Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu:Rais Dkt.Mwinyi asema Serikali zote mbili zinaendela kuweka mazingira mazuri kwa vijana

ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema,Serikali zote mbili zinaendela kuweka mazingira mazuri kwa vijana ikiwemo kuwapatia elimu, mikopo na fursa mbalimbali ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika uzinduzi wa Matembezi ya Umoja wa Vijana yenye Mnasaba na Sherehe za kutimia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Makombeni Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema,matembezi haya yanaendana na fikra na falsafa za waasisi wa Mapinduzi, hivyo ni lazima vijana kuyatumia matembezi hayo kwa kuyatangaza mambo mazuri yanayofanywa na viongozi wakuu wa nchi.

Aidha,amesema ni lazima vijana kushirikiana na Viongozi wa Serikali zote mbili kuyaenzi kwa vitendo ili viongozi waweze kuwaletea maendeleo wananchi na kuwaondolea changamoto zinazowakabili.

Vilevile, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi,Mhe. Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha vijana wajibu wa kusaidia kulinda Taifa lao sambamba na kupiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, udhalilishaji na dawa z kulevya kwa kutoa elimu kwa vijana wenzao ili kuweza kudumisha amani na utulivu nchini.

Sambamba na hayo amewataka viongozi walioandaa matembezi hayo na bijana kwa ujumla kusimamia nidhamu ili kuweza kufikia lengo la kuwepo kwa jumuiya hiyo ambayo ni tegemeo la chama na Taifa kwa ujumla katika kuandaa viongozi wazalendo wa sasa na wajao.

Hata hivyo,Dkt. Mwinyi amewataka vijana wenye sifa kushiriki kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura linaloendelea, ili wapate nafasi ya kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa (CCM) Taifa, Mohamed Ali Mohamed (Kawaida) amesema,katika kipindi cha Miaka 60 ya Mapinduzi, Zanzibar imepiga hatua kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo, itakayoweza kuondosha changamoto za wananchi.

Mbali na hayo amesema, dhamira ya Mapinduzi ni kuwaletea wananchi wa Mjini na Vijijini maendeleo na kuwapa nafasi vijana katika kujitawala wenyewe hivyo Jumuia ya Umoja wa Vijana itaendelea kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa kuwalinda viongozi wakuu wa nchi kwa kuhakikisha wanawaweka tena madarakani ifikapo mwaka 2025.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Matar Zahor Massoud amesema kuwa, kupitia mapinduzi matukufu ya Mwaka 1964 Zanzibar imepata maendeleo makubwa ambayo yanaletwa na viongozi wakuu waliopo madarakani na waliopita,hivyo ni vyema kila mmoja kuyaenzi maendeleo hayo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news