SHILINGI TRILIONI 1.33 KUJENGA BARABARA YA IGAWA-TUNDUMA

SONGWE-Serikali imepanga kuanza ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa (Mbeya) hadi Tunduma (Songwe) yenye urefu wa km. 218 ambao utagharimu sh. trilioni 1.33.

Amesema, mradi huo utahusisha barabara ya mchepuo ya kutoka Inyala - Uyole hadi Songwe yenye urefu wa km. 48 ambayo itapita nje ya Jiji la Mbeya ikiwa ni sehemu ya mradi huo mkubwa.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ruanda, wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe alipopewa nafasi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awasalimie wananchi.

"Tuna mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya kutoka Igawa hadi Tunduma, na ikifika hapa, kutakuwa keep-left kubwa ambayo itaunganishwa na barabara hii ya kutoka Ruanda kwenda Malawi," amesema.

Akielezea kuhusu mradi wa barabara ya Ruanda - Nyimbili - Hasamba - Izilya- Itumba yenye urefu wa km. 79.62, Mhandisi Kasekenya alisema barabara hiyo iko kwenye matengenezo ya mwanzo kabisa lakini utekelezaji wake ni wa kipekee hapa nchini kwa sababu km. 21 za mwanzo zitajengwa na wakandarasi wanne wa kike.

"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kuwa katika kuonesha uwezo walionao, km. 21 za awali, zigawanywe kwenye vipande vya kilometa tano tano na zijengwe na wakandarasi wa kike ambao tunao hadi daraja la kwanza."

Amesema Songwe ni mkoa mpya na hauna barabara za mikoa za lami na kwamba ikikamilika, barabara hiyo itakayokuwa short cut ya kwenda Mbeya, itakuwa ni ya kwanza.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Meneja wa TANROADS wa mkoa huo, Mhandisi Bishanga alisema awamu ya kwanza ya mradi huo itakuwa na km. 21 na hadi sasa wameshaanza kilometa 1.2. Alisema barabara hiyo itakuwa na stendi mbili za abiria na pia itawekwa taa.
Akizungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Songwe aliwataka wakazi wa Ruanda wajenge miundombinu ya sehemu za chakula na malazi ili wageni wapate huduma za uhakika.

"Mgeni anayetoka Malawi hivi sasa atapita hapa. Tujipange kuweka miundombinu ya vyakula na malazi. Tumeambiwa patakuwa na keep-left kubwa hapa, kwa hiyo magari yatakuwa mengi na wageni watakuwa wengi."

Akielezea masuala ya mbolea na VETA ambayo yaligusiwa na wabunge walioambatana naye kwenye ziara hiyo, Waziri Mkuu alimtaka Afisa Kilimo wa Mkoa ahakikishe anapeleka wakala kwenye kijiji cha Ruanda ili wananchi wapate huduma badala ya kuhangaika kwenda Vwawa au Mlowo.

Kuhusu VETA, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wake wa kujenga vyuo hivyo kwenye kila Halmashauri. "Tulianza na Halmashauri 28, na mwaka huu tunazo 48. Kila mwaka tutaendelea kujenga hadi halmashauri zote ziishe," alisisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news