UCSAF mbioni kuunganisha barabara zote nchini kwa mawasiliano

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umesema, kwa kushirikiana na watoa huduma mbalimbali nchini wanatarajia kuunganisha njia (barabara) zote nchini hususani maeneo ambayo si rafiki kama Mlima Kitonga na huduma ya mawasiliano.

“Mradi mwingine ambao tunaufanya ni kuhakikisha njia zetu zote zinakuwa na mawasiliano, mwaka 2009 tulipoanza idadi ya watu ambao ilikuwa inapata mawasiliano ilikuwa asilimia 45, lakini hadi sasa tumefikia asilimia 96, ninadhani hata ninyi ni mashaidi ukienda vijijini hata kwenye milima kuna mawasiliano, ingawa kuna yale maeneo machache ambayo tunaendelea kuyafanyia kazi;

Hayo yamebainishwa leo Novemba 21, 2023 jijini Dar es Salaam na Bi.Justina Mashimba ambaye ni Mtendaji Mkuu wa mfuko huo katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria ya Bunge nambari 11 ya mwaka 2006 Sura ya 422.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho ambapo amesema,lengo ni kuwapa elimu na kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu mambo gani ambayo yanaendelea ndani ya taasisi, mashirika pamoja na mafanikio yao ili umma uweze kupata ufahamu wa kutosha kupitia vyombo vya habari nchini.

Lengo likiwa ni kupeleka na kufanikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi waishio katika maeneo machache ya mijini na maeneo mengi yaliyo mbali vijijini yasio na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma ya mawasiliano.

Bi.Mashimba amesema, mwaka 2009 kanuni za kuhuisha Mfuko zilipitishwa na Mfuko kuanza kazi Julai Mosi, 2009.

“Tunashukuru sana Msajili wa Hazina kwa kuweza kuandaa fursa hii ambayo inawezesha umma kufahamu yale ambayo yanafanywa na taasisi za umma kupitia wahariri na wanahabari nchini."
Pia, amemshukuru Mtendaji Mkuu wa kwanza wa taasisi hiyo, Peter Ulanga kwa kujenga msingi imara katika uanzishwaji wa taasisi hiyo ambapo maeneo mengi nchini yameendelea kufikiwa na huduma ya mawasiliano.

“Jukumu la UCSAF ni kupeleka mawasiliano kwa baadhi ya maeneo ya mijini na vijijini.Kwa namna ya kipekee niwashukuru watoa huduma wote wa kampuni za simu ambao wamekuwa mstari wa mbele kupeleka mawasiliano maeneo mbalimbali nchini.”

Amesema, kutokana na ukubwa wa Taifa letu, Serikali iliona ianzishe UCSAF ili kuwezesha mtandao wa mawasiliano uweze kuenea kila kona nchini.

“Kwa takwimu, asilimia 80 ya Watanzania wakati UCSAF inaanza 2006 walikuwa wanaishi vijijini, ndiyo maana Serikali ikaona ianzishe chombo mahususi ambacho kitawezesha kufikisha huduma ya mawasiliano huko.”
Amesema, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mawasilino ya simu, posta, runinga pamoja na redio yanawafikia wananchi kila kona.

“Tunafanya kazi zetu kwa kushirikiana kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika jukumu la kupeleka huduma za mawasiliano vijijini,Kwa hiyo sisi kama UCSAF tunaainisha baadhi ya maeneo ambayo yana changamoto ya mawasiliano.

“Tukishaainisha hayo maeneo sisi kama Serikali tunatoa ruzuku, na tunaingia makubaliano na mtoa huduma ambaye atafikisha huduma hiyo maeneo husika.

“Lakini, kuna maeneo mengine ni magumu sana ambayo hayajafikiwa na mawasiliano, hivyo kwa kuwa Watanzania wanahitaji mawasiliano huwa tunatoa ruzuku kubwa ili kuhakikisha huduma inafika huko.”

“Wale ambao wanachangia mawasiliano kwa njia ya UCSAF ndiyo wanafaidika na ruzuku ambayo Serikali inatoa.”

Amesema, dhamira ya mfuko huo ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu.

“Pia, kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi na serikali katika utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wote katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu,”amesema Mtendaji Mkuu huyo.

Jukumu lingine ni kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu.

“Na kutengeneza mfumo kwa ajili ya upatikanaji wa mitandao ya mawasiliano na huduma rahisi na zenye ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji katika soko la kiushindani.”

Vile vile, mfuko huo unahamasisha utoaji wa huduma bora katika viwango nafuu na kuhakikisha kuwa teknolojia ya habari na mawasilianpo inapatikana vijijini na sehemu za mijini zenye mawasiliano hafifu kwa bei nafuu.

Sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za wote kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kupitia ushiriki wa sekta binafsi.

Amesema, hivi karibuni zaidi ya Watanzania milioni 23.78 watapata huduma ya mawasiliano vijijini. Mtendaji Mkuu huyo amesema, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 326 za ruzuku kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini.

“Huu ni uwekezaji mkubwa ambao umefanyika kwenye miradi vijijini. Ukiwa na kitochi sehemu yenye 2G unaweza kupiga simu popote pale vijijini,”amefafanua.

Ofisi ya Msajili

Kwa upande wkae Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Thobias Makoba amesema, Mfuko wa UCSAF una jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya mawasiliano hususani yale maeneo hafifu ambayo hayajafikiwa.
“UCSAF ni sehemu ya mashirika ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Hazina.Wote tunafahamu kwamba mawasiliano ni sehemu muhimu sana katika jamii, kwa hiyo UCSAF imeangukia katika mashirika yasiyotengeneza faida badala yake wamejikita katika kuwekeza kuhakikisha watanzania wanapata mawasiliano ya uhakika.

“UCSAF kwa kile ambacho wanakifanya kwa sasa ni kuhakikisha kwamba wanawaunganisha Watanzania katika mawasiliano na sisi Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kuhakikisha kuwa, wanafikia malengo yao.

“UCSAF ni non commercial entity haifanyi biashara moja kwa moja, hivyo inahitaji ushirikiano wa kutosha ili waweze kutimiza malengo yao.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news