Serikali yafunguka kuhusu uhusiano kati ya Misri na Zanzibar

DODOMA-Serikali imeeleza kwamba, Uhusiano kati ya Misri na Zanzibar umeendelea kukua na kuimarika licha ya Serikali ya Misri kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar kwenye miaka ya 1990.
Hayo yameelezwa Oktoba 31, 2023 bungeni jijini Dodoma na Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa akijibu Swali la nyongeza la Mhe. Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo, aliyetaka kujua sababu za nchi ya Misri kufunga Ubalozi wake Mdogo Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Waziri alifahamisha kwamba Misri haikutoa sababu za kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar. Hata hivyo, alieleza zaidi kuwa pamoja na kufungwa kwa ofisi hizo, mahusiano na ushirikiano kati ya Misri na Zanzibar yameendelea kukua na kuimarika siku hadi siku kupitia Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam.

Awali, katika suala lake la msingi, Mhe. Mohamed alitaka kujua idadi ya Balozi ndogo zilizopo Zanzibar, ambapo alijibiwa kuwa hadi kufikia Agosti, 2023, nchi zilizofungua Ofisi ndogo za Ubalozi Zanzibar ni China; India; Msumbiji; Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Aidha, Mheshimiwa Naibu Waziri alieleza kuwa suala la kufungua na kufunga Ubalozi ni suala la kawaida katika ulimwengu wa Kidiplomasia.

Alitaja sababu za nchi kufunga Ubalozi kuwa ni pamoja na; Kutetereka au kuharibika kwa mahusiano ya nchi husika; nchi kubadili mwelekeo wa kimaslahi na kistrategia; kukosekana kwa usalama katika nchi husika; na mwisho ni hali ya kiuchumi ambapo nchi hufunga Ubalozi au Konseli Kuu kwa ajili ya kubana matumizi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news