WAKUU WA NCHI ZA SADC KUKUTANA KWA DHARURA ANGOLA

LUANDA-Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajia kukutana katika mkutano wa dharura Jijini Luanda, Angola tarehe 04 Novemba, 2023.

Mkutano huo unalenga kujadili juhudi za SADC katika kuimarisha hali ya amani, ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia mapigano ya muda mrefu yanayoendelea nchini humo yakitekelezwa na vikundi vyenye silaha katika majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.

Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ataambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo unatarajiwa kusisitiza umuhimu wa utashi wa kisiasa kwa Nchi Wanachama katika kuchangia askari na vifaa vya kijeshi kwa ajili ya Misheni ya Ulinzi wa Amani ya SADC nchini DRC (SAMIDRC), ambapo hadi sasa nchi tatu pekee ndizo zimechangia askari na vifaa vya kijeshi katika misheni hiyo. Nchi hizo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu na Mawaziri vitakavyofanyika tarehe 3 Novemba 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news