GBT yatunisha pato la Taifa, fursa za ajira nchini

NA GODFREY NNKO

SEKTA ya michezo wa kubahatisha nchini imeendelea kuchangia mapato ya Serikali kutoka shilingi bilioni 33.6 mwaka wa fedha 2016/17 hadi kufikia shilingi bilioni 170.4 mwaka 2022/23 huku katika mwaka huu wa fedha wakitarajia kufikia zaidi ya shilingi bilioni 200.
Hayo yamesemwa leo Machi 6, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini (GBT), James Mbalwe katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

GBT ni kati ya taasisi na mashirika ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo leo ilikuwa zamu yao kuelezea umma kuhusu walipotoka, walipo na wanapoelekea.

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Mbalwe amefafanua kuwa,ongezeko hilo ni wastani wa asilimia 407.1 kwa mwaka katika kipindi hicho.

Amesema, katika mwaka wa fedha 2016/17 kiasi kilichokosanywa kupitia michezo hiyo ni shilingi bilioni 33.64 huku mwaka 2017/18 ikikusanywa mapato ya shilingi bilioni 78.77 sawa na ongezeko la asilimia 134 kwa mwaka.

“Na kwa mwaka 2018/19 kiasi kilichokusanywa kilikuwa shilingi bilioni 95.85 na mwaka 2019/20 zikakusanywa shilingi bilioni 89.09 huku kwa mwaka 2020/21 zikikusanywa shilingi bilioni 131.99 sawa na ongezeko la asilimia 48 kwa mwaka.”

Mbalwe ameendelea kubainisha kuwa, kwa mwaka 2021/22 zilikusanywa shilingi bilioni 148.9 sawa na ongezeko la asilimia 12.8 kwa mwaka.

Vile vile kwa mwaka wa fedha 2022/23 zilikusanywa shilingi bilioni 170.4 sawa na ongezeko la asilimia 14.5 kwa mwaka huku kwa mwaka wa fedha 2023/24 katika kipindi cha Julai hadi Desemba zikikusanywa shilingi bilioni 108.16.

Katika hatua nyingine, Mbalwe amesema, sekta hiyo imefanikiwa kuzalisha ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi zipatazo zaidi ya 25,000.

‘Hivyo, sekta hii imefanikiwa kutoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa ajira nchini.Mapato ya Serikali yatokanayo na kodi ya biashara ya michezo ya kubahatisha yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.”

GBT ni nini?

Mbali na hayo amesema, GBT ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.4 ya 2003 (Gaming Act No.4 of 2003).

Sheria ambayo, Mbalwe amesema ilifuta Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa (BNT) na kuanzisha Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, GBT ilianza kazi zake rasmi Julai Mosi, 2003. “Tofauti na BNT ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya udhibiti na wakati huo huo ikiendesha michezo ya bahati nasibu, GBT yenyewe imepewa jukumu la kusimamia, kuratibu na kudhibiti uendeshaji wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini na haijihusishi na uendeshaji wa michezo hiyo.”

Wakati huo huo amesema, bodi hiyo imesajili jumla ya kampuni 91 zinazoendesha biashara za aina mbalimbali ya michezo ya kubahatisha nchini.

"Hadi kufikia mwezi Juni, 2023, GBT imesajili jumla ya kampuni 91 zinazoendesha biashara za aina mbalimbali ya michezo ya kubahatisha nchini, leseni zote ni za muda wa mwaka mmoja isipokuwa ile ya kuendesha BNT ambayo ni ya miaka minane.

"Na leseni uhuishwa baada ya muda kuisha,kampuni moja inaweza kuendesha zaidi ya aina moja ya michezo ya kubahatisha,"amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Pia, amesema mwendeshaji sharti awe na leseni hai iliyotolewa na bodi hiyo, na michezo hiyo hairuhusiwi kuendeshwa katika maeneo yaliyopo karibu na nyumba za ibada, shule, usalama na maeneo yasiyofikika kirahisi.

Changamoto

Pia, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, licha ya mafanikio waliyoyapata wameendelea kupitia changamoto mbalimbali.

Miongoni mwa changamoto hizo ameswema ni pamoja na kuwepo kwa wimbi la waendeshaji wa michezo ya kubahatisha hususani wa mashine za sloti ambao hawana usajili wa bodi.

“Waendeshaji hawa wamekuwa wakiingiza nchini mashine za kamari kinyume na tararibu zilizowekwa kisheria.

“Hali hii inapelekea kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali.” Amesema, katika kipindi cha kati ya mwaka 2018/19 hadi Agosti, 2022 GBT ilifanikiwa kukamata mashine zipatazo 1,846 katika maeneo mbalimbali nchini.

“Endapo mashine hizi zisingedhibitiwa zingeweza kuikosesha Serikali mapato yanayofikia shilingi bilioni 2.44 kwa mwaka.

“Waendeshaji hawa pia, wamekuwa wakiendesha biashara yam ashine hizi kiholela katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria na hivyo kuleta usumbufu kwa jamii, kuwepo uwezekano wa Watoto kushiriki na hivyo kuharibu taswira ya sekta hii.”

Ameongeza kuwa, bodi hiyo katika kaguzi zake za mara kwa mara imekuwa ikiwabaini waendeshaji hususani wa mashine za sloti ambao wanaweka mashine zao kwenye maeneo yasiyosajiliwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linaharibu taswira ya michezo ya kubahatisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news