Wapinga pendekezo la kuwashusha vyeo walimu Musoma

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara Dkt. Halfan Haule, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini Denis Ekwabi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa pamoja wamepinga pendekezo la kuwashusha vyeo baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi wilayani humo ambao shule wanazozisimamia hazikufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2023.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeshika nafasi ya sita Kati ya Halmashauri tisa za Mkoa wa Mara kwa kupata wastani wa asilimia 75. Ukiwa umepanda kwa asilimia 8 ukilinganishwa na matokeo ya mwaka jana ambapo ufaulu ulikuwa ni asilimia 67.9 kwa shule 118 za Msingi za Wilaya ya Musoma, shule za Serikali zikiwa ni 114, na shule za binafsi ni shule nne.

Hatua hiyo, inatokana na pendekezo lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Mheshimiwa Nyeoja Wanjara Novemba 30, 2023 katika kikao cha baraza la madiwani wakati akiwasilisha mapendekezo ya kuboresha ufaulu katika Halmashauri hiyo likiwemo suala la kuwashusha vyeo Walimu wakuu ambao shule zao hazikufanya vizuri.

Diiwani wa Kata ya Musanja, Ernest Mwira amesama kuwa, matokeo mazuri yanachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo miundombinu bora na ushiriki wa Jamii katika kuinua ufaulu hivyo kigezo cha Walimu wakuu kuwashusha hakiwezi kuwa suluhisho.

Naye Diwani wa Kata ya Tegeruka, Modekai Mashauri amesema kuwa, miongoni mwa mambo yanayochangia ufaulu mzuri ni pamoja na wazazi na walezi kuwajibika, wadau kushiriki kutatua changamoto za elimu na kuboresha mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Halfan Haule akizungumzia Jambo hilo, ameunga mkono hatua ya madiwani hao kupinga pendekezo hilo kwa kusema kuwa,

"Njia ambayo tunaitumia moja ni kufanya tathmini kuanzia ngazi ya shule pale kuna kamati ya shule wanakaa na kujadili kuona ufaulu ukoje, Ukiwauliza Walimu wanakwambia zipo sababu za Jamii, shule zenyewe, mfano Watoto wanasoma kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa 10:00 jioni hawajapata chakula hii ni sababu pia unakuta hawasomi kwa ufanisi.

"Tuna mambo ya kurekebisha katika sekta ya elimu kuanzia Kijiji, kwenye kata, tukitoka kata tunakuja kwenye Wilaya watasema. Yako mambo yanamhusu Mkurugenzi madai yawezekana Walimu Wana madai yao hayajatekelezeka morali ya kazi iko chini.

"Ukimvua madaraka Mwalimu Mkuu huwezi kusaidia hata kidogo, kuna Mwalimu Pale Makojo alipigwa mapanga hili pia ni tatizo kwa jamii yetu lazima tukae pamoja tuwe na mikakati baina ya Wananchi, wadau na Serikali badala ya kumtoa Mwalimu kwenye madaraka.

"Lazima tubebe mawazo kutoka kwenye Jamii Wananchi wanasemaje na ushiriki wao, yako mambo mengi Kuna shule ukienda unakuta Kuna Walimu wanne au watano shule zimechoka Sana hayo yate yanachangia kwenye ufaulu.

"Utakuta shule ina wanafunzi 800 walimu ni wanne au watano kumbe tunapaswa pia kiwatia moyo Walimu wetu wanaofanya vizuri na kutafuta walau utaratibu wa adhabu kama vinyago kwa shule ambazo hazifanyi vizuri, tofauti na kuwashusha vyeo wakuu wa shule ambazo hazikufanya vizuri wakati mwingine hawana makosa, kumbe yapo kwa jamii," amesema Dkt. Haule.

Aidha,Dkt. Haule amepongeza ufaulu wa Halmashauri hiyo kupanda kwa mwaka huu na ameomba ushirikiano uwepo kuhakikisha elimu inazidi kupanda.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Charles Magoma amewataka madiwani kuwapenda na kuwathamini watumishi wa umma walioko katika maeneo yao kwani mchango wao ni mkubwa katika kuwahudumia Wananchi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini Denis Ekwabi amesema kuwa, "maagizo ya chama ni kwamba Walimu wakuu ambao shule zao hazina matokeo mazuri wasishushwe, waachwe kwani suala la ufaulu linahusisha mambo mengi kwa hiyo Chama kinatoa maelekezo wabakie katika nafasi zao wakati mikakati mingine ya kuboresha elimu na ufauli ikiendelea kufanywa,"amesema Denis Ekwabi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news