AfDB yaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kukuza uchumi

NA BENNY MWAIPAJA

WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki, ambapo ameishukuru Benki hiyo kwa kufadhili miradi 29 ya kitaifa na kikanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 3.84.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na AfDB, baada ya kumalizika mkutano kati yao uliojadili fursa mbalimbali za ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo katika miradi ya nishati, kilimo. Miundombinu ya barabara na maji, mkutano huo umefanyika jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha).

Dkt. Nchemba amesema jijini Dodoma kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ambapo kati ya miradi hiyo, miradi 26 ni ya kitaifa na 3 ni ya kikanda ambayo iko katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati, maji na kilimo.

Alisema kuwa zaidi ya asilimia 13.6 ya fedha hizo zimeelezwa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme kupitia miradi 5 ambapo mitatu kati ya hiyo ni ya Kitaifa na mingine miwili ni ya Kikanda inayolenga kuunganisha umeme katika nchi za Afrika Mashariki.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza kuhusu nishati safi wakati wa kikao na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki, uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Nchemba, aliitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Umeme wa Mto Malagarasi (49.5 MW), Kakono (87.8 MW), Gridi ya kaskazini Magharibi (400 KV), Maporomoko ya Maji Rusumo (80 MW) na utakaounganisha nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania pamoja na mradi wa umeme unaoziunganisha Kenya na Tanzania.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), akiwa katika mkutano na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki (kulia) uliojadili fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, Ujenzi wa Reli ya SGR ya Kikanda, mkutano uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Nchemba alibainisha kuwa Benki hiyo imekubali kushiriki katika Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) wa Kikanda wenye lengo la kuunganisha huduma za usafiri na usafirishaji abiria na mizigo kati ya Tanzania nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo mikataba ya mkopo huo nafuu itasainiwa hivi karibuni.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki baada ya mkutano kati yao uliojadili fursa za uwekezaji katika sekta ya Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR wa Kikanda, mkutano huo umefanyika jijini Dodoma.

Aliiomba Benki hiyo kusaidia utekelezaji wa mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Raverley, akizungumza jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki (kushoto), uliofanyika jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayesimamia masuala ya Nishati, Dkt. Kevin Kariuki, aliahidi kuwa Benki yake ipo tayari kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza katika Nishati safi ya kupikia, kuendelea kufadhili miradi ya ujenzi wa miudombinu ya usambazaji umeme, kilimo na maji.
Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki (kushoto), akieleza nia ya Benki yake kuendeleza kusadia maendeleo ya Tanzania na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, wakati wa mkutano jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Raverley.

Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano kwa kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuwa Benki yake itamuunga mkono ili kufanikisha mradi huo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) akipeana mkono na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Raverley, baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Waziri huyo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki (hayupo pichani), jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Kevin Kariuki, ambaye ni raia wa Kenya, aliambatana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Raverley.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news