Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii-Rais Dkt.Samia

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema,Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha huduma hizo zinapatikana.
Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kumpa mkono wa pongezi Mkuu wa Kanisa la KKKT Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wakati wa Ibada ya kuingizwa kazini kwa Mkuu huyo wa Kanisa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2024.

Rais Samia amesema hayo leo wakati wa hafla ya kuingizwa kazini kwa Askofu Dkt.Alex Gehaz Malasusa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) iliyofanyika Kanisa Kuu la Azania Front.

Aidha, Rais Samia amesema taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kuwajenga waumini kiimani na kujenga taifa lenye watu wema, wanaowajibika katika jamii na kuwa wastahmilivu zinapotokea changamoto.

Vile vile, Rais Samia amesema ni muhimu kuimarisha taasisi ya familia kwani ikiwa imara na yenye masikilizano, itatoa malezi mema kwa mtoto na itaandaa muumini, mwanajamii na raia mwema.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhama na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya

Hewa nchini ili kuepuka athari zinazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Rais Samia pia ameitaka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufuatilia kwa karibu changamoto zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yameathiriwa na mvua hizo.

Hali kadhalika, Rais Samia ameziagiza pia Wizara za kisekta zikiwemo Wizara ya Maji, Nishati, na Ujenzi kuwa kwenye hali ya tahadhari na kujipanga kutoa msaada kwa haraka katika maeneo yanayokumbwa na athari za mvua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news