Serikali kufanya marekebisho ya kodi kila baada ya miaka mitatu

NA PETER HAULE
WF

SERIKALI imeeleza kuwa, itakuwa inafanya marekebisho ya kodi kila baada ya miaka mitatu ili kuwa na Sera ya Kodi inayotabirika na kuwafanya wawekezaji kuweka mipango yenye ufanisi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akieleza kuwa Serikali imeweka Sera ya Kodi inayotabirika ili Wawekezaji waweze kuweka mipango yao vizuri, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika Jijini Mbeya, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa kodi.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati wa Kongamano la ukusanyaji maoni ya Kodi Kikanda Jijini Mbeya, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano kama hayo yanayofanyika Kanda mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha Sera ya Kodi kwa mwaka 2024/25.

Alisema kuwa Utaratibu wa sasa ni kufanya marekebisho ya kodi kila baada ya miaka mitatu, hivyo marekebisho yaliyofanywa mwaka huu hayafanyiki tena hadi miaka mitatu ili kuwa na Sera za Kodi inayotabirika.

“Awali kulikuwa na utratibu ulioasababisha wananchi kusema bajeti ni ya pombe, Sigara na Soda, maana ya kauli hizo ni kuwa kila mwaka Serikali ilikuwa inabadilisha viwango vya kodi vilivyokuwa vinatozwa kwenye bidhaa hizo jambo ambalo kwa sasa halitakuwa linafanyika kila mwaka,”alieleza Bw. Mwandumbya.
Mkurugenzi wa Livy Afrika, Bw. Chris Mwasambili, akitoa maoni yake ya kuhusu uboreshaji wa Sera ya utozaji Kodi kwa mwaka 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda, lililofanyika jijini Mbeya.

Akizungumzia maboresho ya Kodi yaliyofanyika, Bw. Mwandumbya alisema kuwa Serikali imeongeza bidhaa za mtaji (Capital goods) zinazozalishwa nchini katika wigo wa ahirisho la kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuanzia tarehe Mosi Julai, 2023 na kuondoa katika wigo huo bidhaa za mtaji zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kuanzia tarehe Mosi Julai, 2026.

Alieleza kuwa,nchi imebarikiwa kuwa na watu wengi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, bidhaa zinazozalishwa katika sekta hizo zinapaswa ziongezwe thamani ili kuwezesha wananchi kupata bei ambazo zitawanufaisha, ili kufanikisha hilo zinahitajika mashine, viwanda vidogo vidogo na vikubwa vitakavyosaidia kuchakata bidhaa hizo kwa maana ya capital goods.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mbeya Bw. Joseph Mwakisu, akieleza kuhusu maboresho ya kodi kwa wafanyabiashara kwa mwaka wa fedha 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mbeya.

Alifafanua kuwa,Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa utaratibu maalumu kwenye Mashine zinazokwenda kuongeza thamani ya bidhaa ili kuwaongezea wananchi kipato na pia kukuza uchumi wa Taifa.

Bw. Mwandumbya alisema kuwa, ikiwa bidhaa ya mtaji imeingizwa kutoka nje ya nchi ushuru wake umesamehewa, lengo likiwa kuwapeleka wananchi waende kwenye uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa ili kuongeza thamani ya bidhaa na hatimaye kupata mapato mengi zaidi.

Pia alisema kuwa, Serikali imeweka utaratibu rahisi wa utozaji kodi ya mapato yatokanayo na biashara ya usafirishaji wa abiria, mizigo na utalii kutegemeana na uzito wa gari, idadi ya abiria wanaobebwa, chombo husika pamoja na biashara inayofanywa.
Mkulima wa mazao mchanganyiko mkoani Mbeya, Bw. Gidion Siame, akitoa maoni ya maboresho ya Kodi kwa mwaka 2024/25 kwenye sekta ya kilimo, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda, lililofanyika jijini Mbeya.

Alieleza kuwa,gari aina ya Toyota Hiace inayoweza kubeba abiria 18 kodi yake kwa mwaka ni shilingi 550,000 ambayo inalipwa kwa awamu kwa miezi mitatu na Gari aina ya Fuso ya Tani 10 kodi yake ni 750,000 kwa mwaka ambayo pia inalipwa kwa awamu nne.

Maboresho mengine yaliyofanywa ni kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa vifaa vinavyotumika kubadili mfumo wa magari kutoka matumizi ya mafuta kwenda matumizi ya gesi au umeme na kusamehe kodi hiyo kwenye magari yanayoingia nchini yanayotumia gesi au umeme kwa kuwa nchi inaenda kwenye matumizi ya gesi na umeme kutokana na changamoto kubwa ya mafuta.
Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, akieleza hatua ambazo mlipakodi anaweza kuzichukua iwapo hatakubaliana na maamuzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwemo kwenda kwenye Taasisi hiyo, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mbeya.

Kwa upande wake, Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, alisema kuwa nia ya Utawala bora kwenye mfumo wa kodi nikutaka mlipa kodi alipe kodi ya haki, asionewe lakini pia asiache kulipa kodi halali ya Serikali.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya akisalimiana na Mzee John Bakilile, mkazi wa Mbeya, baada ya kumalizika kwa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mbeya.

“Kama kuna mlipa kodi ana malalamiko anayo nafasi ya kwenda kwenye Mahakama ya Biashara ambako atakutana na wanasheria, pia anaweza kulalamika kupitia ofisi ya TOST, sisi tutamsikiliza na kuwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutatua tatizo ndani ya muda mfupi,”alieleza Bw. Barongo.

Alisema kuwa, taasisi hiyo haipo kwa ajili ya kuichonganisha Serikali na TRA bali ipo kwa kazi ya kuwasaidia walipa kodi na TRA ili kodi ya Serikali iweze kulipwa kwa uhalali.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mbeya, Bw. Erick Sichinga, akitoa maoni kuhusu uboreshaji wa Sera ya Kodi wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda, lililofanyika jijini Mbeya.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), mkoa wa Mbeya, Bw. Erick Sichinga, alisema kuwa ufafanuzi wa kisheria unaotolewa kupitia Kongamano la ukusanyaji wa Kodi utawasaidia wafanyabiashara kwa kuwa mara nyingi taratibu zinazotumiwa na wafanyabiashara kufikisha maoni Serikalini zilikuwa na mlolongo mrefu hivyo maoni yanafika ikiwa tayari Sheria zimetungwa.

Bw. Sichinga ameipongeza Wizara ya Fedha kwa uamuzi wa kuwafuata wafanyabiashara katika Kanda zao na kusikiliza maoni yao moja kwa moja na kutoa matumaini ya kufanyiwa kazi kwa kuwa wanauhakika maoni yao yamefika sehemu sahihi na kwa wakati.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (katikati) na wadau wa kodi Jijini Mbeya wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Ukusanyaji maoni ya Kodi kutoka Wizara ya Fedha na Sekta binafsi, baada ya Kongamano la ukusanyaji maoni ya utozaji kodi kwa mwaka 2024/2 jijini Mbeya.

Timu ya Wataalam wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha ianendelea na ukusanyaji wa maoni kwa wananchi Kikanda ambapo hadi sasa mkoa wa Arusha, Mwanza na Kigoma na Mbeya imefikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news