Rais Dkt.Mwinyi awapongeza wakulima wa karafuu nchini

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewapongeza wakulima wa karafuu nchini kwa bidii ambazo wanaonesha kuhakikisha zao hilo la kimkakati linaendelea kuwa na manufaa kwao na Taifa.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa pongezi hizo Januari 4, 2023 baada ya kutembelea Bandari ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ziara ya kushtukiza na kushuhudia karafuu za magendo tani 9.5.

Karafu hizo zenye thamani ya shilingi milioni 140 zilitaka kusafirishwa kwa magendo na kukamatwa kwa ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Vikosi hivyo vinajumuisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) na Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati wakulima wa karafuu,nataka mtambue kwamba zao la karafuu kwetu sisi Serikali ya Zanzibar ni zao la kimkakati.

“Ni zao ambalo linatuokoa sana na hapa ninataka niseme hivi,mwaka huu kutokana na uhaba wa dola kama isingekuwa karafuu hizi kuziuza kupata dola, basi hata chakula nchini hapa kingekuwa matatizo makubwa.

“Kwa hiyo, ninawashukuruni sana,kwa kuendeleza zao hili na Serikali inatambua mchango wenu mkubwa na tutafanya kila jitihada kuondoa changamoto ambazo zinawakabili katika zao hili, kwa sababu tunalitegemea kama nchi zao hili.

“Kuhusu vituo hivi vya kukusanyia karafuu viboreshwe viwe bora zaidi, na viweze kutoa huduma nzuri zaidi hilo ninawaagiza ZSTC, mimi pia ninataka nikubaliane na mzungumzaji kwamba sasa wakati umefika hivi vituo tangu vimejengwa vipo hivyo hivyo, wakati umefika sasa wa kufanya mabadiliko.

“Tufanye mabadiliko hili tuendane na wakati uliopo, watu waondoke katika ile hali ya kusubiri kwa muda mrefu na huko nyuma kulikuwa kuna matatizo mengi ya watu kuuza bila kusafisha,kulikuwa kuna matatizo ya mizani.

“Hayo mambo yote,yanatakiwa yafanyiwe utaratibu wa kugeuzwa twende na mageuzi ili tuweze kuwapa wakulima bei nzuri, lakini huduma bora,”amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameleeza kuwa, Serikali imeamua asilimia 80 ya mauzo ya karafuu katika soko la Dunia kumpatia mkulima wa karafuu na 20 kwa Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC) kutumika katika uendeshaji.

Vile vile Rais Dkt.Mwinyi amesema, karafuu bora inatoka Zanzibar, hivyo kwa kuitunza vizuri na kuisafisha bei yake itaendelea kuimarika duniani.

Rais Dkt.Mwinyi aliwasihi wananchi wasifanye magendo kwa maana watapata hasara kulingana na sheria za nchi, pia amesema Serikali itaendelea kuongeza bei ya karafuu.

Awali, mkulima wa zao la karafuu mkaazi wa Wete,Khatib Khamis Khatib akizungumza mbele ya Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane kwa kuendelea kuimarisha bei ya karafuu nchini.

“Ninashukuru sana kutokana na bei ya sasa ni nzuri sana na vile vile,tunakushukuru (Mheshimiwa Rais) kwa kututembelea katika kituo hiki, na vile vile kutukagua, tunashukuru sana.

“Vile vile, kila penye uzuri, pia hapakosi kasoro hiyo ni tabia ya kibinadamu kidogo, mimi ninalosemea hasa ni kutokana na kituo chetu hiki cha ununuzi wa karafuu, pengine kama kuna uwezekano hiki kituo ni kidogo sana, kusema kweli hakitukidhi kutokana na mahitaji yetu ya sasa.

“Kwa, hiyo mimi ninaomba aidha tuwekewe sehemu nyingine au kiboreshwe zaidi ili tupate nafasi zaidi ya kuuza zao hili la karafu,”amesema Khatib mbele ya Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news