Usiyoyafahamu kuhusu ujio wa Bima ya Afya kwa Wote

DODOMA-Kamati ya Hudama za Afya na Masuala ya Ukimwi imeipongeza Serikali kwa kuchukua hatua kuandaa na kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote wa mwaka 2022.

Muswada huo unalenga kuweka utaratibu utakaowawezesha wananchi kupata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha.

Hayo yamesemwa ma Mheshimiwa Stanslaus Nyongo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi.

Mhe. Nyongo amesema, sheria inayopendekezwa ni muhimu sana kwa maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Amesema, kutungwa kwa sheria hii kutawawezesha wananchi kunufaika na huduma za afya katika vituo vyote na kuongeza kiwango cha kuishi.

"Serikali ina dhamira ya kutambua ma kugharamia huduma za bima za afya kwa watu wasio na uwezo ambapo kamati ilishauri Serikali kuanzisha mfuko maalum (Equit Fund) ambao utakua na vyanzo mahususi vya fedha na vyenye uhakika,"amesema Mhe.Nyongo.

Aidha, Nyongo ameitaka Serikali kuweka juhudi katika kutoa elimu mara kwa mara kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kijiunga na skimu za bima ya afya, utaratibu wa ugharamiaji wa huduma za afya kwa kutumia bima za afya.

Waziri wa Afya

Akiwasilisha Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na.8 wa Mwaka 20022 bungeni jijini Dodoma Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema, zaidi ya Watanzania milioni 15.8 sawa na kaya zaidi ya milioni 3.6 zinakwenda kunufaika na muswada huo.

Waziri Ummy amesema, hatua hiyo licha ya kuongeza unafuu mkubwa katika huduma za matibabu kwa wananchi pia inakwenda kuondoa malalamiko na kelele za kuzuiwa maiti katika hospitali, hali ambayo huwa inachangamiwa na gharama za matibabu.

"Tunamshukuru Waziri wa Fedha kwa kuridhia vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kwenye mfuko huu, vyanzo ambavyo ni sehemu ya ushuru wa vinywaji, vipodozi na ushuru wa vyombo vya moto, hivyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha,"amesema.

Fuatilia neno kwa neno alichokiwasilisha Waziri Ummy hapa chini;

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha maelezo kuhusu Muswada wa kutunga Sheria
ya Bima ya Afya kwa Wote (Na.8) wa Mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee naomba uniruhusu nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na shupavu kwa nchi yetu katika Nyanja zote.

Sisi katika sekta ya Afya tunajivunia mageuzi makubwa anayofanya katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa watanzania wote bila vikwazo vyovyote.

Vilevile, ameendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini hususani katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi na kutibu magonjwa, kuongeza bajeti kwa ajili ya ununuzi wa dawa na bidhaa nyingine za afya na kuimarisha upatikanaji wa wataalam wa afya katika ngazi zote.

Hakika jitihada za Rais Samia zinaonekana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kipekee tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake alizozianzisha mwaka 2018 ambazo zimewezesha nchi yetu kupunguza Vifo vya Watoto wa umri chini na miaka mitano kwa asilimia 35 kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022.

Aidha, Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 80 kutoka vifo 530 katika kila vizazi hadi 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 katika kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022. Hakika hii ni rekodi ya kutukuka kwa nchi yetu.

Vilevile, nawapongeza Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.

Aidha, nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Dkt. Dotto Mashaka Biteko (Mb) kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza wewe binafsi, kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Mabunge Duniani (InterParliamentary Union) na Rais wa kwanza mwanamke kutoka Bara la Afrika kushika wadhifa huo.

Hii ni fahari na heshima kubwa kwa nchi yetu kwani inaonesha ukuaji wa diplomasia na kielelezo cha imani kubwa ambayo mataifa mengi Duniani wanayo juu ya nchi yetu na wewe mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, niendelee kukupongeza kwa kuongoza vyema Bunge letu na kusimamia vikao na mijadala ndani ya Bunge letu kwa umahiri na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zinazoliongoza Bunge hili.

Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge kwa kukusaidia vyema katika kuliendesha Bunge letu.

Vilevile, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuendelea kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa Kikatiba wa kutunga Sheria pamoja na kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Spika, nimalizie shukrani zangu kwa kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo - Mwenyekiti wa Kamati, na Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndungulile - Makamu Mwenyekiti, kwa ushirikiano na ushauri mzuri waliotupatia wakati wa kupitia Muswada huu mbele ya Kamati hiyo.

Kamati hii ilifanya kazi kubwa ya kuchambua Muswada huu kwa makini, weledi na umahiri mkubwa na kusikiliza na kuchambua maoni yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali walioitwa mbele ya Kamati hiyo na kuishauri Serikali kuboresha Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, naomba kutoa Chimbuko la kuandaliwa kwa Muswada huu wa Bima ya Afya kwa Wote kuwa ni kutimiza wajibu wa Serikali wa Kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.

Aidha, kuwasilishwa kwa Muswada huu ni Utekelezaji wa Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 83 (e) inayotaka kuimarishwa kwa mfumo wa Bima ya Afya nchini ili kufikia lengo la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote.

Mheshimiwa Spika, Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu ya kufikia malengo ya Huduma za Afya kwa Wote (Universal Health Coverage).

Dhana ya huduma za afya kwa wote imejengeka katika Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948; Katiba ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 1948; na kuwekewa viwango vya Kimataifa katika Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 102 wa mwaka 1952 pamoja na pendekezo Na. 202 kuhusu hifadhi ya jamii la mwaka 2012.

Pia, Azimio la Alma Ata la mwaka 1978 (Alma- Ata Declaration of 1978) ambalo limeeleza wazi kwamba, upatikanaji wa huduma za afya ya msingi na yenye ubora ni haki ya kila mtu.

Dhana ya Huduma za Afya kwa Wote imejengeka katika nguzo kuu tatu ambazo ni; uwezo wa kuwafikishia wananchi huduma za afya, upatikanaji wa huduma bora za afya na mfumo madhubuti wa ugharamiaji wa huduma za
afya bila kikwazo cha fedha.

Mheshimiwa Spika, Tangu uhuru Serikali za awamu zote sita zimewekeza katika sekta ya afya kwa kiasi kikubwa ili kuwezesha wananchi wengi kuzifikia huduma za afya ambapo kwa sasa huduma zinapatikana kuanzia ngazi ya
Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya/Halmashauri, Hospital za Rufaa za Mikoa, Hospital za Rufaa za Kanda, Hospital Maalum na Hospitali ya Taifa.

Kutokana na uwekezaji huo, upatikanaji wa huduma za afya nchini umeendelea kumeimarika kuanzia ngazi ya msingi, kati na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuchochea tiba utalii.

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa ugharamiaji huduma za afya ulianza na Sera ya Serikali ya huduma bila malipo mwaka 1960 hadi mwaka 1990 ambapo utaratibu wa wananchi kuchangia huduma za afya ulianza kutumika.

Utaratibu huu ulikua na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi wengi kukosa huduma za afya kutokana na kukosa fedha za kugharamia matibabu papo kwa papo.

Aidha utaratibu huu unawaingiza wananchi wengi hususani wasio na uwezo katika umaskini kutokana na gharama kubwa za matibabu.

Kutokana na changamoto hizo, kuanzia mwaka 2000 Serikali ilianzisha utaratibu wa bima ya afya kwa Mifuko ya bima ya afya ya Umma na Kampuni binafsi za bima ya afya.

Hata hivyo, bado wananchi wengi takribani asilimia 85 wapo nje ya utaratibu huo kutokana na uhiari wa kujiunga na Bima za afya.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Septemba 2023 ni asilimia 15.3 tu ya wananchi wote ndio wapo katika mfumo wa bima ya afya (NHIF 8%; CHF 6%, NSSF-SHIB 0.3% na Bima Binafsi 1%).

Hivyo, Muswada ninaouwasilisha unalenga kuimarisha mfumo wa ugharamiaji huduma za afya kupitia bima ya
afya kwa wote ili kufikia lengo la huduma bora za afya kwa wote.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022.

Lengo la kutungwa kwa Sheria inayopendekezwa ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote kupitia mfumo wa bima ya afya na kuweka mfumo wa ushiriki katika skimu za bima ya afya kwa raia na wakazi wote.

Utaratibu unaopendekezwa utawezesha mwananchi kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha pindi anapohitaji huduma hizo na kumwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na hivyo kumuepusha mwananchi kuingia katika janga la umaskini.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Tisa. Sehemu ya Kwanza inahusu masharti ya utangulizi ambapo Kifungu cha Kwanza kinahusu Jina na kuanza kutumika kwa Sheria.

Kifungu hiki kimempa Waziri Mamlaka ya kubainisha tarehe za kuanza kutumika kwa Vifungu mbalimbali vya Sheria ili kutekeleza mfumo wa Bima ya Afya kwa wote.

Kifungu cha Pili kinaainisha mipaka ya matumizi ya Sheria hii. Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 3 kinaweka masharti kuhusu tafsiri ya misamiati mbalimbali iliyotumika katika Sheria kwa lengo la kuweka maana iliyokusudiwa na kuondoa utata wa tafsiri unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa Sheria hii.

Aidha, Serikali inapendekeza kifungu hicho kifanyiwe marekebisho kwa kuondoa na kuongeza misamiati kama inavyobainishwa katika Aya C ya Jedwali la Marekebisho.

Kifungu cha 4 kimeainisha Malengo ya Sheria hii ambayo ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.

Lengo la kifungu hiki ni kuweka misingi ya kuzingatiwa wakati wa usimamizi na utekelezaji wa Sheria hii. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Pili inaweka masharti kuhusu Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.

Kifungu cha 5 kinaweka wajibu wa ushiriki wa kila mtu katika Mfumo wa Bima ya Afya. Aidha, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu hiki kwa lengo la kuweka ulazima wa kila mtu kujiunga na Bima ya Afya kama inavyoainishwa katika Aya D ya Jedwali la Marekebisho.

Kifungu cha 6 kinapendekeza kuanzisha Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo makundi mbalimbali yatajumuishwa na kushiriki katika Skimu za Bima ya Afya.

Makundi hayo ni pamoja na Waajiri, Watumishi wa Umma, Wafanyakazi walioajiriwa katika sekta binafsi, waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi na wananchi wasio na uwezo.

Washiriki wengine katika mfumo wa bima ya afya ni skimu za bima ya afya, vituo vya kutolea huduma za afya na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tanzania Insurance Regulatory Agency - TIRA).

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 7 kinaainisha majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tanzania Insurance Regulatory Authority-TIRA) katika kudhibiti na kusimamia mfumo wa bima ya afya nchini.

Kwa mujibu wa kifungu hiki, Mamlaka hiyo, pamoja na mambo mengine, itakuwa na wajibu wa kusajili na kudhibiti skimu za bima ya afya; kuhakikisha kuwa kila skimu ya bima ya afya inatoa kitita cha mafao ya huduma muhimu (Standard Benefit Package) kwa mujibu wa Sheria hii; na kutoa miongozo kuhusiana na uendeshaji wenye tija na ufanisi wa shughuli za skimu za bima ya afya.

Lengo la usimamizi na udhibiti wa bima ya afya ni kuhakikisha ufanisi wa utoaji wa huduma za bima ya afya. Serikali inapendekeza marekebisho katika kifungu hiki kama ilivyoainishwa katika Aya E ya Jedwali
la Marekebisho.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tatu inaweka masharti kuhusiana na skimu za bima ya afya. Kifungu cha 8 kinatambua uwepo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kama skimu ya bima ya afya ya umma.

Aidha, kifungu hiki kimempa mamlaka Waziri kuboresha skimu ya bima ya afya ya umma. Lengo la kifungu hiki ni kuendelea kuboresha huduma za bima ya afya katika skimu ya bima ya afya ya Umma kwa kuzingatia matokeo ya tafiti na tathmini mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 9 kinaweka utaratibu wa kampuni binafsi kusajiliwa kama skimu za bima ya afya binafsi baada ya kutimiza vigezo na masharti yatakayoainishwa katika Kanuni zitakazotungwa chini ya Sheria
inayopendekezwa.

Dhumuni la kifungu hiki ni kuwawezesha wananchi kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya Skimu ambazo watapenda ziwahudumie na kupanua wigo wa uwepo wa skimu za bima ya afya ili kuongeza fursa ya ushiriki kwa lengo la kukuza ushindani na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za Bima ya Afya nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza kufutwa kwa kifungu cha 10 kama inavyoonekana katika Aya F ya jedwali la marekebisho.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 11 kinaweka katazo la uendeshaji wa skimu za bima ya afya bila kusajiliwa. Lengo ni kuhakikisha kuwa skimu zote za bima ya afya za umma na binafsi nchini zinasajiliwa na kuendeshwa kwa mujibu wa Sheria inayopendekezwa.

Kifungu cha 12 kinaipa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima jukumu la kutunza Rejesta ya Skimu za Bima ya Afya zilizosajiliwa chini ya Sheria inayopendekezwa ili kuwezesha uratibu na usimamizi wa Skimu hizo.

Aidha, Kifungu cha 13 kinaweka utaratibu ambao Mamlaka ya Usimamizi wa Bima itaufuata ikiwa inataka kufuta usajili wa skimu ya bima ya afya na hatua zitakazochukuliwa iwapo skimu ya bima ya afya itataka kujiondoa katika utoaji wa huduma za bima ya afya.

Dhumuni la kifungu hiki ni kuhakikisha kuwa watoa huduma za bima ya afya wanafuata utaratibu wa kujiondoa au kuondolewa katika shughuli ya utoaji wa huduma za bima ya afya ili kulinda haki na maslahi ya wanachama na watoa huduma za afya.

Aidha, Serikali katika Aya G ya Jedwali la Marekebisho inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu hiki kwa kuongeza utaratibu wa kuzingatiwa kabla ya skimu ya bima ya afya kufutiwa usajili kwa lengo la kulinda maslahi ya wanachama na watoa huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne inaweka masharti kuhusu vitita vya mafao. Kifungu cha 14 kinaweka ulazima kwa skimu za bima ya afya kutoa kitita cha mafao ya huduma muhimu (Standard Benefit Package) kwa wanufaika.
Aidha, kifungu hiki kinatoa fursa kwa wanachama kupata kitita cha mafao ya ziada kinachojumuisha huduma zaidi ya zilizomo katika kitita cha mafao ya huduma muhimu.

Lengo la kifungu hiki ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama anapata huduma za kitita cha mafao ya huduma muhimu kwa usawa, na kutoa fursa ya upatikanaji wa huduma za ziada pale ambapo mwanachama atahitaji.

Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu hiki kama inavyobainishwa katika Aya I ya Jedwali la Marekebisho.

Mheshimiwa Spika, Kama ilivyoainishwa katika Aya J ya Jedwali la marekebisho, Kifungu cha 15 kimefutwa na kuandikwa upya kwa kuainisha huduma za afya zilizojumuishwa katika kitita cha mafao ya huduma muhimu.

Vilevile, kifungu hiki kinampa Waziri mamlaka ya kufanya marekebisho ya kitita hicho kwa kuzingatia matokeo ya tathmini na uendelevu wa Skimu za bima ya afya. Dhumuni la kifungu hiki ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wanachama wote.

Mheshimiwa Spika, katika kufikia lengo la Bima ya Afya kwa Woe na kwa kutambua uzoefu na uwekezaji uliofanywa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kama inavyobainishwa katika Aya K ya Jedwali la marekebisho kwa kuanzisha kitita cha bima ya afya cha jamii (Community Health Insurance Package – CHIP) ikiwa ni mpango mbadala wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo Sheria iliyoanzisha Mfuko huo inapendekezwa kufutwa na kuianzisha upya chini ya sheria hii.

Lengo la kuanzishwa kwa kitita hicho ni kuhakikisha wananchi wote wanajumuishwa katika utaratibu wa bima ya afya ili kupata huduma bora za afya pasipo vikwazo wanavyokutana navyo sasa. Vikwazo hivyo ni pamoja
na:

(i) Wananchi kutopata huduma za afya wanapokuwa nje ya maeneo waliyojiandikisha na hivyo kulazimu kulipia huduma za afya kwa utaratibu wa papo kwa papo hali inayoathiri shughuli za kijamii na kiuchumi;

(ii) Wigo mdogo wa kuchangiana kati ya Mikoa na Halmashauri zenye uchumi mkubwa na mdogo, wananchi wenye kipato kikubwa na kidogo na wagonjwa na wasio wagonjwa kutokana na kusimamiwa katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa;

(iii) Ufinyu wa huduma katika kitita cha mafao kinachotolewa na hivyo kukosekana kwa huduma muhimu mathalani huduma za afya ya kinywa na meno, kutojumuishwa kwa baadhi ya dawa na hivyo kumlazimu mwanachama kulipia
(iv) Muundo wa CHF kutokidhi misingi na kanuni za uendeshaji wa bima ya afya mathalani kutotenganisha kwa majukumu kati ya mnunuzi na mtoa huduma za afya; na

(v) Uhiari wa wananchi kujiunga unaosababisha wananchi kujiunga wakiwa wagonjwa. Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 16 kinaweka utaratibu wa utoaji wa kitita cha mafao ya ziada kama itakavyoidhinishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima kwa kuzingatia uhitaji.

Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kupitia Aya M ya Jedwali la marekebisho kwa kufuta Kifungu cha 17 na maudhui ya kifungu hicho kuwekwa katika kifungu kipya kama inavyobainishwa katika Aya N ya Jedwali la marekebisho.

Lengo la kifungu hiki ni kutoa wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyoingia mkataba na skimu za bima ya afya kwa lengo la kuhakikisha wanufaika wanapata huduma kwa utaratibu
utakaowekwa.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tano inaweka masharti kuhusu uanachama na uchangiaji katika skimu za bima ya afya.

Kifungu cha 18 kinaainisha watu wanaopaswa kujiunga na skimu za bima ya afya na kuweka wajibu wa kila mtu kujiunga.

Kifungu cha 19 kinabainisha aina na idadi ya watu wanaoweza kujumuishwa katika skimu za bima ya afya kama wategemezi wa mwanachama mchangiaji.

Kifungu cha 20 kinaweka utaratibu wa usajili wa wanachama ambapo waajiri katika sekta za umma na binafsi watatakiwa kuwasajili waajiriwa wao ndani ya siku 30 toka kuanza kwa mkataba wa ajira.

Aidha, kila mtu katika sekta rasmi na isiyo rasmi atatakiwa kujiunga na skimu ya bima ya afya kwa utaratibu utakaoainishwa katika kanuni.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 21 kinaweka viwango vya uchangiaji kwa wanachama kutoka sekta ya umma, sekta rasmi binafsi na sekta isiyo rasmi.

Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Kifungu hiki kwa kubainisha kuwa mchango wa asilimia sita wa mshahara utakuwa kwa ajili ya mwajiri wa sekta ya umma na mwajiri wa sekta rasmi binafsi atakayechagua kuwasajili waajiriwa wake katika skimu ya bima ya afya ya umma kama ilivyoainishwa katika mapendekezo ya mabadiliko katika Aya O ya Jedwali la marekebisho.

Kwa muktadha wa Sheria hii mshahara wa sekta ya Umma na sekta rasmi binafsi, umetafsiriwa kwa maana sawa na ile inayotumika na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa sekta zote mbili mtawalia.

Dhumuni la kifungu hiki ni kuwa na maana zinazofanana na kuhakikisha uwepo wa uwiano katika uchangiaji wa Kitita cha mafao ya Huduma Muhimu.

Vilevile, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu hiki kwa kutoa uhuru kwa waajiri wa sekta rasmi binafsi kuchagua skimu ya bima ya afya ya umma au binafsi kuwasajili waajiriwa wao.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 22 kinaweka utaratibu wa utambuzi na usajili wa kundi la watu wasio na uwezo kwa lengo la kuhakikisha wanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha kwa utaratibu utakaowekwa na Serikali, ambapo kundi hili litajumuishwa chini ya skimu ya bima ya afya ya Umma kwa namna itakavyoainishwa kwenye kanuni.

Aidha, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya kifungu hiki kama inavyobainishwa katika Aya P ya Jedwali la marekebisho. Ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kundi hilo, Serikali inapendekeza kuanzishwa Mfuko wenye lengo la kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

Aidha, Mfuko utaweza kutumika kugharamia huduma za matibabu kwa magonjwa sugu na ya muda mrefu kama vile saratani na magonjwa ya figo na huduma za dharura zitokanazo na ajali kama inavyobainishwa katika Aya Q.

Vyanzo vya Mfuko huo ni pamoja na sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vyenye kaboni (carbonated drinks), Vinywaji vikali (Liqour), bidhaa za vipodozi (Cosmetic Products), Kodi ya michezo ya kubahatisha, Ada ya bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki (Eletronic Transaction Levy) kwa kadri itakavyopendekezwa na Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha,fedha zitakazotengwa na Bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko; na zawadi na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali.

Kipekee nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kuhakikisha kuwa watu wasio na uwezo wanapata huduma bora za afya bila kikwazo chochote, hakika historia ya Tanzania na Dunia itamkumbuka.

Mheshimiwa Spika, Kipekee tunaishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI, kwa kuweka msisitizo wa umuhimu wa kuwa na Mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.
 
Hili tutalisimamia kikamilifu kwa kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wanapata huduma bora za afya.

Katika kuwatambua watu wasio na uwezo mapendekezo ya Serikali ni kuboresha mifumo ya utambuzi wa watu kwa kutumia Mamlaka zilizopo.

Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (Household Budget Survey – HBS) wa mwaka 2017/18 zinaonyesha kuwa asilimia 26.4 ya watu wote Tanzania Bara ni wananchi wasio na uwezo.

Kwa kuzingatia utafiti huo asilimia 26.4 ya takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 (59,851,347) idadi wa wananchi wasio na uwezo ni 15,800,756 sawa na kaya 3,637,121.

Aidha wananchi wasio na uwezo na ambao wanaishi katika umaskini uliokithiri ni 4,044,843 ambao ni asiliia 8 sawa na kaya 1,113,513.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 23 kinaweka sharti kwa skimu za bima ya afya kuweka na kutunza amana katika Benki Kuu ya Tanzania ambayo itatumika kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanachama waliosajiliwa chini ya skimu husika hawaathiriki endapo skimu hizo zitashindwa kuendelea kutoa huduma kwa wanufaika wake kutokana na sababu mbalimbali.

Aidha, Serikali inawasilisha mapendekezo yaliyoainishwa katika Aya R ya Jedwali la Marekebisho yanayobainisha jukumu hili kutekelezwa kupitia Sheria ya Bima, Sura ya 394.

Kifungu cha 24 kinaweka utaratibu wa utambuzi wa wanachama na wanufaika kwa lengo la kupata taarifa zitakazowezesha uhakiki wa wanachama na kudhibiti udanganyifu.

Kifungu cha 25 kinaweka masharti kuhusiana na ukomo wa uanachama ambapo uanachama utafikia ukomo iwapo mwanachama atafariki au ataacha kuchangia katika skimu ya bima ya afya.

Hata hivyo, kifungu kinabainisha kuwa wategemezi wa mwanachama aliyefariki, wataendelea kupata huduma kwa kipindi kitakachobainishwa na Waziri mwenye dhamana katika Kanuni.

Dhumuni la kifungu hiki ni kulinda haki za wategemezi wa mwanachama. Vilevile, Serikali inapendekeza kuongeza sababu za ukomo wa uanachama kama ilivyoainishwa katika Aya S ya Jedwali la Marekebisho.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Sita inaweka masharti kuhusu udhibiti ubora wa huduma zitolewazo na vituo vya kutolea huduma za afya na skimu za bima ya afya.

Kifungu cha 26 kina lengo la kuhakikisha skimu za bima ya afya zinazingatia ubora katika utoaji wa huduma za bima ya afya kulingana na miongozo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima.

Kifungu cha 27 kinaipa Wizara jukumu la kuhakikisha kuwa vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoingia mikataba na skimu za bima ya afya za umma na binafsi vinatoa huduma bora za afya kwa wanufaika kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyotolewa na Wizara kama inavyopendekezwa katika Aya T ya Jedwali la marekebisho.

Dhumuni la kifungu hiki ni kuhakikisha vituo vinatoa huduma bora za afya kwa wananchi kupitia mfumo wa Bima ya Afya.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Saba inaweka masharti mengineyo ambayo kwa namna moja au nyingine yatahusika katika utekelezaji wa masharti ya Sheria hii.

Kwa kuwa uendeshaji wa skimu utazingatia kanuni za uendeshaji wa bima za afya, Kifungu cha 28 kinaitaka kila skimu ya bima ya afya ya umma na binafsi kufanya tathmini ya uhai na uendelevu wake kila baada ya miaka mitatu au wakati wowote itakavyoelekezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na taarifa ya tathmini kuwasilishwa kwa Mamlaka hiyo pamoja na Waziri.

Kifungu hiki kinaipa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya skimu kutokana na upungufu utakaobainishwa na taarifa ya tathmini ya uhai na uendelevu.

Dhumuni la kifungu hiki ni kuhakikisha skimu za bima ya afya zinakuwa na ukwasi na uendelevu wa kutoa huduma kwa wanufaika.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 29 kinaruhusu skimu za bima ya afya za umma na binafsi kufanya uwekezaji kwa lengo la kukuza mtaji na hivyo kuimarisha uhai na uendelevu wake.

Aidha, Kifungu cha 30 kinaipa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima jukumu la kutoa miongozo kuhusiana na ukomo wa gharama za uendeshaji wa skimu za bima ya afya ili kuhakikisha skimu hizo zinakuwa na uwezo wa kujiendesha na kusimamia utekelezaji wa majukumu yake bila kuathiri utoaji wa huduma za bima ya afya kwa wanachama wake.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa haki za wanufaika na watoa huduma katika mfumo wa bima ya afya zinalindwa, Kifungu cha 31 kinaweka utaratibu wa namna ambavyo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima
itakavyoshughulikia malalamiko.

Mheshimiwa Spika, Kufuatia maoni na ushauri wa wadau mbalimbali pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Serikali, kupitia Aya W ya Jedwali la Marekebisho, inapendekeza kukifuta kifungu cha 32 kilichokuwa kimefungamanisha huduma mbalimbali za kijamii na bima ya afya.

Huduma zilizokuwa zimefungamanishwa ni pamoja na leseni ya udereva, bima za vyombo vya moto, viza ya kuingilia nchini, utambulisho wa mlipa kodi, Usajili wa Laini za Simu, hati ya kusafiria, uandikishaji wa wanafunzi kidato cha tano na cha sita na utoaji wa kitambulisho cha Taifa.

Mheshimiwa Spika, Hata hivyo ni lengo ya Serikali kuwa kila mtu nchini awe na bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

Baada ya Sheria hii kupitishwa, Serikali itaendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kuhusu dhana na umuhimu wa bima ya afya lengo likiwa ni kuwaepusha wananchi kuingia katika umaskini.

Tunayo mifano iliyo hai ya wananchi ambao walilazimika kuuza mali zao ikiwemo mashamba, mifugo, vyombo vya usafiri, vifaa vya ndani na kuweka rehani mali zao ili kugharamia matibabu yao au ya wapendwa wao.

Aidha Seerikali itaendelea kuboresha huduma za afya katika ngazi zote ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 33 kinampa Waziri mamlaka ya kutunga Kanuni kwa masuala mbalimbali kwa lengo la kutekeleza sheria inayopendekezwa kwa ufanisi.

Aidha Kifungu cha 34 kinaweka katazo kwa wanufaika, vituo vya kutolea huduma za afya na skimu za bima ya afya na
mtu yeyote kutoa taarifa za uongo na kuweka adhabu iwapo watathibitika kufanya hivyo.

Dhumuni la kifungu hiki ni kulinda uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya kwa kuzuia masuala ya udanganyifu na ubadhirifu wa pesa za wanachama ili kuhakikisha huduma za bima ya afya zinazotolewa zinakidhi vigezo na ni endelevu.

Aidha, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu hicho kwa kutenganisha adhabu ya Skimu ya Bima ya afya na vituo vya kutolea huduma za afya, kuongeza kiwango cha kulipa faini,kuongeza sharti la ulipaji wa fidia kwa hasara iliyosababishwa na kuweka adhabu kwa wataalam, kama inavyobainishwa katika Aya Y ya Jedwali la
Marekebisho.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maoni ya kutokufungamanisha huduma za kijamii na bima ya afya na katika kuhakikisha ulazima wa kuwa na bima ya afya unatekelezwa, Serikali katika Aya Z ya Jedwali la marekebisho inapendekeza kufanya marekebisho kwa kuweka adhabu ya asilimia 10 ya mchango wa kila mwaka kwa mtu yeyote ambaye hatajiunga na bima ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu tangu kuanza kutekelezwa kwa Sheria
inayopendekezwa.

Hata hivyo, Waziri amepewa mamlaka ya kutoa msamaha wa ulipaji wa adhabu ya asilimia 10 kwa kuzingatia maslahi ya umma au sababu nyingine yoyote.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 35 kinaweka utaratibu wa kushughulikia madai ya skimu za bima ya afya ambapo mahakama ina uwezo wa kuamuru ulipwaji wa fidia iwapo kosa litathibitika kutendwa na mwanachama au mtu
yoyote.

Vilevile, Kifungu cha 36 kinatoa adhabu ya jumla kwa makosa ambayo adhabu mahsusi haijatolewa chini ya Sheria inayopendekezwa.

Dhumuni la kifungu hiki ni kuweka utaratibu wa kushughulikia makosa yote ambayo hayajawekewa adhabu mahsusi katika Sheria. Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya kutenganisha adhabu kati ya mtu binafsi na taasisi
kama inavyobainishwa katika Aya AA ya Jedwali la Marekebisho.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 37 kinaweka utaratibu wa uwajibishwaji wa chombo hodhi pamoja na watendaji kwa makosa yatakayofanywa chini ya Sheria inayopendekezwa kwa lengo la kuweka utii wa Sheria.

Kifungu cha 38 kinaweka ukuu wa Sheria inayopendekezwa na sheria nyingine katika masuala yanayohusu uendeshaji na usimamizi wa mfumo wa bima ya afya nchini.

Lengo la kifungu hiki ni kuondoa ukinzani wa sheria baina ya Sheria hii na sheria nyingine yoyote inayohusiana na masuala ya bima ya afya.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nane inaainisha masharti kuhusu Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii, masharti ya mpito na masharti yanayoendelea.

Kifungu cha 39 kinafuta Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii na wanufaika wataendelea kupata huduma kupitia kitita cha bima ya afya cha Jamii (Community Health Insurance Package – CHIP) kama inavyobainishwa katika Aya BB ya Jedwali la Marekebisho.

Kifungu hiki pia kinabainisha masharti yatakayoendelea kutekelezwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii ili kulinda haki za wanufaika wake.

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kuchukua hatua hii ni Muundo wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kutokidhi misingi na kanuni za uendeshaji wa bima ya afya mathalani, Mfuko wa Afya ya Jamii una wigo mdogo wa kuchangiana kati ya Mikoa na Halmashauri zenye uchumi mkubwa na mdogo, wananchi wenye kipato kikubwa na kidogo na wagonjwa na wasio wagonjwa kutokana na kusimamiwa katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa,wanufaika kutoweza kupata huduma za afya nchi nzima isipokuwa katika Halmashauri walizojiandikisha tu.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ni ufinyu wa huduma katika kitita cha mafao kinachotolewa na hivyo kukosekana kwa huduma muhimu mathalani huduma za afya ya kinywa na meno, kutojumuishwa kwa baadhi ya dawa na hivyo kumlazimu mwanachama kulipia.

Vilevile, wananchi kutopata huduma za afya wanapokuwa nje ya maeneo waliyojiandikisha na hivyo kulazimu kulipia huduma za afya kwa utaratibu wa papo kwa papo hali inayoathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 40 kinaweka masharti kuhusiana na kipindi cha mpito kisichozidi miezi kumi na miwili tangu kuanza kutumika kwa Sheria inayopendekezwa ambapo wadau wote watapaswa kutekeleza masharti ya
Sheria hiyo.

Vilevile, Kifungu hicho kinampa Waziri mamlaka ya kuongeza kipindi cha ziada cha mpito kisichozidi miezi sita baada ya kipindi cha awali cha mwaka mmoja kupita.

Lengo la kifungu hiki ni kuhakikisha uendelevu wa huduma kwa wanachama walio kwenye skimu mbalimbali na kuwawezesha wadau mbalimbali kufanya maandalizi na kukamilisha taratibu za utekelezaji wa Sheria inayopendekezwa.

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tisa inabainisha Sheria mbalimbali zitakazofanyiwa marekebisho baada ya Muswada huu kupita.

Sheria hizo ni Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura ya 395; Sheria ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135; Sheria ya Bima, Sura ya 394; Sheria ya Mtoto, Sura ya 13; Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366; Sheria ya Udhibiti wa Hospitali Binafsi, Sura ya 151; na Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kutoa ufafanuzi kuhusu sababu za kufanya marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Sura ya 50.

Marekebisho haya yanalenga kuendelea kutoa fao la matibabu kwa wanufaika wake kama fao la afya na sio bima ya afya.

Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha Sheria inayopendekezwa inatekelezwa kwa ufanisi Serikali imejipanga kutoa elimu kwa umma kuhusu dhana na umuhimu wa bima ya afya. Utoaji wa elimu kwa umma utatekelezwa kupitia Mkakati wa Utoaji wa Elimu kwa Umma unaobainisha jumbe mahususi zinazotakiwa kutolewa, ushirikishaji wa wadau mbalimbali hususan viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, pamoja na viongozi katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Elimu kwa umma itatolewa kabla na wakati wa utekelezaji wa Sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, tunatambua pia kuwa utekelezaji wa Sheria inayopendekezwa na utayari wa wananchi kujiunga na Skimu za Bima ya afya unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya zinazotolewa kwa wananchi wenye bima ya afya.

Hivyo huduma za afya zikiwa bora zitawavutia wananchi wengi kujiunga na skimu za bima ya afya.Katika kutambua hilo, Serikali itahakikisha huduma bora za afya zinapatikana katika ngazi zote.

Kwa mfano katika kipindi cha takriban miaka mitatu vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka vituo 8,449 mwaka (2019) hadi kufikia vituo 11,630 mwezi Septemba, 2023, sawa na ongezeko la Vituo 3,181.

Vilevile, upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya umeimarika kutoka asilimia 62 mwezi Agosti, 2022 hadi kufikia asilimia 73 (mwezi Agosti, 2023).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umefanyika uwekezaji mkubwa katika vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi wa
magonjwa na matibabu ikiwemo X-rays (199), CT-Scan (30), MRI (4) ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa Idara ya Wagonjwa wa Dharura (EMD) (111) na Wodi za Wagonjwa Muhtuti (ICU) (73) hadi katika ngazi ya Hospitali za
Halmashauri.

Uwepo wa hatua hii katika vituo vya kutolea huduma za afya kumesogeza huduma za kiuchunguzi karibu zaidi na wananchi na kuwapunguzia gharama waliyokuwa wakitumia kufuata huduma hizo katika Hospitali za Taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kuongeza rasilimali watu katika sekta ya Afya, ambapo Mwaka 2020/2021 iliajiri watumishi wa afya 3,347,Mwaka 2021/2022 watumishi 10,285 na mwaka 202/23 watumishi 8,8277
waliajiriwa.

Vilevile, katika mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha Shilingi bilioni tisa (9) zimetengwa kwa ajili ya ufadhili wa mafunzo ya Ubingwa na Ubingwa Bobezi kwa watumishi wa Afya wa Serikali.

Aidha, tutaendeleza jitihada za kuhakikisha watumishi wa afya wanatoa huduma kwa kuzingatia Weledi na Maadili.

Mheshimiwa Spika, katika kuwezesha utoaji wa huduma bora za bima ya afya kwa wananchi, Serikali pia itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA.

Ili kuwezesha utekelezaji wa Sheria hii, tutazitaka skimu za bima ya afya kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za bima ya afya ikiwemo usajili na utambuzi wa wanachama na vituo vya kutolea huduma za afya na utekelezaji wa majukumu ya skimu hizo.

Hatua hii pia itasaidia kudhibiti udanganyifu na vitendo vya ubadhirifu ambapo fedha nyingi hupotea na hivyo kuzifanya skimu za bima ya afya kutokuwa endelevu.

Serikali itahakikisha kwamba mfumo wa bima ya afya unasimamiwa ipasavyo, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) ambayo itahakikisha haki na wajibu wa mwanachama, mtoa huduma na skimu za bima ya afya
zinatekelezwa kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha maelezo yangu kuhusu Muswada huu, naomba kutoa kwa ufupi manufaa ya kutungwa kwa sheria hii ambayo ni pamoja na; Kundi kubwa la wananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha; kuimarisha Uboreshaji wa huduma katika Vituo vya kutolea huduma za afya vya Umma na binafsi, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba; kuimarika kwa Uhimilivu na ustahimilivu wa Skimu za bima ya afya kutoa huduma kwa kuwa wananchi watapaswa kujiunga na Skimu za Bima ya Afya kabla ya kuwa ni wagonjwa; Kuimarika kwa usimamizi na udhibiti katika utoaji wa huduma za Bima ya Afya zitolewazo na Mifuko na Kampuni Binafsi za Bima ya Afya; Kuboreshwa kwa vitita vya mafao vinavyotolewa na skimu za bima ya afya na Kuimarisha hali ya kipato kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, athari zitakazoendelea kujitokeza endapo Sheria hii haitatungwa ni pamoja na; Wananchi kujiunga kwa hiari na wakiwa tayari ni wagonjwa na hivyo kuondoa dhana ya kuchangiana gharama za matibabu;

Kudhoofisha uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya zilizopo; Kundi kubwa la wananchi kuwa nje ya mfumo wa bima ya afya (asilimia 85) hivyo kuwa katika hatari ya umaskini; Wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizwa (NCDs);

Kukosekana kwa Udhibiti Madhubuti wa utoaji wa huduma katika soko la bima ya afya na Serikali kushindwa kufikia lengo la Afya Bora kwa Wote.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu, naomba nisisitize kuwa,Bima ya Afya ndio mfumo bora, rahisi na endelevu ambao umethibitika katika nchi mbalimbali duniani kuwawezesha wananchi wengi hususani wa kipato
cha chini kupata huduma bora za afya pindi wanapozihitaji.

Wengi tunafahamu kuwa pale familia inapokuwa na mgonjwa basi huuza mali zao ili kupata fedha za kulipia gharama za matibabu. Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote kujiunga na Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa
matibabu kabla ya kuugua.

SHUKRANI

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshukuru sana Mhe. Dkt.Godwin Mollel (Mb.), Naibu Waziri wa Afya kwa ushirikiano anaoendelea kunipa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yangu hasa katika kipindi
cha maandalizi ya Muswada huu.

Aidha, ninawapongeza watumishi wote wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Dkt. John A.K. Jingu, Katibu Mkuu, Dkt.Grace E. Magembe, Naibu Katibu Mkuu na Prof. Tumaini J. Nagu, Mganga Mkuu wa Serikali. Kwa mara nyingine tena nimshukuru Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuongoza vyema katika mchakato huu, Mhe. Jenista J. Mhagama (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa uratibu na ushirikiano wake katika maandalizi ya Muswada huu.

Kipekee nitambue mchango wa Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), Waziri wa Fedha, kwa ushirikiano wake katika kipindi chote cha maandalizi ya muswada huu hususan katika kuwezesha upatikanaji wa vyanzo vya fedha kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

Kwa namna ya pekee pia ninamshukuru Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ndugu Onorius Njole, Mwandishi Mkuu wa Sheria na watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano walioutoa wakati wa Maandalizi ya Muswada huu.

Vilevile, niwashukuru wataalam kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wote wa sekta ya afya waliotoa ushauri, maoni na mapendekezo yaliyowezesha maandalizi ya Muswada huu.

Mwisho na si kwa umuhimu nitambue taasisi zifuatazo:- TASAF, APHTA, TEA, Kampuni binafasi za Bima ya Afya, TIRA, NHIF, NBS na NSSF.

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie tena kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI. Nimalizie kwa kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kwa kunipa fursa ya kuwasilisha Muswada huu na nichukue nafasi hii kuliomba Bunge lako Tukufu liujadili Muswada huu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Na.8) wa Mwaka 2022 na kuupitisha katika hatua ya Kusomwa kwa Mara ya Tatu na hatimaye Sheria inayopendekezwa kuwa sehemu ya Sheria za Nchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Ummy Ally Mwalimu (Mb.)
WAZIRI WA AFYA
01 NOVEMBA, 2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news