Rhobi Samwelly awapa neno wanawake mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

WANAWAKE mkoani Mara wameombwa kuendelea kusimamia malezi na maadili mema kwa watoto katika familia zao ikiwemo kuhakikisha watoto wa kike wanawasimamia vyema wapate fursa ya elimu kwani mchango wao ni mhimu katika kuleta mabadiliko chanya na maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa Januari 17, 2024 na Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani Mara wakati akitoa semina ya mafunzo ya biashara kwa wanawake wajasiriamali wa Manispaa ya Musoma.

Rhobi amesema, nafasi ya wanawake ni kubwa katika kuwafanya watoto wawe na maadili mema pamoja na kufikia ndoto zao na kwamba wakisimama kidete familia na jamii itapiga hatua katika nyanja ya maendeleo.
"Tuzungumze na watoto wetu baada ya kazi zetu tuwajenge, vijana pia wasipolelewa katika maadili mema ndio tunasikia wengine wanakuwa mashoga.

"Tuisaidie Serikali yetu kuwaandaa watoto katika makuzi bora, lakini pia tuwafundishe misingi ya imani ya Mwenyezi Mungu huku tukifanya kazi kwa bidii na kuwaombea," amesema Rhobi.

Aidha,Rhobi amewataka wanawake kujenga tabia ya kupendana, kusaidiana, kuthaminiana na kushirikishana katika fursa mbalimbali za kibiashara kwani kufanya hivyo watapanuka na kuwa na mtandao madhubuti utakaowaunganisha pamoja na hivyo kufanikisha malengo yao.
"Kupitia Erasto Widows Empowerment Programme ambayo iko chini ya Shirika la Hope, shauku yangu ni kuona wanawake wa Mkoa wa Mara tunapiga hatua na fursa ambazo ninazipata niwaunganishe nazo zitunufaishe kwa pamoja,"amesema Rhobi na kuongeza kuwa.

"Ninachowaomba, tupendane na kujaliana kama ambavyo Mheshimiwa Rais Wetu Dkt. Samia amekuwa akisisitiza ili tuwe wazalishaji na mchango wetu katika familia tukisaidiana na waume zetu uonekane, kusimamia malezi kwa watoto na kufanya shughuli za maendeleo kama ni biashara zifanyike kwa ubunifu na kwa umahiri,"amesema Rhobi.
Anastazia Jerome ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Kata ya Kitaji Manispaa ya Musoma amesema,wanawake mbali na kufanya shughuli za ujasiriamali, lakini wanalo jukumu la kusimamia malezi kwa watoto wao pamoja na kuwalinda dhidi ya vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news