Waziri Mhagama azindua One Pacific Hotel, ahimiza uwekezaji Sekta ya Utalii Mbinga

RUVUMA-Imeelezwa kwamba,uwekezaji wa hoteli kubwa na za kisasa unasaidia katika kuchochea shughuli za utalii na kuongeza thamani ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kwa sababu ya upekee wa vivutio vyake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) akizindua mradi wa Hoteli ya One Pacific katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Hoteli ya One Pacific yenye hadhi ya nyota tatu katika Wilaya ya Mbinga.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Aziza Mangosongo (aliyesimama) akimkaribisha ofisini kwake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Mbinga.

Waziri Mhagama amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kwa kuwa balozi kinara wa sekta ya utalii na uwekezaji kwa ujumla katika sekta ya utalii.

“Mkakati wa Taifa wa ROYAL TOUR na kuifungua nchi yetu Tanzania katika sekta ya utalii ni mkakati mkubwa sana, na uliotukuka na tunaungana na wawekezaji katika kutafsiri ROYAL TOUR ndani ya wilaya yetu ya Mbinga,”alifafanua.

Akieleza kuhusu vivutio vinavyopatikana, Waziri amesema, wilaya ya Mbinga inavivutio vya kutosha; kama safu za milima zilizojipanga kwa kuvutia, zenye maporomoko ya maji, uoto wa asili, unaopendezesha madhari ya milima hiyo.

"Aidha, hapa ndio mahali ambapo kuna mapango ya kale katika eneo la Litembo, na inaaminika wazee wetu wa zamani waliishi katika mapango hayo."{
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo mafupi kutoka kwa Mhandisi Selemani Kinyaka (kulia) kuhusu mradi wa Hoteli ya One Pacific.

“Hii historia kama itawekezwa vizuri, ni kivutio na utalii wa kutosha sana katika eneo letu,”alibainisha.

Kwa upande wake Dkt. Erasmo Nyika akizungumza kwa niaba ya bodi ya wawekezaji wa mradi wa hoteli hiyo amesema wamesukumwa kuja kuwekeza Mbinga kutokana na msukumo wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amejenga mazingira rafiki ya uwekezaji.

“Tumewekeza miradi miwili ndani ya Wilaya ya Mbinga yenye thamani ya zaidi ya shilingi Billioni 4, na tumeona fursa zipo na tunashukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga kwa kutushawishi kuwekeza Mbinga, mradi umelenga kuzalisha ajira nyingi kwa wazawa,"amesema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama akiwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo wakitembelea baadhi ya maeneo ya mradi wa Hotel One Pacific kabla ya uzinduzi rasmi kufanyika.

Awali, Mhandisi Selemani Kinyaka katika taarifa yake amesema Ujenzi wa Majengo ya mraadi wa One Pacific Hotel; unavyumba vya kawaida 14, vyumba vya daraja la juu 23 vyumba vya hadhi ya kiutawala 3, Ukumbi mdogo wa mikutano, Migahawa 2, sehemu ya mazoezi, eneo la kuogelea na eneo la kufulia nguo.

Katika kipindi cha utekelezaji wa mradi wametoa ajira zaidi ya 250 ambapo 30 zilikuwa ajira za kudumu, na nyingine ni ajira zilizojitokeza kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news