Waziri Simbachawene aridhishwa na utendaji kazi wa eGA, asisitiza kasi

IRINGA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) huku akiitaka iongeze kasi zaidi katika kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwa umma kwa haraka na ufanisi.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na watumishi wa eGA-Kituo cha Iringa ambapo amewataka Watumishi hao kuhakikisha Serikali inaendeshwa kidigitali kwenye kila nyanja kupitia mifumo wanayoisanifu.

Amesema eGA ni taasisi muhimu katika dunia ya sasa ambapo Serikali inahitaji mapinduzi ya TEHAMA ili itoe huduma zake kwa wananchi kiurahisi na kwa haraka.

“Dunia inakwenda kasi na teknolojia ni kila kitu kwa sasa, hivyo ni muhimu kwa eGA kufanya utafiti, kubuni na kutengeneza mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma” amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa eGA imeweka juhudi kubwa katika kusimamia TEHAMA Serikalini na imetengeneza na inaendelea kutengeneza mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka, mahali popote na kwa gharama nafuu na kuchagiza utawala bora.

Aidha, Mhe. Simbachawene ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao katika ofisi zake zilizopo Iringa na amewataka watumishi wa Mamlaka kwa jumla kuendelea kubuni Mifumo ya TEHAMA inayotatua changamoto zilizopo nchini pamoja na kuwa wazalendo kwa maslahi ya Taifa.
Vile vile, amewasisitiza watumishi wa eGA kuhakikisha mifumo inayotengenezwa na iliyopo inakuwa na uwezo wa kuwasiliana ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Simbachawene kwa kutenga muda wake kutembelea kituo hicho cha Iringa na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news