Serikali yawalipa Wazabuni shilingi trilioni 2.1

NA KHADIJA IBRAHIM
WF

WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameliambia Bunge, Mjini Dodoma kuwa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi Desemba 2023, imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani zaidi ya shilingi trilioni 2.1 kati ya madai ya zaidi ya shilingi trilioni 3.1 yaliyowasilishwa.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (kulia), bungeni Jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WF, Dodoma).

Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, aliyetaka kufahamu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa ama kukataa kuwalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki.

“Jumla ya madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyowasilishwa kwa uhakiki yalikuwa zaidi ya sh. bilioni 3,110.33, kati ya kiasi hicho madeni yaliyolipwa ni zaidi ya sh. bilioni 2,128.54 ambapo sh. bilioni 1,032.13 ni madeni ya wazabuni na sh. bilioni 1,096.41 ni madeni ya wakandarasi,” alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa madeni ya sh. bilioni 981.79 yalikataliwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa nyaraka, madeni kubainika kulipwa tayari, pamoja na makosa ya ukokotoaji.

Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo na uchumi wa Taifa, imeendelea kutenga na kulipa madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyohakikiwa na kukubaliwa.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, kuhusu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki, bungeni jijini Dodoma.

Alifafanua kuwa Serikali imeongeza bajeti ya kulipa madeni kutoka wastani wa shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 700 kwa mwaka na kuahidi kuwa madai ya wazabuni na wakandarasi yataendelea kulipwa kadri watakavyowasilisha hati zao za kukamilisha kazi (certificates).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news