NHIF:Serikali imefanya mageuzi makubwa Sekta ya Afya, nasi tumefanya maboresho

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Bernard Konga amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya nchini.
“Kama nchi tumepiga hatua kubwa sana katika eneo la afya, mambo ambayo yanaendelea kwenye sekta ya afya ni makubwa mno.

“Kwa hiyo lazima tutambue mchango wa mambo hayo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ili nasi kama taasisi za umma tuweze kufanya maboresho ambayo yatawezesha wananchi kupata huduma bora na kwa haraka;

Konga ameyasema hayo leo Desemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi baina ya mfuko huo na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Lengo la kikao hicho ni kupeana mrejesho wa maboresho ya huduma zake kwa wanachama na wadau wake nchini.

Akiwasilisha mada kuhusu kitita cha mafao yaliyoboreshwa kwa mwaka 2023, Bw.Konga amesema, "Lengo la kwanza ni kuboresha upatikanaji wa huduma bora na za uhakika kwa wanachama.

“Pili kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia ya tiba na hali hali ya bei katika soko.”

Aidha, amefafanua kuwa, lengo lingine ni kuwianisha kitita cha mafao na orodha ya dawa muhimu (NEMLIT) pamoja na Mwongozo wa Tiba wa Taifa (STG).

“Nne, ni kujumuisha maoni na mapendekezo mbalimbai ya wadau,” amesema Konga huku akifafanua kuwa, walipita kwa wadau mbalimbali ili kupata maoni kuhusu maboresho ya kitita.

Lengo lingine amefafanua ni kutekeleza ushauri wa taarifa ya mapendekezo ya tathimni ya uhai na uendelevu kwa kipindi kilichoishia Juni 31, 2021.

“Pia, kuwezesha kundi kubwa la wananchi kumudu gharama za matibabu kwa kuzingatia hali zao za kiuchumi.”

Lengo lingine amesema, ni kujenga uwezo wa vituo vya afya ngazi zote kuanzia afya ya msingi, kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha udhibiti ili kuzuia mianya ya udanganyifu.

Vile vile amefafanua kuwa, mfuko huo katika kufanya maboresho hayo uliwashirikisha wadau mbalimbali.

Miongoni mwa wadau walioshirikishwa ni Umoja wa Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Huduma za Afya (APHFTA), Tume ya Huduma za Kijamii za Kikristo (CSSC) na BAKWATA.

Wengine ni vyama mbalimbali vya kitaaluma, Chama cha Madaktari Tanganyika (MAT), vituo vya huduma vinavyomilikiwa na Serikali ikijumuisha Hoispitali za Rufaa, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa na waganga wafawidhi wa hospitali za halmashauri.

Bw.Konga amefafanua kuwa, mambo muhimu yaliyozingatiwa wakati wa maboresho ya kitita hicho ni kufanya tafiti ya gharama halisi za matibabu katika soko husika.

Pia, kushirikisha taasisi chini ya Wizara ya Afya ikiwemo Bohari ya Dawa nchini (MSD) na TMDA, lengo likiwa ni kuwianisha kitita cha mafao na orodha ya dawa zilizosajiliwa.

“Na tulishirikisha wadau wa sekta binafsi kwa lengo la kupata maoni, ushauri na mapendekezo kuhusu kitita.”

Katika hatua nyingine, Bw.Konga amebainisha kuwa, walijumuisha maelekezo ya Serikali kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Sambamba na kutekeleza mapendekezo ya taarifa ya tathimini ya uhai na uendelevu wa mfuko pamoja na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Bw.Konga ameongeza kuwa, kupitia maboresho yaliyofanyika kuna ongezeko la jumla ya dawa 124 katika kitita cha mafao cha mfuko kutoka Orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT) na kuweka mbadala wa dawa 309 katika kitita cha mafao ili kuwianisha na NEMLIT.

Habari-Maelezo

Akitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, mwakilishi Lilian Lundo amesema kuwa, utaratibu wa NHIF kuvishirikisha vyombo vya habari katika masuala mbalimbali unatoa nafasi umma kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu huduma za bima.
“Hongereni sana kwa utaratibu huu wa kuvikuitanisha vyombo vya habari kwa ajili ya kupata uelewa kabla ya kwenda kutoa elimu na kuhabarisha umma.”

TEF

Akitoa salamu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Mjumbe wa Kamati Tendaji ya jukwaa hilo, Jane Mihanji ameushukuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuendelea kuonesha ushirikiano na vyombo vya habari nchini.
“Niwashukuru kwa niaba ya TEF kwa kuona umuhimu wa sisi kuwa hapa,wakati wowote mkiwa na jambo msisite kuwasiliana na sisi vivyo hivyo nasi linapotokea jambo, msisite kupokea simu zetu ili kuweza kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yatakayowezesha umma kupata taarifa sahihi.

“Ni kuhusu umuhimu wa bima ya afya,umuhimu wa kujiunga na bima ya afya na umuhimu wa Serikali kuboresha sekta ya afya kwa ustawi bora wa jamii.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news