Rhobi Samwelly awaunganisha wanawake Rorya na fursa za kiuchumi

NA FRESHA KINASA

KATIKA kuhakikisha wanawake wanainuka kiuchumi na kuwa na kipato thabiti,Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly amewaunganisha wanawake wajasiriamali zaidi ya 2,500 wanaoishi wilayani Rorya na Benki ya CRDB ambapo wamepewa mafunzo ya ujasiriamali.

Pia,wanatarajia kunufaika na fursa ya mikopo bila riba ambayo watapewa na benki hiyo kupitia vikundi walivyounda chini ya usimamizi wake.

Akizungumza na wajasiriamali hao wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nyanduga wilayani humo,Rhobi amesema kuwa, iwapo wanawake wakiinuka kiuchumi hata vitendo vya ukatili wa kijinsia vitapungua katika familia zao na jamii kwa ujumla.
"Kina mama uchumi ukiwa mzuri hata vitendo vya ukatili wa kijinsia vitapungua katika familia, Niwashukuru viongozi wa UWT Wilaya ya Rorya wamekuwa mstari wa mbele kutafuta fursa za kiuchumi.

"Hii pia ni dhamira ya Serikali yetu chini ya Dkt.Samia Hassan amekuwa na shauku kubwa kuona Mwanamke anasimama kiuchumi.
"Kupitia programu yetu ya 'Erasto Widows Empowerment Programme chini ya Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania tumeamua kushirikiana na CRDB kuwainua wanawake, tunaamini tukiwasaidia kina mama kiuchumi watasomesha watoto wao, kuwahudumia vyema na kwa hakika ndoto zao zitatimia ndio maana tumewaunganisha kina mama 30 kwenye kila kikundi zaidi ya wanawake 2,500 wa Rorya,"amesema Rhobi Samwelly.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Rorya, Loth Olemeirut amepongeza juhudi za Rhobi Samwelly ambazo ameendelea kuzionesha katika kuhakikisha anachangia maendeleo ya wanawake mkoani Mara ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na fursa ambazo zinafaida katika kuwaletea maendeleo na kutetea haki zao.

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Serengeti, Everlyn Munyeri amesema kuwa, benki hiyo imeanzisha taasisi nyingine ndani yake ya kuwasaidia wanawake ambayo iko nje na mfumo wa kibenki ijulikanayo kwa jina la IMBEJU inayolenga kuhakikisha inawainua wanawake kiuchumi kupitia vikundi vyao kuanzia watu 10 na kuendelea.
Amesema, mkopo unaotolewa kupitia programu hiyo ya vikundi utakuwa hauna riba ila una ada ya asilimia saba kulingana na mkopo ambao utachukuliwa na marejesho ya mkopo huo ni kuanzia miezi mitatu hadi miezi 12.

Amesema kuwa ,ada ya uanachama itakuwa asilimia saba, ambapo asilimia sita ni ada ya uanachama, na asilimia moja itakuwa malipo ya bima ya mkopaji na mdhamini atakuwa ni kikundi ambacho Mjasiriamali huyo atakuwa amejiunga. Na mkopo utarudishwa kwa kila wiki na kila mwezi kutegemeana na uendeshaji wa biashara na aina ya biashara.
Aidha, amewataka wanawake kusimama kwa ujasiri kutumia vyema fursa za mikopo kusudi waweze kuendeleza biashara zao. Huku akiwaomba kutambua kuwa mchango wao katika maendeleo ni mkubwa kutokana na kujishughulisha kufanya shughuli mbalimbali za kuwaingizia vipato.

Jesca Ayubu mjasiriamali na Mkazi wa Kata ya Kirogo wilayani humo amesema kuwa, fursa hiyo ya mikopo itamsaidia kupanua biashara yake ya matunda na kwamba mikopo ya benki inamanufaa kwani haina riba kama ambavyo wamekuwa wakipata kutoka kwa taasisi za fedha za watu binafsi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news