Balozi Kairuki:Nitamkumbuka Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa haya

LONDON-"Nilipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini China mwaka 2017 kabla sijakwenda kuripoti kwenye kituo changu cha kazi moja ya watu niliokwenda kuwaaga alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki.

Katika nasaha zake kwangu aliniambia maneno machache ambayo yalikuwa chachu katika utekelezaji wa majukumu yangu ya uwakilishi wa nchi yetu.

Aliniambia hivi ninanukuu "Unakwenda China kwa marafiki zetu wa jadi. Wenzio waliokutangulia- wameyaimarisha mahusiano yetu na Wachina kwa miaka mingi- na wewe nenda ukayaimarishe.

"Lakini ikitokea kazi ya kuyaimarisha imekushinda, basi yaache pale pale ulipoyakuta- yasirudi nyuma"...

Maneno yale ndio yalikuwa yakinipa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili mahusiano hayo yasirudi nyuma bali yaimarike zaidi- sikutaka kumuangusha Mzee Mwinyi.

Mwezi Novemba mwaka jana alipokuwa hapa London kwa ajili ya matibabu nilimkumbusha nasaha alizonipa mwaka 2017.... alifurahi sana kwamba nilizingatia ushauri wake-- kisha akaniambia na hapa Uingereza uendelee kufanya hivyo hivyo.

Watu wengi wamemuelezea vizuri Mzee Mwinyi alivyokuwa jasiri, mnyenyekevu, muungwana, mzazi na mlezi.

Ameelezewa pia alivyofanya mageuzi ya kiuchumi na kufungua nchi. Mfano mmoja (close to home) ni namna alivyotoa kibali cha kufunguliwa Hospitali Binafsi ya TAG Mikocheni Hospital (ambayo hivi sasa inajulikana kama Kairuki Hospital).

Marehemu Prof. Hubert Kairuki alipata wazo la kuanzisha hospitali katika miaka ya 80 kipindi ambacho Sheria ilikuwa hairuhusu watu binafsi kuanzisha hospitali isipokuwa taasisi za dini.

Prof Kairuki aliamua kushirikiana na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ili kufanikisha azma hiyo.

Hata hivyo watendaji ndani ya Wizara ya Afya waliokuwepo wakati huo walimshawishi Waziri wa Afya aliyekuwepo wakati huo asikubali kutoa kibali... na huo ndio ulikuwa ni uamuzi wa mwisho wa Waziri- hakutaka kusikiliza habari ya hospitali hiyo.

Mzee Mwinyi alipata taarifa ya changamoto hiyo kutoka kwa Mpambe wake (ADC) Marehemu Colonel Thabit.

Baada ya kusikia habari hiyo Mzee Mwinyi alimuita Marehemu Prof Kairuki na kumtaka amsimulie yaliyomsibu.

Baada ya kusikiliza- Mzee Mwinyi alitoa idhini mwenyewe kwamba Hospitali ifunguliwe na akamuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Marehemu Hemed Mkali akaifungue kwani watu wa Wizara ya Afya walikuwa na kinyongo. Shughuli hiyo ilifanyika tarehe 17 Machi 1987.

Sina shaka kwamba, kama sio Mzee Mwinyi kufanya uamuzi ule- leo hii Kairuki Hospital na taasisi nyingine kama HKMU, KPIL zisingekuwepo.

Funzo kubwa alilotuachia Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi hususan wenye dhamana za kutumikia wananchi katika ngazi mbalimbali - tunapaswa kuwa na usikivu, unyenyekevu na kutenda haki.

Ubabe, umaarufu binafsi wa muda mfupi sio sifa nzuri na za kudumu kwa mtumishi wa umma.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Hayati Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi Mahala Pema Peponi. AMEN."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news