Zanzibar yaandaa mikakati kuwezesha wajane

ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar,Mhe. Riziki Pembe Juma amesema, Serikali kupitia wizara hiyo imeandaa mikakati maalumu ya kuwawezesha wanawake wajane waliotelekezwa na watoto.
Akizungumza na Rais wa Umoja Wajane wa Afrika na Ujumbe wake huko ofisini kwake, Mhe. Riziki amesema, hatua hiyo inasaidia kuwaandaa kisaikolojia na kuweza kukabiliana na maisha baada ya tukio hilo.

Aidha, alifahamisha kuwa wizara yake imekuwa ikitoa ujuzi wa ujasiriamali pamoja na kutoa mikopo midogomidogo kwa akina mama hao ili kuanzisha biashara itakayosaidia kumudu gharama za maisha ya mama na mtoto.

Naye Rais wa Wajane wa Afrika, Hope Nwakwesi alisema ipo haja ya jamii kupatiwa elimu juu ya madhara yatokanayo na talaka kwani hali hiyo imekua ikipelekea kwa kiasi kikubwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa, kukosa jamii yenye upendo na kuwa na Watoto wasio na muelekeo mzuri wa misingi ya maisha kwa kukosa malezi ya baba na mama.

Daktari wa Magonjwa ya Afya Aya Akili Zanzibar, Dkt. Khadija Abdulrahman Omar alisema, wajane wengi hufikiria juu ya namna gani wataweza kumudu gharama hizo binafsi na kwa watoto wao jambo linalopelekea kuathirika kisaikolojia na kupelekea kuugua ugonjwa wa afya ya akili.

"Takwimu zinaonesha nusu ya wagonjwa Wanawake wanaolazwa kwa ugonjwa waafya ya akili inasababishwa na ujane iwe wa kuachwa au kuondokewa na mwenza,"alisema Dkt.Khadija.

Hata hivyo alisema Serikali inaendelea na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili na kuiomba Ofisi ya Mufti kuyafanya mafunzo ya kuwajengea uelewa kabla ya ndoa kuwa ni ya lazima wakihusisha wataalamu wa afya yaakili katika mafunzo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwat amesema,wajane wamekuwa wakipunguza nguvu kazi na upendo kwa familia kadiri wanavyoendelea kukaa hospitalini wakiugua ugonjwa wa afya ya akili.

Alifahamisha kuwa, maamuzi ya talaka hayamuathiri mjane peke yake bali huathiri hata watoto na kuwataka wanandoa na wenza kufikiria muelekeo wa watoto kabla ya kutengana au kupeana talaka kwani nao ni miongoni mwa waathirika wakubwa baada ya tukio hilo.

"Tunapofikia hatua ya Kua tumechokana tuangalie na watoto tuangalie nguvu kazi inayopotea kwa kuugua muda mrefu wewe upo hospitali watoto wapo sehemu Fulani wanadhalilika na kuteseka, mwisho nao wataugua magonjwa ya akili,"alisisitiza Rose.

Alifahamisha kuwa migogoro kati ya wawili hao sambamba na kufariki kwa Baba huchangia kumpa mtoto msongo wa mawazo na hatimaye kuugua afya ya akili.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajane Zanzibar,Tabia Makeme amesema, ipo haja ya kushirikiana kwa pamoja kati ya taasisi zinashughulikia masuala hayo,Kituo cha Afya ya Akili na Ofisi ya Mufti ili kupunguza ongezeko la wajane linalopelekea wimbi la wagonjwa wanawake wanaogua afya ya akili.

Amesema, hali ya magonjwa ya akili kwa wajane sio nzuri na jumuiya hizo haziridhishwi na hali hiyo hivyo aliishauri jamii kutokuingia katika ndoa bila kuwa na elimu nzuri itakayowawezesha wawili hao kuweza kuvumiliana na kupelekea kupeana talaka.

Katika ziara hiyo ya siku moja, Umoja wa Wajane Afrika ulipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Magonjwa ya Akili Kidongo Chekundu, Tume ya Ukimwi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuelekea Mkutano Mkuu wa siku ya Wajane Duniani unaotarajiwa Kufanyika mwakani jijini Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news