Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu:Serikali yazindua Kituo cha Wajasiriamali Hanyegwa Mchana

ZANZIBAR-Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Suleiman Masoud Makame amewataka wajasiriamali wa Wilaya ya Kati na maeneo jirani kulitumia vyema eneo la karakana ili kuendelea kuwaunganisha pamoja.

Hayo ameyasema huko Hanyegwa Mchana Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa uzinduzi wa karakana hiyo kuelekea kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema, jengo hilo limejengwa kwa fedha za Mfuko wa Ahueni ya Uviko-19 na liko tayari kutumiwa na wajasiriamali katika kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo na vitongoji vyake.

Waziri huyo amewataka wananchi hao kuunga mkono juhudi zinazochukiliwa na viongozi wao na kuzichangamkia fursa zitakazowaondolea changamoto za maisha.

Pia, aliwataka wananchi hao kulipia tozo zitakazowekwa kwani fedha hizo ndio zinazoenda kutumika kwa mahitaji mbalimbali ya jengo hilo ikiwemo malipo ya maji, gharama za umeme ulinzi na gharama nyengine mara baada ya kumalizika kwa muda waliopewa kufanya kazi zao katika eneo hilo bila malipo.

Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikala za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Issa Mahfudhi Haji alisema karakana hiyo imejengwa na Kikosi cha Zimamoto ambapo ujenzi huo ni wenye viwango na kukidhi mahitaji yaliyotakiwa.

Katibu Mkuu huyo alisema, jumla ya wajasiriamali 300 wataweza kufanya kazi mbalimbali katika karakana hiyo ikiwemo utengenezaji wa vyombo vya moto, wafanya biashara za mbao, ufundi seremala na wauzaji wa bidhaa nyingine kwa wakati mmoja.

Akitoa salamu za Mkoa Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Ayuob Mohammed Mahmoud amesema kuwa, lengo kuu la mradi huo ni kuzalisha ajira kwa vijana na kuwataka vijana kujitokeza kuikimbilia fursa hiyo.

Hata hivyo aliishauri Mkurgenzi wa Manispaa ya Wilaya ya Kati kuweka kipaombele kwa maombi ya wazawa na wakaazi wa wilaya hiyo kuweza kupata nafasi katika jengo hilo.

Mradi huo umekamilika ukiwa na bloki tisa za maeneo ya kufanyia kazi na biashara na umegharimu jumla ya shillingi bilioni 1.9 za kitanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news