Hifadhi za Taifa zavunja rekodi ya watalii, Serengeti yaongoza

DODOMA-Serikali imesema kuwa, licha ya makadirio ya idadi ya watalii kwa hifadhi zote za Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa mwaka 2023/24 kuwa 1,387,987, hadi kufikia Februari 2024 (miezi nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii 1,451,176 wameshaingia huku Serengeti ikiwa na wengi zaidi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi ameyasema hayo leo Machi 10,2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanahabari ambapo ametoa taarifa ya mafanikio ya ongezeko la watalii nchini.

"Itakumbukwa kwamba tangu mwezi Oktoba 2023 nchi yetu ilianza kupata mvua kubwa za El Nino ambazo hadi sasa bado zinaendelea katika baadhi ya maeneo nchini.

"Moja ya athari za mvua hizo ni uharibifu wa miundombinu, ikiwemo barabara za kwenye hifadhi za taifa zilizo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ikiwemo Serengeti."

Amesema, kwa eneo la Kaskazini mwa nchi ambako ndiko Serengeti ilipo, El Nino ilikuja wakati wa majira ya mvua za vuli za Oktoba hadi Desemba na kisha kuendelea kunyesha na kuunganisha na majira ya mvua za masika ya Machi hadi Mei.

Msemaji Mkuu huyo, amesema kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ingawa chanzo cha El Nino, ambacho ni ongezeko la joto katika bahari ya Pasifiki bado kipo lakini sasa kinaendelea kupungua. 

Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa kuna visababishi na viashiria vingine vya mvua kubwa, bado mvua hizi zitakuwa ni za wastani au zaidi, ikimaanisha mvua zitakuwa kubwa kuliko ilivyozoeleka.
"Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo pia imeathirika na El Nino, ni hifadhi ya pili kwa ukubwa nchini yenye kilomita za mraba 14,763. Hifadhi kubwa zaidi nchini ni Ruaha yenye kilomita za mraba 19,822 lakini Serengeti ndiyo hifadhi ya kwanza nchini kwa kuingiza watalii wengi zaidi.

"Hadi sasa, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo. 

"Serengeti ni maarufu zaidi kwa tukio la uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu ambapo kila mwaka nyumbu wapatao milioni 1.5 hutumia miezi kumi wakizunguka ndani ya hifadhi ya Serengeti na kisha kwenda nchi jirani na kurejea."

Amesema,katika uhamaji huo tukio la kusisimua zaidi ambalo ndilo huvuta watalii wengi ni lile la kuvuka mto Mara pamoja na matawi yake.

Serengeti ambayo ilianzishwa mwaka 1959, ni kati ya hifadhi chache Afrika na duniani ambapo mtalii anaweza kuona wanyama wote watano maarufu, yaani simba, chui, tembo, nyati na kifaru. 

Wanyama wengine wengi hifadhini Serengeti ni pamoja na pundamilia, twiga, jamii ya swala, duma, viboko na mamba.
TANAPA inasimamia na kuendeleza jumla ya hifadhi 21 zenye ukubwa wa kilomita za mraba 98,908.88 - sawa na asilimia 10.2 ya eneo zima ya Tanzania.

Hifadhi hizo ni Arusha (Arusha), Burigi-Chato (Geita na Kagera), Gombe (Kigoma), Ibanda-Kyerwa (Kagera), Katavi (Katavi), Kilimanjaro (Kilimanjaro), Kitulo (Njombe na Mbeya), Mahale (Katavi na Kigoma), Manyara (Arusha na Manyara), Mikumi (Morogoro),

Mkomazi (Kilimanjaro na Tanga), Ruaha (Iringa, Dodoma na Mbeya), Kisiwa cha Rubondo (Geita na Kagera), Rumanyika-Karagwe (Kagera),

Saadani (Pwani na Tanga), Kisiwa cha Saanane (Mwanza), Serengeti (Mara, Arusha na Simiyu), Tarangire (Dodoma na Manyara), Milima ya Udzungwa (Morogoro na Iringa), Mto Ugalla (Tabora na Katavi) na Nyerere (Pwani, Morogoro na Mtwara).

Amebainisha kuwa, TANAPA ina jukumu la kuendelea kuhifadhi wanyamapori, bioanuai na makazi ya wanyama katika hifadhi za taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo; na pia kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii katika hifadhi zote za taifa.

"Katika kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi, TANAPA imefanikiwa kutoa mchango mkubwa katika idadi ya watalii ambapo kwa mwaka 2022 ilichangia watalii 697,264 kati ya 1,454,920 walioingia nchini."

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Utalii la Dunia (World Travel and Tourism Council – WTTC) kwenye ripoti ya Tanzania ya mwezi Februari 2023, asilimia 90.7 ya wageni wanaoingia nchini hutembelea vivutio vya hifadhi za taifa, hifadhi ya Ngorongoro na fukwe za Zanzibar.

ONGEZEKO LA WATALII KATIKA HIFADHI YA SERENGETI

Msemaji Mkuu wa Serikali amefafanua kuwa, jufuatia mafanikio makubwa ya filamu ya Royal Tour – ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe alikuwa mshiriki mkuu, idadi ya watalii wanaokuja Serengeti sasa imekwenda juu kupita malengo makubwa yaliyowekwa kwa mwaka huu wa fedha.

"Taarifa ya mafanikio hayo ni kwamba, ingawa makadirio ya idadi ya watalii kwa hifadhi zote za TANAPA kwa mwaka 2023/24 yalikuwa 1,387,987.

"Lakini mpaka kufikia Februari 2024 (miezi nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii 1,451,176 wameshaingia huku Serengeti ikiwa na wengi zaidi."

MIUNDOMBINU YA SERENGETI

Amesema, hifadhi za taifa 21 zilizo chini ya TANAPA zina barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 16,470.6 ambapo Serengeti peke yake ina jumla ya kilomita 3,176.

"Kimsingi ndiyo hifadhi yenye mtandao mrefu zaidi wa barabara ambazo ni za udongo ama changarawe.

"Barabara hizi zimegawanyika katika barabara kuu ilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) na kundi la pili la barabara ndogondogo zilizo chini ya TANAPA yenyewe.

"Serengeti pia ina viwanja vidogo vya ndege (airstrips) vipatavyo saba ambavyo ni Serengeti, Kogatende, Lobo, Lamai, Grumeti, Kusini na Fort Ikoma.

"Hivyo basi, watalii wanaokuja Serengeti huja ama kwa njia ya barabara au ndege ndogo kutoka maeneo mbalimbali nchini yanayopokea wageni kutoka nje au kutoka kwenye vivutio vingine kama fukwe."

Amesema,TANAPA yenyewe ndiyo huzitunza barabara hizi na viwanja vya ndege ili kuhakikisha kwamba watalii wanaendelea kuingia hifadhini.

TANAPA hutumia wataalam wake pamoja na vifaa vyake. Na kwa mujibu wa sera yake ya uhifadhi, TANAPA hutumia changarawe kutoka ndani ya hifadhi kwa ajili ya matumizi endelevu, kupunguza gharama na kuepuka kuingiza mimea-vamizi ambayo huharibu malisho ya wanyama na pia kuleta magonjwa ya mimea.

"Katika mtandao wa kilomita 3,176 za barabara za Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,kilomita 2,407 ni za udongo na kilomita 769 ni za changarawe. Kutokana na hoja kadha wa kadha za kiuhifadhi hakuna barabara za lami wala zege."

Amesema,maji yanayotumika katika matengenezo ya barabara hizo hutoka kwenye visima badala ya mabwawa na mito iliyopo hifadhini ili kuwaachia wanyama maji hayo
ambayo ni muhimu kwa uhai.

"Pale ilipotokea changamoto ya mvua za El Nino kulitokea mafuriko makubwa hifadhini kiasi cha kufunika barabara kuu zinazoleta watalii.

"Uharibu ulikuwa mkubwa. Hivyo basi, TANAPA ilichukua hatua za haraka za awali za kuzifanyia matengenezo barabara hizo ili kuhakikisha kwamba wageni wanaendelea kutalii na usafirishaji haukwami."

MATOKEO YA JUHUDI ZA TANAPA

"Napenda kuchukua nafasi hii kuufahamisha umma na wadau wa sekta ya utalii kwamba TANAPA katika hatua za awali imekamilisha matengenezo na sasa barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma zinazostahili.

"Hakuna changamoto kubwa iliyotokea kwenye upande wa viwanja vidogo vya ndege saba vilivyopo zaidi ya maji kujaa kwenye baadhi ya maeneo ya kuegeshea ndege.

"Hivyo baada ya maji hayo kukauka, huduma ziliendelea kwa usalama.Aidha, kwa hatua za kati TANAPA inataka kunyanyua barabara nzima ya Golini– Naabi – Seronera (km 68) kwa wastani wa sentimita 50 (nusu mita).

"Kufuatana na ukaguzi uliyofanyika ili kuifanya iwe juu kidogo ya usawa wa ardhi, hivyo kuruhusu maji kutoka barabarani yapite kwenye mifumo ya mifereji na mitaro maji iliyopo pembezoni mwa barabara. Kazi hii inaendelea."

NJIA MBADALA ZA UTATUZI WA MUDA MREFU

"Lakini baada ya matumizi ya miaka takriban 65 malighafi hizi za changarawe na maji, sasa zimepungua na kusababisha matengenezo kugharimu fedha nyingi na kuhatarisha uhifadhi.

"Hivyo basi, kwa kuangalia hatua za muda mrefu, TANAPA inatafuta njia mbadala za kuzitunza barabara hizi. Njia hizi mbadala ni zile za kuweka tabaka gumu kama la zege au lami.

"Kwa kuzingatia kanuni za uhifadhi, TANAPA na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaandaa andiko la kitaalam la kuwasilisha kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusiana na suala la kuweka tabaka gumu kwani Serengeti imo katika Orodha ya Urithi wa Dunia inayosimamiwa na Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO.

"Njia ya kutumia andiko la kitaalam ndiyo iliyotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambapo sasa imepata kibali cha kujenga barabara yenye tabaka gumu.

"Barabara hiyo ndiyo pia inayoingia hifadhini Serengeti kwa kuzingatia kuwa vivutio hivi viwili maarufu duniani vinapakana.

Kuna barabara kuu nne zenye changamoto zaidi kutokana na upitaji wa magari makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda mikoa ya jirani ya Mara, Arusha,Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambazo TANAPA ndizo inazozilenga katika mkakati wake wa mbinu mbadala ya tabaka gumu iwapo itakubalika."

Amesema, barabara hizo pia hupitisha magari ya watalii kati ya 600 hadi 800 kwa siku,hivyo kuharibika mara kwa mara hata kama hakuna mvua kubwa.

Barabara hizo zenye jumla ya kilomita 291 tu (asilimia 9) kati ya kilomita 3,176 za mtandao wa barabara katika hifadhi nzima ni kama ifuatavyo:

Ø Golini – Naabi - Seronera (km 68)

Ø Seronera – Lango la Ndabaka (km 121)

Ø Seronera – Lango la Ikoma (km 30)

Ø Banagi (Seronera) – Lobo – Lango la Kleins (km 72).

Amesema,TANAPA inatarajia kwamba utatuzi wa kudumu utapatikana katika barabara kuu zinazoihudumia Serengeti na hivyo kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kiasi kikubwa kufuatia matunda ya filamu ya Royal Tour.

TAARIFA ZA ZIADA

Takwimu za watalii 1,451,383 walioingia nchini kati ya Julai 2023 na Februari 2024 kwa mgawanyo wa wanakotoka ni kama ifuatavyo:

o Watalii kutoka nje ya nchi za Afrika Mashariki = 749,365

o Watalii wageni lakini wakaazi wa nchini Tanzania = 10,531

o Watalii wa Afrika Mashariki wakiwemo Watanzania = 230,785.(Idadi hii ya watalii 230,785 ina watalii Watanzania = 127,650)

o Wafanyakazi wa hoteli, kambi na madereva = 460,702.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news