Mvua za Masika kugusa kila sekta, TMA yatoa ushauri kuepuka madhara makubwa

DAR ES SALAAM-Kutokana na mvua zinazotarajiwa, sekta ya usafiri na usafirishaji inatarajiwa kuathirika na kupelekea uharibifu wa miundombinu ya barabara na reli.
Mvua zikiwa zimeharibu miundombinu ya barabara. Picha na Bamiza).

Sambamba na ongezeko la ajali barabarani katika usafiri wa nchi kavu, kuchelewa au kusitishwa kwa safari za nchi kavu, ndege, majini.

Hayo yamebainishwa Februari 22, 2024 jijini Dar es Salaam na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TM) kupitia taarifa ya utabiri wa Masika 2024.

Vile vile, TMA imebainisha kuwa, hali hiyo inatarajia kusababisha mawasiliano hafifu angani na kwenye maji na kupelekea kuongezeka kwa gharama za uendeshaji katika usafiri wa anga, nchi kavu na majini.

"Mamlaka husika na wadau wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika utekelezaji wa matengenezo na ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza."

Nishati

TMA imefafanua kuwa, mvua zinazotarajiwa zitachangia kuongezeka kwa kina cha maji katika mito, maziwa na mabwawa hivyo matumizi sahihi ya maji majumbani na uzalishaji wa umeme ni muhimu kupewa kipaumbele.

Hata hivyo, kupungua kwa ubora wa maji, kuongezeka kwa kifusi cha mchanga maji na uharibifu wa kingo za mito na mtandao wa usambazaji maji pia unatarajiwa.

"Sekta ya Madini hususani shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, huenda zikaathirika, hivyo tahadhari za kiusalama ni muhimu kuchukuliwa ili kukabiliana na maporomoko ya ardhi na miamba.

"Mvua zinazotarajiwa huenda zikaathiri mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme na kupelekea kukosekana kwa umeme.

"Hivyo, mamlaka husika na wadau zinashauriwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali maji na mgawanyo wake kwa maeneo mbalimbali kama vile shughuli za uchakataji madini, uzalishaji umeme, matumizi ya viwandani na majumbani."

Taarifa

Wakati huo huo, vyombo vya habari vinashauriwa kupata, kufuatilia na kusambaza taarifa za utabiri na tahadhari, pindi tu zinapotoka ili jamii iweze kuzipata kwa wakati.

Vilevile, vinashauriwa kutafuta ushauri wa kitaalamu kutoka katika sekta husika wakati wa kuandaa, kutayarisha na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji.

"Pia, inapendekezwa kutumia lugha nyepesi wakati wa kuhabarisha jamii.

"Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji, afya.

"Shughuli za ujenzi (Makandarasi), uchimbaji madini, upakuaji na ushushaji mizigo Bandarini kuendelea kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalam katika sekta husika,"imeeleza taarifa hiyo ya TMA.

Aidha,Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imebainisha kuwa, itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua na hali ya hewa kwa ujumla nchini kadri inavyohitajika.

"Wadau wanashauriwa kuwasiliana na mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za mwelekeo na utabiri wa hali ya hewa ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao."

Mamlaka

Kwa mujibu wa TMA,vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha kutuama kwa maji na mafuriko.

Hali hii inaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu na upotevu wa maisha na mali.

"Mamlaka za miji na kamati za maafa zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kukabiliana na athari zinazohusiana na mafuriko ikiwa ni pamoja na shughuli za utafutaji, uokoaji na msaada wa kitabibu. "

Sekta ya Afya

TMA imebainisha kuwa, magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu ya maji unaoweza kusababishwa na maji ya mvua kutuama na kutiririka.

Hivyo,mamlaka za fya na jamii zinashauriwa kuchukua tahadhari stahiki ili kupunguza athari za kiafya zinazotarajiwa kwa kuharibu mazalia ya mbu, kutibu maji kabla ya kuyatumia, kunywa maji safi na salama pamoja na kuhakikisha uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kutosha katika vituo vya afya.

Sekta Binafsi

Aidha, Sekta binafsi inatarajiwa kunufaika na mvua zinazotarajiwa katika msimu huu wa Masika hususani katika shughuli za kilimo, uzalishaji viwandani, n.k.

Hata hivyo, wingi wa mvua unaweza kupelekea athari katika shughuli za ujenzi wa miundombinu, uhifadhi na usafirishaji wa mazao tete na bidhaa.

"Sekta binafsi zinashauriwa kushirikiana na wataalam mbalimbali ikiwemo wataalam wa hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

"Taasisi mbalimbali zikiwemo benki na bima zinashauriwa kuandaa na kutoa huduma mahususi kwa wadau ili kujenga ustahamilivu katika biashara."

Mvua kubwa

TMA imebainisha kuwa,vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kupelekea uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa mali na maisha.

"Hivyo, mamlaka husika katika idara mbalimbali na Idara ya Menejimenti ya Maafa nchini zinashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

"Aidha, sekta, mamlaka husika na kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji na mitaa zinashauriwa kushirikiana.

"Na kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa elimu na miongozo itakayohamasisha kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa, kukabiliana na maafa na kurejesha hali endapo maafa yatatokea."

Kwa mujibu wa TMA,kwa ujumla mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Aidha,ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Machi, 2024 katika maeneo hayo.

"Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara) pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo).

"Mvua za masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma."

Vile vile,mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuungana na mvua za Masika 2024.

TMA imebainisha kuwa,mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2024.

Wakati huo huo, kwa upande wa Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, TMA imebainisha kuwa,mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini.

"Mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024 na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2024."

Kwa upande waNyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani na zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024.

"Mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Mei, 2024,"imeeleza taarifa hiyo ya TMA.




Kwa mujibu wa TMA, mvua za msimu zilizoanza mwezi Novemba, 2023 zimenyesha kwa kiwango cha juu ya wastani katika mikoa ya Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Katavi, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara na Kusini mwa mkoa wa Morogoro na wastani katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe na Njombe katika kipindi cha Novemba, 2023 hadi Januari, 2024.

Mvua hizi zilianza mapema wiki ya kwanza na ya pili mwezi Novemba, 2023 na zilitawaliwa na vipindi vya mvua nyingi zilizochangiwa na uwepo wa El Niño.

Katika kipindi kilichosalia cha msimu kuanzia Februari hadi Aprili, 2024 mvua zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa mwezi Oktoba, 2023, ambapo kwa ujumla mvua zilitabiriwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Aidha, mamlaka hiyo imefafanua kuwa,msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro).

Pia, Pwani ya Kaskazini (Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news