Baada ya Amaan Stadium, Rais Dkt.Mwinyi asema kabla ya AFCON 2027,Serikali itakuwa imejenga uwanja mwingine wa kisasa

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kujenga uwanja mpya mwingine wa kisasa ambao utatumika katika mashindano ya AFCON mwaka 2027.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo wakati akizindua rasmi Uwanja mpya wa Amaan Stadium leo Desemba 2023, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali imelenga kujenga miundombinu ya michezo kila wilaya kwa viwanja vipya vya kisasa.
Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika la maendeleo GIZ imefunga mkataba wa makubaliano kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vitano vya michezo midogomidogo ikiwemo mpira wa kikapu, mpira wa wavu , mpira wa mikono na mpira wa pete.
Viwanja hivyo vinatarajiwa kujengwa Kangani Wilaya ya Mkoani, Mchangamdogo Wilaya ya Wete, Tumbatu na Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini A na Haile Selasie Wilaya ya Mjini pamoja na viwanja vitatu vya Tennis Chakechake, Chuo kikuu cha SUZA Kampasi ya Nkurumah na Skuli ya Regeza Mwendo katika Wilaya ya Magharibi B.

Halikadhalika Serikali imefanikiwa kuwapeleka vijana katika nchi mbalimbali ikiwemo Uturuki na Afrika Kusini kwa lengo la kuendelezwa na baadae kucheza soka la kulipwa.
Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza wananchi kushiriki Tamasha la kila mwaka la mazoezi linalofanyika tarehe Mosi ya mwaka mpya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news