Askari wanandoa waliofariki kwa ajali waombewa kwa kufanyiwa ibada

ARUSHA-Mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Arusha TPF-Net katika kuelekea siku ya wanawake Duniani leo wamefanya ibada maalumu kwa ajili ya kuwaombea Askari Polisi wanandoa waliofariki Dunia kwa ajali ya gari siku mbili baada ya kufunga ndoa.
Akiongea mara baada ya ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Theresia Jijini Arusha Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoani humo Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Happiness Temu amesema mtandao huo umekuwa na utaratibu wa kuyakumbuka makundi mbalimbali yenye uhitaji katika jamii ambapo kwa mwaka huu waliona ni vyema kuwakumbuka Askari waliofariki kwa ajali.

ASP Temu amebainisha kuwa wameamua kufanya Ibada hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwaombea marehemu hao ambao walikua wanafanya nao kazi mkoani humo kabla kupatwa na umauti Desemba 20, 2022 ambapo pia katika ibada hiyo wamewaombea Watoto wawili ambao waliachwa na marehemu.
Nao baadhi ya askari wa mtaandao huo waliofanya kazi kwa Karibu na marehemu wamebainisha Pamoja na kuwaombea marehemu, pia wametumia ibada hiyo kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuwalinda katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake Mrakibu wa Polisi SP Asia Matauka ambaye anafanya kazi katika Mkoa wa Kilimanjaro amesema mara baada kusikia juu ya uwepo wa ibada hiyo aliona ni vyema kuungana na mtaandao huo kuwaombea marehemu.
Askari waliofariki na kufanyiwa ibada leo ni Konstebo Noah Simfukwe na Agness Martin.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news