Muhimbili:Atolewa mawe 62 kwenye mfuko wa nyongo

DAR ES SALAAM-Madaktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Chakula Ini na Kongosho wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamemfanyia upasuaji mgonjwa mwenye umri wa miaka 48 na kutoa mawe 62 yaliyokuwa kwenye mfuko wa nyongo ikiwa ni mara ya kwanza kutoa kiasi hicho cha mawe kwa mgonjwa hospitalini hapa.
Akizungumza kwa niaba ya Jopo lililoshiriki kufanya upasuaji huo, Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na Kongosho, Dkt. John Bosco Ngendahayo amesema mgonjwa huyo alikuja hospitalini hapo akiwa na maumivu makali na mwili uliodhoofika baada ya kupewa Rufaa kutoka Mbeya akiwa na dalili mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa manjano, kuwashwa mwili mzima ambao ulimfanya ajikune mwili kiasi cha kumsababishia vidonda.

“Mgonjwa alikuwa hajui kuwa ana mawe kwenye mfuko wa nyongo kwakuwa alikuwa na dalili mbalimbali ila baada ya kumfanyia kipimo cha CT-Scan kilionyesha kuwa mfuko wa nyongo ulikuwa umeathirika kwa sababu mawe yalikuwa mengi na nyama za tumbo kushikana hivyo tulishauriana na wataalamu kumfanyia upasuaji ili kutoa mawe uliochukua saa nne,” ameeleza Dkt. Ngendahayo.

Ameeleza sababu zinazosababisha mtu kupata mawe kwenye mfuko wa nyongo kuwa ni nyongo kupata mgandamizo ndani ya mfuko wa nyongo na kujiongeza uzito kutokana na madini ya chumvi au mafuta mwilini (rehemu) ambayo hutengeneza ujiuji na baadaye kuganda na kutengeneza mawe na mawe hayo baadaye huyeyuka ila kuna mengine ambayo huwa hayayeyuki.

Pia ameongeza kuwa mtu anaweza kuishi na mawe hayo bila kujua ila baadaye yanaweza kumsababishia kupata maumivu makali tumboni hasa upande wa kulia chini ya mbavu, kupata manjano, mwili kuwasha kiasi cha kukosa usingizi, kupata kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na dalili nyingine kama hizo.

Dkt. Ngendahayo ametoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kwenda hospitali kufanya uchunguzi wa afya hasa pale wanapohisi kuwa na maumivu kwenye tumbo au wanapopata manjano.Mgonjwa anaendelea vizuri .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news