Kamati yaonesha kutoridhishwa urejeshaji fedha za mikopo ya KKK

NA MUNIR SHEMWETA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imesema kuwa, haijaridhishwa na urejeshaji mikopo ya fedha za mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK) unaofanyika kwenye halmashauri mbalimbali nchini.
Mbunge wa jimbo la Chalinze na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe, Ridhiwani Kikwete akimkabidhi Hati Milki ya Ardhi mmoja wa wananchi wa Chalinze wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi eneo la Chalinze machi 18, 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Hayo yamebainishwa leo tarehe 18 Machi 2024 na Kamati hiyo wakati ilipotembelea na kukagua utekelezaji mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Msolwa katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava ameeleza kuwa, mbali na Kamati yake kuridhishwa na mradi wa KKK kwa ujumla lakini hawajaridhishwa na namna mikopo hiyo inavyorejeshwa na halmashauri.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe, Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze Machi 18, 2024.

Akitolea mfano wa Halmashauri ya Chalinze katika mkoa wa Pwani, Mhe, Mzava amesema pamoja na halmashauri hiyo kukopeshwa kiasi cha shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa KKK lakini imeshindwa kurejesha fedha kwa wakati.

‘’Kama Kamati bado hatujaridhishwa kabisa namna ya kasi ya urejeshaji fedha hizi na wito na msisitizo wetu zifanyike kila aina ya jitihada kuhakikisha fedha zinarudi ili zikasaidie maeneo mengine yenye uhitaji ili dhamira ya Rais ya kutoa fedha hizo iweze kufikiwa,’’ alisema Mzava.

Kwa mujibu wa Mhe, Mzava, hadi Machi 2024 kwa ujumla wizara imepokea marejesho ya shilingi bilioni 22.7 kati ya shilingi bilioni 50 sawa na asilimia 45 kutoka kwenye halmashauri na taasisi mbalimbali zilizonufaika na mkopo huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon mara baada ya Kamati yake kuwasili mkoa wa Pwani kukagua utekelezaji Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani tarehe 18 Machi 2024. Katikati ni Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda.

Amesema, fedha zinazotolewea kama mkopo usio na riba kwa halmashauri zikirejeshwa zitasaidia kukopesha halmashauri nyingine na hivyo kuisaidia kutatua changamoto za sekta ya ardhi nchini na kuboresha katika maeneo mengine.

Hata hivyo, ametaka kufanyika jitihada mbalimbali ili kusaidia katika urejeshaji mikopo hiyo na kuweza kuzisaidia halmashauri nyingine ili ziweze kuondoa changamoto za sekta ya ardhi nchini.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Deo Msilu (Kulia) akielezea matumizi ya kifaa cha upimaji mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika eneo la Msolwa Chalinze Machi 18, 2024.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amebainisha kuwa, mpaka sasa halmashaurii zilizorejesha kiasi chote cha fedha ya mkopo ni 12 huku zile zilizorejesha sehemu ya fedha zikiwa ni 43.

Mhe, Pinda amesema, Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) ni program ya miaka kumi inayotekelezwa na wizara yake kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Deo Msilu akisisitiza jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika eneo la Msolwa Chalinze Machi 18, 2024.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa Programu hiyo ulianza mwaka 2018/2019 na unatarajiwa kukamilika 2028/2029. Lengo la Programu ya KKK ni Kupanga miji na kuhakikisha makazi holela yanaondolewa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Programu hiyo inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ambazo ni mamlaka za upangaji na sekta binafsi ambapo program hiyo inagharimiewa na serikali kupitia fedha za ndani za bajeti ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda wakimsikiliza Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Deo Msilu (wa pili kulia) kuhusu mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi unaotekelezwa katika eneo la Msolwa Halmashauri ya Chalinze Machi 18, 2024.

Serikali ilitoa mtaji wa shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa program ya KKK kwa utaratibu wa kuzikopesha halmashauri na taasisi ambapo wizara kwa kushirikiana na wizara ya fedha na Ofisi ya Rais TAMISEMI ziliweka utaratibu kwa kuweka vigezo vya kutoa mkopo huo bila riba kwa ajili ya utekelezaji wa program.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news