BoT kuwachukulia hatua kali wanaokopesha mikopo mbalimbali bila leseni nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, wanaokopesha mikopo mbalimbali nchini bila kuwa na leseni watachukuliwa hatua.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Januari 3,2023 na Gavana wa BoT,Emmanuel Tutuba.

"Benki Kuu ya Tanzania inapenda kukumbusha umma kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, ni kosa kwa taasisi,kampuni au mtu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni.

"Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania haitasita kuwachukulia hatua za kisheria, taasisi, kampuni au watu binafsi wanao fanya biashara ya kukopesha bila ya kuwa na leseni.

"Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 16(2)(a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa Sheria ni pamoja na faini isiyopungua Shilingi Milioni 20 au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili au vyote viwili kwa pamoja.

"Benki Kuu inawakumbusha wakopaji wote kuhakikisha wanasoma mikataba ya mikopo inayotolewa na wakopeshaji, kuelewa na kukubaliana na vigezo na masharti ikiwa ni pamoja na riba na gharama nyingine za mikopo hiyo.

"Tunasisitiza kuwa mkopeshaji anatakiwa kutoa nakala ya mkataba wa mkopo kwa mkopaji, kadhalika mkopaji ana haki ya kudai na kupewa mkataba wa mkopo kila anapochukua mkopo.

"Tunapenda kuusisitizia umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi,kampuni au mtu binafsi ambae hana leseni kutoka Benki Kuu.

"Aidha, orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zinatolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwenye tovuti yetu ambayo ni www.bot.go.tz,"amefafanua Gavana Tutuba.

Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na: Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha Idara ya Usimamizi wa Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha Benki Kuu ya Tanzania, 2 Mtaa wa Mirambo, S.L.P 2939 Dar es Salaam au Simu Na. +255-22-223-5585; Barua Pepe: info@bot.go.tz or botcommunications@bot.go.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news