TANZANIA YANUFAIKA KUTOA WALINZI WA AMANI KATIKA MISHENI ZA UMOJA WA MATAIFA

DODOMA-Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ameliambia Bunge kuwa ushiriki wa Tanzania katika Misheni za Ulinzi wa Amani umekuwa na manufaa mbalimbali kwa Taifa ikiwemo mafunzo ya ziada na ajira za kiraia kwa watanzania.

Mhe. Balozi Mbarouk alitoa kauli hiyo Bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi aliyetaka kujua Tanzania inanufaika kiasi gani katika uuzaji wa bidhaa na huduma katika maeneo ambayo Jeshi la Tanzania linafanya ulinzi wa amani.

Balozi Mbarouk amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kwenye jitihada mbalimbali za kutafuta amani duniani kama ilivyoainishwa katika Sera ya Mambo ya Nje 2001 na yapo manufaa makubwa katika ushiriki huo.

“Ushiriki wa Tanzania katika Misheni za Ulinzi wa Amani umekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo; Walinda amani wetu kufaidika na mafunzo ya ziada ambayo yanawajenga na kuwaimarisha,” alisema Balozi Mbarouk

Ametaja faida nyingine nchi inayopata kuwa ni pamoja na ajira za kiraia kwa watanzania na kudumisha utamaduni hususan kukua kwa lugha ya Kiswahili na kutolea mfano katika eneo la DRC, Lebanon na Darfur kumekuwa na ongezeko la matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Mhe. Balozi Mbarouk amesema mbali na manufaa yaliyoainishwa, zipo fursa za kiuchumi ambazo nchi inazipata katika shughuli za ulinzi wa amani.

Balozi Mbarouk ametaja fursa hizo kuwa ni biashara ya bidhaa zinazotumiwa na vikosi vilivyopo katika Misheni kama chakula, mavazi, vinywaji, vifaatiba na dawa.

“Fursa nyingine ni usafirishaji wa mizigo, ujenzi wa majengo yanayohamishika, vifaa na huduma za TEHAMA na kuongeza kuwa Tanzania inaweza pia kuuza teknolojia ya kutumia panya katika kubaini na kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini kama fursa za kiuchumi,”alisema Mhe. Balozi Mbarouk.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news