Waweka kambi Musoma kusikiliza mashauri ya rufani

NA FRESHA KINASA

MAHAKAMA ya Rufani ya Tanzania imeendelea na vikao vya kusikiliza mashauri ya rufani katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma ambapo hatua hiyo inalenga kupunguza idadi ya mashauri hayo yaliyopo katika kanda hiyo.

Vikao hivyo vya kusikiliza mashauri hayo vinaongozwa na Jaji Mwanaisha Kwariko ambaye ni Mwenyekiti na wenzake Jaji Zephrine Galeba na Jaji Paul Kihwelo.

Akizungumza na waandishi wa habari Novemba Mosi, 2023 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Rashid Chaungu amesema kuw,a vikao hivyo vimeanza tangu Oktoba 30, 2023 na mwisho itakuwa Novemba 17, 2023.

Rashid amesema kuwa, vikao hivyo ni vya mara ya pili ambapo vikao vya awali vimekwishafanyika mwezi Juni, 2023.

Huku akisema mashauri yaliyopangwa kusikilizwa na jopo hilo la Majaji katika vikao vinavyoendelea awamu hii ni mashauri 32, ambapo rufani za jinai ziko 24 na maombi ya madai yakiwa nane.

Ameongeza kuwa, tangu Oktoba 30, 2023 hadi Novemba Mosi, 2023, jumla ya kesi za rufani 19 zimesikilizwa ambapo kati ya kesi hizo kesi tisa zimeisha kabisa kwa kutolewa uamuzi na kesi 10 zinasubiri kutolewa uamuzi.

Leonard Magwayega ni Wakili wa kujitegemea anayeishi Manispaa ya Musoma amesema kuwa, hatua hiyo ya Majaji kuendesha vikao vya kusikiliza mashauri ya rufani katika Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imekuwa na faida kubwa kwa wananchi ikiwemo kuwawezesha kupata haki mapema.

"Hii ni hatua ya kupongezwa kwani inaleta ahueni kubwa kwa wananchi ambao zamani kabla ya kujengwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma walilazimika kwenda Mwanza, lakini hivi sasa uwepo wa mahakama hii ya Kanda ya Musoma imewezesha vikao vya rufani kuja kufanyika hapa na hivyo wananchi kuondokana na usumbufu."

Stella Elias mkazi wa Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kwa hatua ya kuleta vikao hivyo vya kusikiliza rufani, kwani vinawanufaisha wananchi na kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa haki kwa weledi na haraka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news