Wanawake wafanyabiashara watakiwa kushiriki Kongamano la Wanawake la AfCFTA 2023

DAR ES SALAAM-Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said ametoa wito kwa wanawake wote wanaojihusisha na biashara kushiriki Kongamano la Pili la Wanawake katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) linalotarajiwa kufanyika tarehe 6 hadi 8 Disemba, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi huyo amayasema hayo Novemba 30,2023 akiwa katika kikao cha maandalizi ya kongamano hilo ambalo Tanzania ni mwenyeji na linaandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Sekretarieti ya AfCFTA na linaongozwa na Kauli Mbiu isemayo "Kuimarisha Ushiriki wa Wanawake katika Biashara na Kuongeza Kasi ya Utekelezaji wa AfCFTA”.

Aidha, alisema kuwa kongamano hilo ni fursa muhimu kwa wanawake wafanyabiashara kutoka Tanzania na Afrika kupata maarifa, ujuzi na ushirikiano kutoka kwa wataalamu na wadau mbalimbali kutoka duniani kote.

Amesema,kongamano hilo pia litakuwa fursa muhimu kwa wanawake wafanyabiashara kubadilishana uzoefu na kushiriki mikakati ya kuimarisha ushiriki wao katika biashara ndani ya Afrika na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

"Kongamano hili linalenga kuwakutanisha pamoja wanawake katika biashara kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara. Hivyo, changamoto mbalimali ambazo wanawake wanakabiliana nazo zitajadiliwa pamoja na njia ya kuzitatua ili waweze kunufaika ipasavyo na fursa za biashara zinazotokana na Mkataba wa AfCFTA," alisema Mhandisi Zena.

Vilevile, Katibu Mkuu Kiongozi huyo alieleza kuwa wanawake ni kiini cha biashara na wamekuwa chachu muhimu katika maendeleo ya uchumi duniani, hivyo wanatakiwa kujumuishwa ili kuchangamkia fursa zinazotolewa chini ya Mkataba wa AfCFTA.

Aliwataka wanawake wafanyabiashara kujisajili kwa ajili ya kushiriki kongamano hilo kupitia anuani ya tovuti https://au-afcfta.org/wit/. Link hii pia inapatikana kupitia tovuti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ni www.viwanda.go.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news