Waziri Mkuu ahimiza vyanzo vipya vya mapato

*Wananchi wa Iboya kulipwa fidia ya sh. bilioni 4.8

SONGWE-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi na wananchi wa Vwawa wilayani Mbozi, mkoani Songwe wabuni vyanzo vipya vya mapato na wachangamkie fursa za uwekezaji.
Ametoa wito huo jana jioni, Novemba 24, 2023 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo waliojitokeza kwenye viwanja vya Malori kumsikiliza akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani humo kukagua shughuli za maendeleo.

Aliwashauri wajenge kituo cha kulaza malori ili yanapopaki yaweze kulipa ushuru lakini pia madereva wa hayo malori wakihitaji kufanya service au matengenezo ya magari yao, watakaotoa hizo huduma watakuwa ni wana-Mbozi.

“Tengeni ekari 50 ziwe za maegesho ya magari, wekeni uzio na mle ndani kuwe na huduma za akinababa lishe na mamalishe. Hawa wenye magari watakula, watanunua vinywaji baridi lakini wakitaka huduma za magari yao kama grisi, oil, watapata huduma hizo humohumo,” alisema.

“Vilevile, jengeni nyumba za kulala wageni na mahoteli ya viwango tofauti tofauti. Madereva wakija kupaki malori yao, watataka kulala kwenye Guest Houses badala kulala kwenye magari. Hatua hiyo itasaidia kuchangia mapato ya Halmashauri lakini pia kipato cha mtu mmoja mmoja kitaongezeka,” alisisitiza.

Mapema, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasenkeya aliwaeleza wakazi hao kwamba Serikali italipa fidia ya sh. bilioni 4.8 kwa wakazi 494 wa kijiji cha Iboya, kata ya Ihanda waliofanyiwa tathmini kupisha ujenzi wa kituo cha kimataifa cha ukaguzi wa magari yanayofanya safari za nje ya nchi.

Alisema, Serikali ya awamu ya sita inataka kujenga kituo cha kimataifa cha mizani (one-stop inspection station) ambacho kitakuwa na ofisi mbalimbali na panafanyika ukaguzi wa magari yanayoenda Tunduma.

“kituo kitakuwa na barabara zenye urefu wa km. 2.5 kwa pande zote za barabara na itachukua mita 300 kila upande wa barabara. Kikikamilika, kitapunguza sana msongamano wa magari kwani wakishamaliza kukaguliwa na kupima, wanaenda moja kwa moja hadi upande wa pili wa mpaka,” alisema wakati akielezea sifa za mradi huo.

“Miaka ya nyuma tulifanya tathmini na kupata sh. bilioni 3.1 zinazotakiwa kulipa fidia kwa wakazi hao lakini tathmini ya hivi karibuni imefanyika na kubaini kuwa jumla ya fidia yote ni sh. bilioni 4.8. Na sasa hivi jedwali la malipo liko kwa Mlipaji Mkuu (HAZINA) ili kuthibitisha wanaostahili kulipwa,” alisema.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema kuwa wamekwishalipa sh. bilioni 23.54 kwa wananchi waliouza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

“Tulitenga sh. bilioni 23.9 na tumeshalipa sh. bilioni 23.54 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amenithibitishia kwamba kiasi kilichobakia cha sh. milioni 360, kitalipwa kabla ya Jumatano, na baada ya hapo, tutaanza tena kununua mazao ya wana-Mbozi,” alisema

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news