Waziri Mkuu atoa maagizo Wizara ya Fedha

ARUSHA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha iimarishe mifumo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha ili baadhi ya watoa huduma wasio waadilifu wasitumie changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha kwa baadhi ya wananchi na kuwadhulumu.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Wizara ya Fedha iendelee kushirikiana na na watoa huduma za fedha kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo muhimu yakiwemo ya usimamizi wa fedha binafsi, kuweka akiba, mikopo, uwekezaji kupitia hatifungani na hisa, bima, mpango wa kujiandaa na maisha ya uzeeni pamoja na kodi.

“Wizara ya Fedha iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha, pia elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika. “

Ametoa maagizo hayo leo Novemba 22, 2023 alipofungua Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, jijini Arusha, ambapo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watoa huduma za kifedha wapunguze gharama za upatikanaji wa huduma za fedha zikiwemo riba na ada ili wananchi wengi watumie huduma za fedha zilizo rasmi.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameisisitiza Wizara ya Fedha iendelee kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Fedha inatakiwa iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuratibu gharama za huduma za fedha. “Pia, elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika.“

Waziri Mkuu amesema watoa huduma za kifedha hawana budi kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi kabla ya kufunga nao mikataba, pamoja na kuwafafanulia taratibu na masharti yao kabla hawajatoa kwao huduma hizo za fedha. Pia amewataka watoa huduma hao waweke mkakati mahususi wa kuongeza matumizi huduma kwa njia ya kidijitali pamoja na kuzisogeza hadi maeneo ya pembezoni na vijijini ili wananchi walio wengi wanufaike.

“Watoa huduma za fedha ongezeni ubunifu katika utoaji wa huduma. Toeni huduma zinazoendana na wakati, mahitaji ya soko na kuzingatia uhitaji wa makundi mbalimbali katika jamii. Suala hili liende sambamba na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta ya fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao. “

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wasimamizi wa Sekta ya Fedha na wadau wengine wazingatien sheria na kanuni za kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha ikiwemo kutatua malalamiko na migogoro na kulipa fidia na mafao kwa wakati.

Amesema lengo la maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa na Maonesho ya Huduma za Fedha yamejikita katika kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa, kusimamia vizuri rasilimali fedha ikiwa ni pamoja na kuimarisha utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa kutoka vyanzo salama na njia sahihi za kulipa madeni ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini.

Naye, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kukuza uelewa kwa Watanzania kuhusu masuala ya kifedha huku akitoa wito kwa Watanzania kuweka utaratibu wa kusoma vigezo na masharti ya huduma za kifedha wanazopata kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadae.

"Ni vyema tukaweka utaratibu wa kusoma na kuelewa vigezo na masharti tunapokuwa tunapatiwa huduma za kifedha hasa mikopo ili tujiepushe kuingia kwenye mikopo yenye masharti magumu ambayo wakati mwingine tunaweza kushindwa kuyatekeleza."

Kwa Upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bi. Natu El-maamry amesema maadhimisho hayo ya tatu ni muendelezo wa jitihada za Serikali katika kuongeza uelewa wa masuala fedha kwa Watanzania ili waweze kuwa na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za kifedha.

Amesema taasisi mbalimbali za kifedha na wadau wa kisekta wanatumia kipindi hiki kutoa elimu na huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news