Wachangiaji wa Mfuko wa Elimu wana nafasi ya kupata nafuu ya kodi-TEA

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imesema kuwa,kuna faida kubwa kwa watu au taasisi zinazochangia Mfuko wa Taifa wa Elimu nchini kupitia mamlaka hiyo.

Hayo yamesemwa leo Novemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt.Erasmus Kipesha katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Ukichangia elimu kupitia Mfuko wa Elimu tutakupa cheti ambacho unaweza kukipeleka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ukapata nafuu ya kodi.

“Lakini, pia ukichangia Mfuko wa Elimu tutakutangaza na kukuingiza katika daftari maalum.Kwa hiyo mkija kuchangia elimu kupitia Mfuko wa Elimu kuna manufaa mengi mno.”

Amesema, cheti ambacho mchangiaji huwa anapatiwa kinakuwa kimesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema, cheti hicho mtu aliyechangia anaweza kukitumia ndani ya miaka mitatu kuomba msamaha wa kodi TRA.

“Ndani ya miaka mitatu cheti hicho kitakuwa kime-expire. Kinacho-expire ni ile nafuu ya kodi, lakini cheti chako hakitakufa, kitakuwa hai siku zote.”

Dkt.Kipesha amesema, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa.Amesema, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2013.

Pia, amesema, madhumuni ya Mfuko wa Elimu ni kuongeza nguvu za Serikali katika kugharimia miradi ya elimu ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa, katika ngazi zote za Elimu kwa Tanzania Bara na Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.
“Mamlaka inatoa wito kwa wadau wote wa sekta ya elimu kuendelea kuunga mkono jitihada za sekta ya elimu kwa kuchangia Mfuko wa Elimu wa Taifa.

“Tunapokea fedha kupitia mifumo ya Serikali ya malipo, mifumo ya kibenki, na pia tunapokea vifaa vya aina mbalimbali,”amesema Dkt.Kipesha.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, kuanzia mwezi Oktoba 2017, mamlaka pia ilipewa jukumu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia la kusimamia na kuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund-SDF).

“Mfuko huu ni sehemu ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta tija katika ajira (Education and Skills for Productive Jobs (ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi (National Skills Development Strategy (NSDS),”amebainisha Mkurugenzi Mkuu huyo.

Amesema, Mfuko wa SDF ulikuwa unatoa ufadhili wa mafunzo ya kuendeleza ujuzi katika sekta sita za kipaumbele zinazoratibiwa na Programu ya ESPJ.

“Sekta hizo ni Kilimo na Kilimo Uchumi, Utalii na Huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Nishta,”amesema.

Amesema, ufadhili na utekelezaji wa miradi ya kuendeleza ujuzi awamu ya kwanza ya ESPJ ulikuwa wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2018/2019 ambao ulikamilika mwezi Juni 2023.

Akizungumzia kuhusu vyanzo vya mapato, Dkt.Kipesha amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya Mwaka 2001, Sura ya 412 pamoja na marekebisho yake ya Mwaka 2013, vyanzo vya mapato vya TEA ni pamoja na tengeo la kibajeti kwa ajili ya uendeshaji na miradi ya maendeleo.

Vingine ni tozo ya asilimia 2.5 ya ushuru wa forodha wa huduma za mawasiliano ya kielektroniki. Kiwango kisichopungua asilimia 2 ya Bajeti ya Serikali ukitoa deni la Taifa.
“Pia, kuna tengeo la kodi ya maendeleo ya ujuzi (SDL) kwa mujibu wa sheria inayoanzisha Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi.

“Na vyanzo vingine ikiwemo, michango ya hiari kutoka kwa wadau mbalimbali, wafadhili wa miradi wa ndani na nje ya nchi, uwekezaji na mikopo yenye riba nafuu kwa taasisi za elimu,“amefafanua Dkt.Kipashe.

TR

Akizungumzia kuhusiana na vikao kazi hivyo, Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema, vikao hivyo vimelenga kuongeza uelewa wa kutosha kuhusu taasisi na mashirika hayo ya umma.

“Kama tunatoa huduma kwa umma basi umma ufahamu taasisi hii ipo na inatoa huduma fulani, ndiyo maana Msajili wa Hazina akasema basi taasisi hizi zitoke na kueleza nini wanakifanya kupitia kundi la wahariri ambalo lina uwezo wa kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.
“Kufahamu hii taasisi ipo, lengo la kuanzishwa kwake, inafanya nini, ina malengo gani na mwelekeo wake katika kufikia malengo ya kuhudumia wananchi kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla,”amefafanua Kosuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news