirika mbalimnali ambayo yapo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Afisa Habari na Mawasiliano wa ofisi hiyo, Sabato Kosuri amesema,lengo ni kuzikutanisha taasisi za umma mbele ya umma kupitia wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Kosuri amesema,vikao hivyo vinazipa nafasi taasisi hizo kuelezea kwa kina walipotoka, walipo, wanapoelekea na mafanikio yao ili umma ambao ni wamiliki wakuu waweze kutambua yanayojiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news