Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi TRA Songwe

*Ahimiza matumizi ya risiti, kulipa kodi

*Akagua miundombinu shule ya msingi ya Dkt. Samia

SONGWE-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mkoa wa Songwe katika eneo la Nselewa Mlowo, wilayani Mbozi.
 
Ujenzi wa ofisi hiyo ambao ulianza Februari 16, 2023 unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 8.98 na utakamilika Juni 17, 2024.

Akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliohudhuria, jana Ijumaa, Novemba 24, 2023, Waziri Mkuu alisema mkoa huo ni mkoa tegemeo kwenye makusanyo kwani siku za karibuni Serikali inatarajia kujenga kituo cha forodha katika eneo la Isongole, wilayani Ileje, jirani na mpaka wa Malawi.

“Haya ni maandalizi ya miundombinu ya kuwasaidia wao wapate huduma bora zaidi. Niwasihi Watanzania msisahau kulipa kodi. Mkakati wa Serikali ni kuongeza mapato ya bajeti hadi asilimia 95 na kama mtu atataka kutuung amkono iwe ni nyongeza tu,” alisema.

Akizungumza na mafundi wanaofanya kazi hiyo, Waziri Mkuu alisema mkakati wa Taifa ambao Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameusisitiza ni kuhakikisha mafunzo ya ujuzi yanafikishwa hadi kwenye ngazi za chini na ndiyo maana kila wilaya inapelekewa VETA. “Naamini mkimaliza ujenzi huu, lazima mtakuwa na ujuzi na ufundi ambao mtaweza kutumia katika siku zijazo,” alisema.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa miundombinu kwenye shule mpya ya msingi ya Dkt. Samia iliyoko kata ya Mlowo, wilayani Mbozi, mkoani Songwe.

Akizungumza na walimu, baadhi ya wazazi na wanafunzi waliokuwepo, Waziri Mkuu alisema shule hiyo ni ya viwango vya hali ya juu na akawapongeza kwa kutumia vizuri za mradi huo.

“Ni shule ya pekee, nimevutiwa na ofisi ya mwalimu mkuu, nimekagua madarasa ni mazuri, nimetembelea madarasa ya awali na kukuta kuna michezo na zana za kufundishia. Nampongeza Mwalimu Mkuu kwani amesimamia vizuri sana mradi huu.”

Akisoma taarifa ya ujenzi wa miundombinu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Bw. Abdallah Nandonde alisema uamuzi wa Serikali ya awamu ya sita kuanzisha mpango wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, ulisababisha kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika shule mama ya msingi ya Lutumbi kutoka wanafunzi 1,650 mwaka 2015 na kufikisha wanafunzi 2,259 mwaka 2023.

“Ongezeko hilo la uandikishaji lilileta changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa 28. Kupitia Mradi wa Kuboresha Sekta ya Elimu (BOOST), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ilipokea shilingi milioni 538.5 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kujifunzia,” alisema.

Alisema ujenzi wa mradi huo ambao umetekelezwa kwa njia ya "Force Account" ulianza Mei 3, 2023 na kukamilika Julai 20, 2023. “Mradi umekamilika kwa asilimia 100 na ulihusisha ujenzi wa madarasa 14 ya wanafunzi wa shule ya msingi, madarasa mawili ya awali, matundu sita ya vyoo vya wanafunzi wa awali, matundu 18 ya vyoo vya wanafunzi wa msingi, matundu mawili ya vyoo vya walimu, jengo la utawala na kichomea taka.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news