Benki Kuu yawapa elimu watumishi wa Mungu namna ya kutambua, kupokea na kutunza fedha

NA GODFREY NNKO

VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kutambua kuwa, wana mchango mkubwa wa kuhakikisha fedha ya Tanzania inakuwa na uhai muda wote kwa ajili ya matumizi sahihi ya shughuli za kila siku za kiuchumi nchini.

Kutokana na hilo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza kuwahamasisha waumini wao kuacha kukunja pesa hususani wanapokwenda kutoa sadaka badala yake watumie bahasha huku nao wakihakikisha sehemu ya kutolea sadaka hiyo haiwi kikwazo.

Wito huo umetolewa Desemba 11,2023 katika makao makuu dogo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam ambapo Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu imetoa elimu ya utambuzi wa alama za usalama zilizopo katika noti zao kwa viongozi wa dini kupitia Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo inajumuisha viongozi wote wa dini wenye nia ya kudumisha amani.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Usimamiaji wa Sarafu, Dkt. Nguling’wa Balele, amesema BoT inawajibu wa kuelimisha umma kuhusu alama za usalama zilizopo katika noti zao pamoja na namna nzuri ya kuzitunza fedha hizo.

Dkt. Balele ameiambia kamati hiyo kuwa, utunzaji mbovu wa fedha hupelekea uharibifu na uchakavu wa sarafu kabla ya muda wake na hivyo kulazimisha uchapishwaji na utengenezwaji wa fedha zingine kwa ajili ya kurudishwa kwenye mzunguko.

Vile vile, Mkurugenzi huyo ameomba ushirikiano kati ya BoT na viongozi wa dini uendelezwe ili kusaidia kupunguza uharibifu wa fedha zetu na kulazimika kutumia fedha za kigeni kugharamia uchapishaji wa fedha nyingine badala ya fedha hizo adimu kutumika katika shughuli nyingine za maendeleo.

Naye Meneja Msaidizi Mipango na Uchambuzi wa Shughuli za Uendeshaji wa Sarafu, Bw. Salala Nchunga amesema, lengo la kutoa elimu hiyo kwa viongozi wa dini ni kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa kutunza fedha.
Bw. Nchunga amesisitiza kuwa, fedha zinapita katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo nyumba za ibada na hivyo kuwaomba viongozi wa dini wasaidie kufikisha elimu hii kwa waumini wao.

“Nia na madhumuni ya semina hii ilikuwa ni kuzungumza na viongozi maaskofu, mashehe, wachungaji pamoja na mapadri ikiwa na maana tunataka tufikishe elimu ya utunzaji bora wa pesa ya Tanzania ikiwemo noti na sarafu.

“Na wao tumewaita ikiwa na maana wana waumini ambao wapo chini yao, pesa nyingi zinapita kwenye mikono mingi, kwa hiyo ile mikono inaishia kanisani, inaishia misikitini katika kutoa sadaka.

“Kwa hiyo tunatambua wao wakitambua alama za fedha halali ya Kitanzania watafikisha elimu, lakini pia utunzaji wa zile pesa, matumizi sahihi, lakini pia mwisho wa siku ile pesa ikikaa kwa muda mrefu inaisaidia nchi kuokoa fedha ambazo zinakwenda kurudishia pesa inayoharibika.

“Kwa hilo ndiyo dhumuni kuu na limefikiwa kwa kiwango kikubwa, tumepata Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo imekuwa na sisi katika siku ya leo kuhakikisha hilo lengo linatimia.

“Pesa ikitunzwa vizuri, ikatumika vizuri haitaondoka kwenye mzunguko kwa urahisi, itakaa muda mrefu wa maisha yake na mwisho wa siku tukija kuirudishia itakuwa katika uhalali, uhalisia na imeshatekeleza majukumu yake ya uchumi.
Katika semina hiyo, Benki Kuu imewaeleza watumishi hao wa Mungu kuhusu matumizi sahihi ya pesa.

“Sadaka mara nyingi ukienda sehemu ya kutolea utakuta katundu kadogo, ambako watu wengi wanaiminya ile hela, wanaikunjakunja mara nyingi ili iweze kupita kwenye kile kitundu, kwa hiyo njia sahihi ni kuiweka ile sadaka kwenye bahasha, mwisho wa siku ukiitoa inakuwa imenyooka, hiyo pesa itakaa kwa muda mrefu.

“Lakini kingine inawezekana kabisa kuna pesa ambazo tunasema ni bandia, ziko kwenye mzunguko, sasa zile zinaweza zikajitokeza kule wakazipokea katika maeneo ya ibada, kwa hiyo tumewafundisha baadhi ya alama jinsi ya kuzitambua mwisho wa siku pesa bandia inatupelekea kumtafuta anayezalisha ili ule mtandao tuweze kuuondoa kabisa.

“Sasa,hawa viongozi ni wa muhimu kama wataiona pesa ya namna hiyo ina maana wanaweza wasimpate muumini,lakini zoezi likiendelea mara kwa mara unaweza ukajikuta unamfahamu aliyeitoa na mwisho wa siku sisi tukaweza kuuondoa huo mtandao, kwa sababu zile pesa bandia zinavyoongezeka kwenye mzunguko zinaipelekea nchi kuanza kufikiria namna ya kutengeneza pesa yenye malighafi ya aina nyingine katika mzunguko.”

Shehe

Kwa upande wake, Shehe Abdalah Idd ambaye ni Shehe wa Wilaya ya Kigamboni na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam amesema, elimu hiyo ya pesa kutoka Benki Kuu itasaidia kwa kiwango kikubwa kuhusu utunzaji, uhifadhi na kuzitambua fedha bandia katika nyumba za ibada.
“Elimu hii itasaidia, kwa sababu sisi viongozi wa dini tumekuwa tukisaidia Serikali na nchi yetu kwenye mambo mengi, yakiwepo Corona, yakiwepo mambo ya amani. Lakini, sasa tunaingia kwenye mambo ya fedha.

“Lazima tuwaambie watu watunze fedha, na kama unataka kumtunza mtu fedha si lazima utengeneze shada umwage nyingi, unaweza kuandika hata cheki na sasa hivi unaweza kutumia miamala hata ya kielektroniki ya simu za mkononi, na lengo ni kwamba umpe mtu fedha umsaidie siyo fahari ya ujinga ambayo itaathiri nchi.

“Kwa hiyo elimu hii tutawafikishia wao na lazima tuwaambie viongozi, watu wetu walio kwenye makanisa, misikiti na waliotuzunguka wajue kwamba wanawajibika kuilinda, kuipenda na kuitunza sarafu ya nchi.

“Lakini,tumepata faida nyingine kama viongozi wa dini, sisi ndiyo tunapokea fedha katika makapu na katika maboksi ya sadaka,na kupitia haya mazingira ya fedha za kapu wakati mwingine zinakuja pesa mbaya, watu mtaani hawajui.

“Kwa hiyo kupitia alama lazima zile kamati zinazosimamia fedha za michango ziangalie ili isipatikane athari sasa tukajikuta kiongozi wa dini amekutwa na fedha feki wakati anaenda kutumia kumbe ilikuwa kwenye sadaka.

“Kwa hiyo elimu inaweza ikaleta mabadiliko makubwa na tunaishukuru BoT na tunaiomba ipanue uelewa huu kwa kutoa elimu zaidi na zaidi,”amesema Shehe Idd.

Padri

Naye Padri Dominick Singano wa Kanisa la Angilkana jijini Dar es Salaam amesema, elimu hiyo imewasaidia katika kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya usalama na matumizi ya fedha halali za Tanzania.

“Kwanza imetujengea uelewa kama viongozi wa dini katika matumizi sahihi ya sarafu ya Tanzania katika kuitumia, lakini kubwa zaidi katika kuitunza ili iendelee kuwa na thamani katika matumizi ya nchi.
“Moja wapo ni suala zima la utunzaji wa fedha, namna ambavyo tunazitunza majumbani au tunapozitunza kwenye mifuko yetu,lakini pia katika shughuli zetu mbalimbali ambazo huwa tunazifanya ambazo zinaweza zikapelekea fedha isitunzike vizuri.

“Kwa mfano kundi la wajasiriamali hususani wauza mkaa, namna ambavyo wanavyozitunza fedha ili iweze kuwa na thamani ni jambo la msingi sana, lakini pia kwenye nyumba zetu za ibada wakati wa kutoa sadaka tumepata elimu nzuri kwamba tusizifiny’ange fedha, ni vizuri ukatoa fedha ikiwa imenyooka vizuri au kutumia bahasha, fedha ikae kwenye bahasha vizuri na kuweza kuiweka kwenye chombo cha sadaka.

“Lakini, pia kuna baadhi ya wananchi au watu mbalimbali ambao huwa wanapenda kuziandika fedha kwa kutia aidha saini zao ama kwa kuandika majina ya kwao ama kitu chochote ambacho wangependa kuandika.

“Ile kwa mafunzo ambayo pia tumeyapata leo ni uharibifu wa fedha ya Tanzania, kwa hiyo tumepata kitu cha msingi sana,”amesema Padri Singano.

Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 inatoa mamlaka kwa Benki Kuu pekee kutengeneza na kutoa fedha (noti na sarafu) kwa matumizi nchini Tanzania.

Hiyo ndiyo fedha halali kwa ajili ya malipo nchini Tanzania. Hivyo, Benki Kuu ina wajibu wa kubuni na kuagiza noti na sarafu ili kukidhi mahitaji ya fedha nchini.
Fedha ya Tanzania ni Shilingi ambayo imegawanywa kwenye senti 100. Benki Kuu imekuwa ikihakikisha kwamba sarafu yake ina ubora unaokubalika kwa sarafu nzuri ambao ni kukubalika na umma kama fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya bidhaa na huduma.

Pia, kuhakikisha kuna alama za usalama ambazo zinafanya iwe vigumu kutengeneza noti na sarafu zisizo halali na uwezo wa sarafu kudumu kwa muda mrefu.

Ili kutekeleza na kuhakikisha kwamba hali inakuwa hivyo, Benki inatekeleza Sera ya Fedha Safi ambayo inatoa elimu katika makundi mbalimbali kupitia njia tofautitofauti.

Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na maonesho yanayofanyika nchini, vipindi vya televisheni na kupitia kampeni za elimu kwa umma kwenye mikoa mbalimbali nchini na kama ilivyofanya kwa watumishi wa Mungu ambao nyuma yao kuna kundi kubwa la watu wanaowaongoza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news