Shanga yatolewa katika mapafu ya mtoto Muhimbili

DAR ES SALAAM-Wazazi wameaswa kufuatilia michezo ya watoto kwa karibu zaidi na kuwazuia kuweka vitu mdomoni, puani pamoja na maskioni ili kuwaepusha na madhara mbalimbali ikiwemo madhara ya kudumu na kifo.
Kauli hiyo imetolewa na Jopo la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Kifua na Moyo, Mapafu na Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao wameshiriki kuondoa shanga ya plastiki iliyokuwa imekwama katika pafu la kulia la mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Daktari Bingwa wa Mapafu na Mfumo wa Upumuaji, Dkt. Mwanaada Kilima amesema, shanga hiyo iliingia kwenye pafu baada ya kumpalia mtoto alipokuwa akiichezea mdomoni takribani mwezi mmoja uliopita.

Dkt. Kilima amesema mtoto huyo alitaabika tangu wakati huo kwa kikohozi na kupumua kwa shida huku njia mbalimbali zikitumika kujaribu kuitoa na kugonga mwamba, ndipo wataalamu wa mapafu walipofanikiwa kuitoa bila madhara yoyote.
“Tulitumia mpira laini wenye kamera ya video ya mapafu (Flexible bronchoscope) na kifaa cha kukamatia (foreign body basket) na kufanikiwa kuitoa hivyo kumwepusha na upasuaji mkubwa ambao ungesababisha ama kutoa pafu au sehemu ya pafu,” amesema Dkt. Kilima.
Dkt. Ramadhan Hamis, Bingwa wa Upasuaji wa Kifua na Moyo ndiye aliyeoongoza jopo hilo kwa kushirikiana na Dkt. Charles Komba Bingwa wa Upasuaji Kifua pamoja na Dkt. Mwanaada Kilima Bingwa wa Mapafu na Mfumo wa Upumuaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news