UNICEF yaahidi mema zaidi kwa Tanzania

NA ASIA SINGANO 
WF

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), limeahidi kuisaidia Tanzania kwenye masuala ya Lishe ili kukabiliana na Udumavu wa watoto ambao unaathari katika ukuaji wa ubongo na uchumi.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (wa nne kulia), na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch (wa tatu kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka UNICEF na Tanzania, baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Naibu Waziri huyo na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha).

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akishauri kuhusu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), kusaidia masuala ya kibajeti, wakati wa mkutano kati yake na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika hilo, Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.

Mhe. Chande, alisema kuwa Shirika hilo limekuwa likiisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ya kibajeti ambapo katika mwaka wa fedha 2023/ 2024, lilitoa dola za Marekani milioni 20.3 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 50 za Tanzania.
Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, akieleza nia ya Shirika hilo kuwekeza katika lishe kwa lengo la kuondoa udumavu na kuchochea ukuaji wa uchumi, alipokutana na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (hayupo pichani), kwa lengo la kujitambulisha, jijini Dodoma.

Mhe. Chande ameliomba Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake inazozifanya kuboresha maisha ya wananchi wake na kujikwamua kiuchumi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, akizungumza jambo wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.

Aidha,amelishukuru Shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali na aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Shirika hilo wakati likitimiza kazi zake nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, alisema UNICEF inaahidi kuwekeza kwenye lishe ya Watoto ili kusaidia kuondoa udumavu kwa kuwa udumavu unaathari katika ukuaji wa ubongo wa mtoto na pia kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (wa pili kulia), na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka UNICEF, jijini Dodoma.

Alisema kuwa Shirika lake linajitahidi kuhakikisha linasaidia masuala ya kibajeti na program zinazoendelea nchini Tanzania kwa kuwa lengo lao ni kusaidia katika maendeleo ya watoto na wanawake kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na UNICEF kama Wakala wake.

Bi. Wisch alisema kuwa, amekuja kujitambulisha lakini pia kuelezea maeneo ambayo watawekeza kwa kushirikiana na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watoto pamoja na sekta za fedha.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiagana na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, baada ya kujitambulisha ambapo walijadiliana pia maeneo mbalimbali ya kukuza ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo jijini Dodoma.

Aidha, aliipongeza Tanzania kwa ushirikiano inaouonesha kwa Shirika hilo na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo katika suala la lishe ya watoto na wanawake lakini pia suala la elimu, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news