TIC yaja na kampeni kabambe ya kuhamasisha uwekezaji nchini

MWANZA-Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimezindua kampeni yake maalum ya kuhamasisha uwekezaji nchini.
Kampeni hiyo imezinduliwa leo katika Mkoa wa Mwanza na Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho, Bw. Gilead Teri na inalenga kufikia mikoa 15 nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha Clouds Tv, Bw. Teri ameeleza namna ambavyo kituo hicho kimejipanga kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa kurahisisha taratibu za usajili wa miradi, punguzo katika ushuru wa forodha sambamba na kuweka vivutio mbalimbali vya kiuwekezaji kama sehemu ya kampeni hii maalumu ya kuufanya mwaka 2024 kuwa mwaka wa uwekezaji.

Aidha, TIC imeeleza namna ambavyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ulioisha wa 2023 kimeweza kuvutia uwekezaji ambapo Bw. Teri ameeleza namna kituo hicho kilivyofanikiwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola Bilioni 5.6 sawa na zaidi ya trilioni 10 za kitanzania ambapo uwekezaji huo unatarajiwa kuzalisha kati ya ajira 50000-100000 kwa watanzania wazawa.

Ikumbukwe TIC kwa sasa inasimamia utekelezaji wa sheria mpya ya uwekezaji ya Mwaka 2022 ambayo pamoja na mambo mengine imeshusha kiwango cha mtaji kinachotakiwa kwa mwekezaji mzawa kusajili mradi wake kutoka Dola 100,000 hadi kiasi cha Dola 50,000 lengo likiwa kuvutia wawekezaji wa ndani kunufaika na fursa za kiuwekezaji zilizopo.

TIC kwa sasa ina ofisi katika kanda zote za nchi huku ikiwa na uwakilishi katika ofisi zote za wilaya na mikoa nchini ikiwa ni mkakati wa kukiweka kituo karibu kabisa na wawekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news