Mapori ya akiba saba mambo safi, TAWA yagusa maisha

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority-TAWA) imebainisha kuwa,kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa kutatua migogoro ya mipaka katika mapori ya akiba saba kati ya nane nchini.
Hayo yamesesemwa leo Machi 18, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna wa mamlaka hiyo, Mabula Misungwi katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"TAWA imeendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kupitia Kamati ya Mawaziri nane wa wizara za kisekta.

"Kwa kushirikiana na wananchi migogoro ya mipaka katika Mapori ya Akiba saba ya Swagaswaga, Mkungunero, Wamimbiki, Igombe, Liparamba, Mpanga Kipengere na Selous kati ya nane yaliyotolewa maelekezo na kamati ya mawaziri nane wa kisekta imemalizika."

Amesema kuwa,jumla ya vigingi 1,681 vimesimikwa kuzunguka mipaka ya hifadhi. 

"Aidha katika utatuzi wa migogoro hiyo eneo lenye ekari 103,544.48 limemegwa kutoka kwenye hifadhi na kuwapatia wananchi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

"Sambamba na hilo, Serikali kupitia TAWA inaendelea kukamilisha zoezi la kulipa fidia kaya 145 zilizo katika Pori la Akiba Mkungunero."

Wakati huo huo, Kamishna Mabula amebainisha kuwa,kutokana na ongezeko la matukio ya wanayapori wakali na waharibifu kati ya mwaka 2021-2024 TAWA imefanya jumla ya doria 58,818 kukabiliana na matukio 8,001 yaliyotokea katika wilaya 73 nchini.

Amefafanua kuwa, jitihada nyingine zilizofanyika ili kupunguza madhara kwa maisha ya watu na mali zao ni pamoja na kujenga vituo 16 vya askari katika wilaya 16 ili kuitikia kwa haraka matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Pia, wamefanikiwa kununua pikipiki 50 na kutoa mafunzo na kushirikisha Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (Village Game Scout) na Jeshi la Akiba wapatao 184.

Askari waliopata mafunzo ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanafanya kazi kwenye maeneo sugu ya matukio ambayo yanajumuisha Bunda, Busega, Meatu, Same, Lindi, Korogwe,Itilima, Liwale, Nachingwea, Mwanga, na Tunduru.

Mafanikio mengine, Kamishna Mabula amesema ni kuongeza vituo vya muda vya askari (ranger stations) kutoka 46 hadi 55.

Vile vile, kuongeza idadi ya askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kutoka 139 hadi 237 na ujenzi wa mabwawa 10 katika mapori ya akiba Kizigo-09 lililopo Manyoni na Mkungunero-01 katika Wilaya ya Kondoa.

"Na tumeendelea kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu rafiki za kujikinga na madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi 764,438 katika vijiji 1,319 nchini.

"Mafanikio mengine ni kuimarisha vikundi 179 vya wananchi vya kufukuza tembo na kutoa vifaa vya kufukuza tembo ikiwemo roman candles 1,320, thunder flashes 1,310, vuvuzela 548, filimbi 288, tochi 524, mbegu za pilipili, mabomu ya pilipili.

"Ikiwemo kufunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa makundi ya tembo nane katika wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwe."

Kamishna Mabula amesema, pia wamefanikiwa kuimarisha mawasiliano kwa kutoa namba ya kupiga simu bure ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa mapema.

Amesema, kufuatia juhudi hizo madhara hasi ikiwemo idadi ya vifo imepungua kutoka vifo 318 kati ya mwaka 2017-2020 hadi vifo 259 kati ya mwaka 2021-2024 licha ya kuongezeka kwa matukio.

Vile vile, amesema ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za uhifadhi umeongezeka huku wakifanikiwa kuwezesha miradi ya maendeleo kwa jamii katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati huo huo, Kamishna Mabula amesema, TAWA imeendelea kushirikiana na jamii katika shughuli za uhifadhi kwa kuchangia miradi ya maendeleo inayoibuliwa na jamii kwenye maeneo mbalimbali hususani yanayozunguka Mapori ya Akiba.

Amesema, kati ya mwaka 2021 na 2024 TAWA imechangia miradi ya jamii yenye thamani ya shilingi milioni 193.3 ikiwemo ujenzi wa soko la samaki katika mji mdogo wa Ifakara huko Kilombero ambalo liligharimu shilingi milioni 66.

Mchango mwingine, amesema ni ujenzi wa darasa, ofisi ya walimu pamoja na ununuzi wa madawati katika Shule ya Msingi Usinge Kaliua mkoani Tabora vikiwa na thamani ya shilingi milioni 50.

Kamishna Mabula amesema, pia wamechangia madawati 100 katika Wilaya ya Bunda,ununuzi wa mashine mbili za kusaga katika Mkoa wa Mara na kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na darasa huko Mwibara.


Vile vile, TAWA wamechangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Bungo iliyopo Korogwe mkoani Tanga na kuwezesha jamii kunufaika na uvuvi na ufugaji nyuki katika hifadhi

"TAWA imeweka utaratibu wa kuwezesha jamii kunufaika na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika maeneo ya Mapori ya Akiba na Tengefu.

"Pamoja na kuimarika kwa mahusiano ajira kwa takribani wavuvi 7,511 na warina asali 2,046 jumla ya shilingi Bilioni 3.98 kutokana na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika Mapori ya Akiba ya Rukwa, Ugalla, Uwanda, Moyowosi Kilombero na Inyonga.

"Wananchi wamekuwa wakinufaika kwa kuvua wastani wa tani 15 za samaki kwa siku katika pori la akiba Uwanda pekee."

Vilevile, kupitia uvuvi Halmashauri ya Sumbawanga imekusanya Shilingi milioni 303 kupitia leseni na ushuru kutokana na uvuvi kwenye hifadhi katika katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2023.

Kamishna Mabula amefafanua kuwa,TAWA ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 na kutangazwa kwa amri (Order) ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 135 la tarehe 09 Mei 2014, pamoja na marekebisho yaliyochapishwa katika gazeti la Serikali Na. 20 la tarehe 23 Januari 2015.

"TAWA ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2016 kwa kuchukua majukumu ya kiutendaji ya Idara ya Wanyamapori kuhusu usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news