Jinsia na usawa ni vipengele muhimu vya kufanikisha maendeleo endelevu Tanzania-Waziri Pembe

ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amesema,Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa jinsia na usawa ni vipengele muhimu vya kufanikisha maendeleo endelevu nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar,Mheshimiwa Riziki Pembe Juma akishereheka na vijana mtandao wa wanawake barani Afrika, baada ya kupokea cheti ikiwa ni tuzo ya mafanikio ya maisha kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa vijana hao, katika kongamano liliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoa wa Pwani.

Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati akifunga kongamano la vijana wanawake viongozi kutoka nchi 16 barani Afrika, lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha,Mkoa wa Pwani.

Alisema,masuala ya jinsia na usawa yameainishwa katika Katiba zote mbili, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1984.

Alieleza kwamba, lengo la kuainishwa humo ni katika kusimamia haki na usawa na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi.

Pia alisema katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 imeainsha umuhimu wa Jinsia na Usawa.
Alisema, katika kufanisha maendeleo hayo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum (SMT) na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (SMZ) zimeanzishwa kisheria kwa lengo la kuratibu na kusimamia masuala ya Jinsia nchini.

Aidha, alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa elimu ni moja ya silaha muhimu hasa kwa wanawake ikiwa watakua na nia ya kufikia maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Alieleza kwamba, Serikali imeweka makusudi hatua za kukuza elimu ya wasichana na kuwahimiza waendele kusoma ili wapate elimu ambapo Jamii kwa ujumla inawasaidia wasichana kuendelea na masomo badala ya kuwalazimisha kuingia kwenye ndoa za mapema.
Mheshimiwa Riziki alitoa wito kwa washiriki wa kongamano hilo kutumia jukwaa hilo kama fursa ya kujifunza mbinu bora zaidi ambazo zitafanya kuongeza uwezo wao na ujuzi.

Alifahamisha kwamba, hatua hiyo itasaidia katika bara la Afrika kuhimiza vijana wa kike kuthamini elimu itakayowasaidia kupata mapato yao na kupata nafasi katika vyombo vya maamuzi.

Kongamano hilo la siku tatu limehudhuriwa na watu 100 wanawake vijana ambao ni wanachama wa harakati pamoja na Maafisa wa zamani na wanaharakati wanaoendesha mashirika ya wanawake yenye mafanikio kutoka nchi mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news