Dkt.Mpango atoa wito magonjwa yasiyoambukiza

ZANZIBAR-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema jitihada inahitajika katika kutoa elimu ya magonjwa yasioambukiza pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha, mazoezi na kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya moyo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa moyo ni muhimu wananchi kufuata njia za kujikinga zaidi ikiwemo kuacha ulevi uliyopindukia, uvutaji sigara, tabia bwete pamoja na uzito uliyopindukia.

Ametoa rai kwa watalaamu wa afya, wasomi, vyombo vya habari pamoja na watunga sera kushiriki katika utoaji elimu kuhusu masuala ya afya.

Aidha,Makamu wa Rais amesema tafiti zinapaswa kufanyika kwa kina ili kubaini visababishi zaidi vya magonjwa ya moyo kwa kupata taarifa zaidi juu ya taratibu za kijamii na tabia za kiutamaduni katika mambo mbalimbali yaliyozoeleka kufanyika barani Afrika.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo kama vile kuimarisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kufanya tafiti za afya za kimkakati ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wananchi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa adimu.

Amesema, Taasisi ya Moyo ya jakaya Kikwete imeendelea kuimarika ambapo kwa sasa inafanya upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 800 kwa mwaka ikiwemo upausaji wa kufungua kifua (upasuaji mkubwa) ukilinganisha na wagonjwa 200 wakati ikianzishwa. Amesema zaidi ya wagonjwa laki mbili hutibiwa kwa mwaka huku zaidi ya 2400 wakitoa mataifa mengine.

Ameongeza kwamba serikali imeweza kuokoa zaidi ya bilioni 63 kila mwaka za matibabu ya wagonjwa wa moyo kutokana na kuimarishwa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Vilevile Makamu wa Rais amesema serikali itaongeza uwekezaji katika huduma za magonjwa ya moyo na kuandaa mipango ya awali, ubunifu, tafiti , mafunzo, ushirikiano, udhibiti na utoaji tiba wa magonjwa ya moyo nchini.

Mkutano huo wa siku mbili uliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete unawakutanisha Madaktari Bingwa, wataalam na wadau wa afya, wauguzi na watunga sera kutoka mataifa zaidi ya 40 duniani kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusu magonjwa ya moyo duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news