Katibu Mkuu Abeida awauma sikio wazazi, walezi wanawake Zanzibar

ZANZIBAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah amewataka wazazi na walezi wanawake kuwachunguza watoto wao sehemu za siri katika miili yao ili kuhakikisha kwamba watoto hao wako salama na hawajafanyiwa vitendo vya udhalilishaji vya aina ya ngono.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Abeida Rashid Abdallah (kati) akiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi cha Banaty baada ya kuwakabidhi cheti cha shukrani katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika Michenzani Mall Unguja.

Kauli hiyo ameitoa katika mafunzo ya kuwajengea uweza kikundi cha Banaty yaliyofanyika Michenzani Mall Unguja mara baada ya mtaalam wa afya, Dkt. Ummulkulthum Omar kuwasilisha mada ya afya ya mfumo wa uzazi pamoja na kueleza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake anakutana na kesi za watoto wachanga wa miezi minane wameingiliwa kinyume na maumbile na kuharibiwa.

Bi.Abeida amesema,kwa vile wazazi na walezi wanawake hawana vibakio ni vyema kuwa karibu na watoto hasa watoto wa kiume waliyofikia umri wa balehe kwa kuwauliza maswali bila kuona haya pamoja na kuwaangalia sehemu zao za siri kama ziko salama na hazijafanyiwa udhalilishaji wa aina ya ngono.
“Tuwe karibu nao hasa watoto wa kiume, sisi wanawake hatuna vibakio kwa hiyo lazima tuwe karibu na watoto wetu tuwahoji, Je? Hakuna mtu aliyeguza sehemu za siri? Na tusiishie kuwauliza tu.

"Pia kuwaangalia hasa huko sehemu ya siri tujue kama kuko salama, tusisubirie azoeshwe mchezo mchafu,"alisema Abeida.

Alieleza kwamba ripoti ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeonesha matukio ya udhalilishaji 199 yameripotiwa kwa mwezi wa Oktoba, 2023.
Kati ya idadi hiyo asilimia 78.9 ni watoto na wanawake ni asilimia 16.2 hivyo ni vyema wazazi na walezi wanawake kila mara wawe karibu na watoto wao.

Aidha,Katibu Mkuu huyo alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo na wanawake wote waliyopata mafunzo ya ujasiriamali kutumia ipasavyo elimu hiyo, kwani Serikali ya Mapinduzi inatoa fursa ya mikopo kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua na umasikini.

Alisema,umasikini pia unachangia matendo ya udhalilishaji kutokea kwa watoto.
Naye Mtaalum wa Afya, Dkt Ummulkulthum Omar kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja Zanzibar katika mada ya mfumo wa uzazi aliyowasilisha alieleza matatizo mbalimbali yanayowatokea wanawake katika mfumo wa uzazi ikiwemo kutoshika mimba, kutokwa na uchafu usiokuwa wa kawaida katika sehemu za siri.

Hivyo,amewataka wanawake kukimbilia hospitali endapo wataona dalili yeyote ambayo sio ya kawaida kutokana na elimu aliyofundisha ili kuwahi kutimbiwa.

Aidha,katika uwasilishaji wa mada hiyo aliezea kwamba anakutana na kesi ya watoto wa umri tofauti ambao wameingiliwa kinyume na maumbile ikiwemo watoto wa miezi minane, hali ambayo inasikitisha hasa ukiangalia matendo hayo yanafanywa na mtu wa karibu.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Abeida Rashid Abdallah (kushoto) akimkabidhi cheti cha shukrani mratibu wa mafunzo ya kuwajengea uwezo kikundi cha Banaty,Raya Hamad Mchele, mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Michenzani Mall Unguja.

Mapema Mratibu wa mafunzo hayo ambaye ni Mkurugeni wa Raha Online TV, Raya Hamadi Mchele amesema,lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kuwapa elimu kundi la Banaty ikiwemo elimu ya afya, kujitambua na elimu ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kimaisha.

Kikundi cha Banaty kimeanzishwa kwa lengo la kusaidiana katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo harusi na msiba.

Hivyo,kikundi hicho kina muda wa miaka minane na mfuko wao wa fedha una pesa zaidi ya shilingi za Tanzania milioni ishirini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news