Programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma yatakiwa kuwa endelevu

ARUSHA-Wizara ya Fedha na wadau mbalimbali wa Sekta ya Fedha wameagizwa kuhakikisha Programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma inakuwa endelevu ili kuongeza wigo wa uelewa na utumiaji wa huduma za fedha.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini, Mhe. Felician Mtahengerwa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella , wakati wa kufunga Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yenye kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Uchumi”, yanayofanyika katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Mhe. Mtahengerwa alisema kuwa, elimu ya fedha kwa umma isisubiri Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa kuwa wananchi wengi bado wanahitaji elimu ya kutumia huduma rasmi za fedha.

Vilevile, ameagiza waratibu na wasimamizi wa sekta ya fedha, kufanya tathmini ya matokeo ya Maadhimisho hayo na elimu ya fedha iliyotolewa kwa umma ili kubaini mafanikio na changamoto kwa ajili ya kuongeza ufanisi.

“Ni muhimu sana kufanya tathmini ya matokeo ya maadhimisho haya katika maeneo yaliyowekewa malengo kwa mujibu wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ili kujua iwapo malengo hayo yamefikiwa,"alisisitiza Mhe. Mtahengerwa.

Alisema, maeneo ya kuangalia zaidi ni pamoja na kufahamu ongezeko la uelewa wa wananchi na ushiriki wao katika matumizi ya Huduma za Fedha na namna ambavyo elimu hiyo imewasaidia katika kujiendeleza kiuchumi.

Aidha, amewasihi wananchi kutumia vyema elimu waliyoipata ili kuitumia katika kuboresha maisha kupitia huduma za fedha.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, alisema maadhimisho hayo ni sehemu utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 – 2029/30 ambapo elimu kwa umma ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango huo.

Dkt. Mwamwaja alisema katika maadhimisho hayo elimu inayotolewa ni pamoja na umuhimu wa kutunza fedha binafsi, kukopa kwa malengo, uwekezaji, umuhimu wa bima pamoja na sheria na sera mbalimbali za fedha zinazomlinda mtumiaji wa huduma za fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news