Afisa wa Serikali athibitisha zoezi la kufyeka mahindi Manispaa ya Mpanda ni endelevu

MPANDA-Kaimu Afisa Mazingira wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Geofrey Mbunda amesema kuwa,zoezi la kufyeka mazao yote marefu mjini litakuwa ni endelevu.
Mbunda amesema,wale wote ambao wana mazao kwenye maeneo ambayo yalikatazwa yatafyekwa kwa mujibu wa taarifa ya katazo iliyotolewa.

“Zoezi litakuwa endelevu, litakuwa endelevu na matangazo yalishatolewa zamani sana kabla hata msimu wa kilimo kuanza, kwamba maeneo yote ya mjini watu wasilime mazao marefu.

“Na tukawa tumewaelekeza kwamba sehemu za kuanzia kata, hata katika kata tulielekeza kwamba hawaruhusiwi kulima mazao marefu, kila maeneo tuliweka hivyo.

“Maeneo yote ambayo yana mazao marefu hayatakiwi, na watu waliolima wajiandae tu kufyekewa kama walivyofekewa wengine,”amefafanua Mbunda kupitia mahojiano na Mpanda Fm.

Afisa huyo ameyabainisha hayo baada ya Desemba 13, mwaka huu Jeshi la Akiba lilipita maeneo ya Msasani na Mpanda Hotel ndani ya Manispaa ya Mpanda na kufyeka mazao yote marefu. Katika zoezi hilo zinakadiriwa zaidi ya hekari sita za mahindi ambayo yalikuwa yamestawi vilivyo yalifyekewa chini.

Ni mazao ambayo yapo karibu na makazi ya watu kufuatia agizo linalokataza kulima mazao hayo ambayo yanadhaniwa kuwa sehemu ya kuficha wezi au vitu vilivyoibiwa ndani na nje ya mji.

Wakizungumza na Mpanda Radio Fm baadhi ya wananchi wamesema kuwa, maamuzi ya kufyeka mazao hayo yamesaidia kuweka mazingira salama.

Sambamba na kuweka usawa kwa wale ambao hawajalima huku kwa upande mwingine wakishauri kutoza faini kwa waliofanya hivyo na si kukata mazao tu.

“Ukirudi nyuma ni sahihi, kwa sababu gani, eneo hili lote halina mhindi, mtoto atapita hapa atakwanyua tu mhindi, watakukamatia mtoto, atakwanyua tu kwa sababu si mvumilivu, ataniletea tu polisi atanipeleka messi, siwezi kutoka kirahisi.

“Kwa nini yeye alime sisi tusilime,hivi elfu 50 unanunua debe ngapi za mahindi sasa hivi, kwa nini yeye aendelee kulima tu,sisi tunamshangaa tu.

“Halafu…tunamjua anakulaga rushwa huyu.Kilichofuata mwaka jana alilima maharage vizuri bila shida. Sasa akaambiwa ni marufuku, akapanda tena,”wamekaririwa baadhi ya wananchi hao kupitia mahojiano na Mpanda Fm.

Wakulima

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima waliokatiwa mazao wamedai uhalali wa maeneo hayo kwa kuomba vibali katika serikali za mitaa.

Vile vile wanadai kuwa,wamekuwa wakilima maeneo hayo kwa muda mrefu huku wakiyawekea ulinzi dhidi ya uhalifu.
“Mimi nilikuwa ninategemea kwamba, mimi nimekosa kulima mahindi ndani ya Manispaa ningekamatwa siyo kufyeka mazao, ndiyo ningekamatwa niwekwe ndani na nikaishtakiwa kwa mujibu wa sheria hivi nilivyo.

“Lakini,badala ya kunikamata mimi yanafyekwa mazao…mimi sijapata taarifa ya aina yoyote na sijawa mwendawazimu wa kukaa juu ya sheria, lazima niwe chini ya sheria.

“Ningepewa miezi mitatu na nikishatoa tu iwe mara yangu ya mwisho,…jana nikiwa hapa nikapigiwa simu kwamba kuna watu kwenye shamba lako wanafyeka, basi mimi nikawa sina jinsi, nikafika nikakuta wanafyeka likawa ni kundi kubwa, kiukweli nilisikitika sana,”wamekaririwa wakulima waliofyekewa mazao yao kupitia mahojiano na Mpanda fm.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news