TAWA:Ujangili wa tembo umepungua nchini

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority-TAWA),Mabula Misungwi amesema, ujangili wa tembo nchini umepungua kutoka mizoga ya tembo sita mwaka 2021/22 hadi mizoga watatu Februari, 2024.
Ameyasema hayo leo Machi 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Kamishna Mabula amefafanua kuwa,mafanikio hayo yanatokana kuimarika kwa ulinzi kulikochangiwa na kuongezeka kwa vitendea kazi, morali ya watumishi.

Pia, mtandao wa kiitelijensia, doria za mwitikio wa haraka matumizi ya teknolojia na kufunga visukuma mawimbi ili kufuatilia mienendo ya wanyamapori katika kuhakikisha wanyama wanakuwa salama.

Amefafanua kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Samia Suluhu Hassan, TAWA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo makuu matatu yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Mamlaka 2021/22 - 2025/26.
Ameyataja malengo hayo kuwa ni uimarishaji wa ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na malikale, uboreshaji wa huduma za utalii pamoja na utendaji kazi wenye ufanisi na tija.

"Lengo la mkutano huu ni kuwashirikisha taarifa na mafanikio ya kiuendeshaji ya TAWA yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.

"Sote tunafahamu kuhusu umuhimu na nafasi ya vyombo vya habari katika kuendeleza uhifadhi wa rasilimali ya wanyamapori na shughuli za utalii nchini na hivyo kuchangia katika juhudi za kukuza uchumi na ustawi wa wananchi kwa ujumla."

Kamishna Mabula amefafanua kuwa,TAWA ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 na kutangazwa kwa amri (Order) ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 135 la tarehe 09 Mei 2014, pamoja na marekebisho yaliyochapishwa katika gazeti la Serikali Na. 20 la tarehe 23 Januari 2015.

"TAWA ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2016 kwa kuchukua majukumu ya kiutendaji ya Idara ya Wanyamapori kuhusu usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro."
Amesema, TAWA inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori sura 283 pamoja na kanuni zake.

Vilevile, inatekeleza Mpango Mkakati wake wa mwaka 2021/22-2025/26 ambao uliandaliwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano 2021/22-2025/26.

Aidha, TAWA pia inazingatia mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori ambayo Tanzania imeridhia.

Kamishna Mabula amebainisha kuwa, miongoni mwa majukumu ya TAWA ni kusimamia maeneo yenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 133,276.36 yanayojumuisha Mapori ya Akiba 28 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 104,176.36.

Pia, Mapori Tengefu 23 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 29,100 na maeneo ya Malikale ya Kunduchi, Kilwa-Kisiwani, Songomnara, Sanje ya Kati na Majoma na Kisiwa cha Lundo.

TR

Licha ya TAWA kuwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Afisa Mawasiliano Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho kati ya TAWA na wahariri chini ya uratibu wa ofisi hiyo leo.

TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.

TAWA leo ni taasisi ya 58 TR kuikutanisha na wahariri wakiwemo waandishi wa habari ili kuelezea walipotoka,walipo, wanapoelekea na mafanikio yao kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news