Rais Dkt.Samia atoa pole ajali iliyoua watu 15 Arusha leo

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 vilivyosababishwa na ajali jijini Arusha leo.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyabainisha hayo leo Februari 24,2024 kupitia taarifa aliyoitoa katika kurasa zake za kijamii.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 katika ajali iliyohusisha magari manne eneo la Ngaramtoni, mkoani Arusha.

"Natuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliopoteza jamaa zao katika katika ajali hii.

"Ajali hizi zinachukuwa wapendwa wetu, nguvu kazi ya Taifa na mihimili ya familia.

"Naendelea kutoa wito kwa kila mmoja kuzingatia sheria za usalama barabarani katika matumizi ya vyombo vya moto.

"Naagiza vyombo vyetu vya ulinzi, usalama na udhibiti kuendelea kuhakikisha vinasimamia sheria kikamilifu, ikiwemo ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri na udhibiti wa leseni kwa madereva wanaorudia kuvunja sheria mara nyingi na wakati mwingine kusababisha watu kupoteza maisha.

"Mwenyezi Mungu azilaze roho za ndugu zetu hawa mahali pema peponi. Amina,"ameeleza Rais Dkt.Samia.

Aidha,chanzo cha ajali hiyo inadaiwa ni baada ya lori lenye tela kuacha njia na kuparamia magari matatu ambayo ni Coster,Hiace na gari binafsi lililokuwa limepakia raia wa kigeni ambao wawili kati yao wanahofiwa kufariki dunia eneo la tukio.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru huku majeruhi wakipelekwa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya ALMC na Mount Meru.

Akitoa taarifa hiyo katika eneo la ajali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polis, SACP Justine Masejo amesema ajali hiyo imetokea leo Februari 24,2024 muda wa saa 11 jioni ambapo ilihusisha lori na magari madogo matatu katika eneo la Ngaramtoni Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.

Kamanda Masejo amesema wanaendelea na uchunguzi wa kina juu ya ajali hiyo ili kubaini chanzo halisi cha tukio.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news