Wanakijiji Magu waishukuru Wizara ya Maji

MWANZA-Wananchi wa Kijiji cha Chabula, Kata ya Nyanguge wilayani Magu mkoani Mwanza wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwajengea mradi wa maji ambao umekuwa na msaada mkubwa katika maisha yao.

Wametoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,CPA Amos Makalla wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo.

"Tunamshukuru Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi; hatukuwahi kufikiria kwamba tutakuwa na maji ya bombani lakini kwa jitihada za Serikali anayoiongoza sasa hivi tunapata maji ya bomba na hii imetuondolea changamoto ya maradhi," amesema Valentina Julius Mkazi wa Kijiji cha Chabula.

Mhe. CPA. Makalla amesema Serikali inatekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kivitendo na amewasisitiza wananchi hao kuhakikisha wanalinda na kutunza mradi huo ili waendelee kunufaika sasa na hata baadaye.

Ameielekeza RUWASA kuhakikisha inasogeza huduma kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa ili kila mwananchi anayepaswa kunufaika na mradi ayashuhudie manufaa hayo kama ilivyo dhamira ya Serikali.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua mama ndoo ya maji kichwani na hapa sote kwa pamoja tunashuhudia dhamira hiyo imetimia," amesema Mhe. Makalla.

Naye Masatu Mgaya, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chabula amepongeza Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza kwa kutekeleza mradi huo kwa niaba ya Serikali ambao amesema umekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa kijiji hicho.

Mradi wa Maji Bugando-Chabula umetekelezwa na wataalam wa MWAUWASA kwa kushirikiana na RUWASA kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 ili kuhudumia vijiji vya Chabula, Bugando, Nyashigwe na Kongolo Wilayani Magu.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu, Mhandisi Daud Amlima, amesema mradi umehusisha ujenzi wa dakio la maji kutoka Ziwa Victoria, tenki la kuhufadhia maji la ujazo wa lita 250,000, vituo 31 vya kuchotea maji na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji.

Amesema kwa sasa mradi unaendeshwa na Jumuiya ya Watumi Maji (CBWSO) ya Nyamwaki na kwamba mradi unatarajiwa kufikishwa kwenye vitongoji vya Dihu, Bugilang'ombe, Nyashigwe, Zuli na Zahanati ya Kijiji cha Bugando.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news