Musoma wapitisha rasimu ya bajeti kwa mwaka 2024/25 huku ikiwa tegemezi asilimia 92 Serikali Kuu

NA FRESHA KINASA

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara limepitisha rasimu ya mpango na bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya Shilingi Bilioni 30 kutoka vyanzo mbalimbali.
Ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 2.3, zinatokana na mapato ya ndani na Shilingi Bilioni 27.6 ni fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu na wafadhili. Huku maombi maalumu yakiwa yenye jumla ya shilingi Bilioni 3.55.

Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Machi Mosi, 2024 katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo baada ya Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu,   Victor Benard Nyamhanga kuwasilisha rasimu ya mpango na bajeti ya mapato na matumizi katika kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Msongela Palela.

Nyamhanga amesema, kati ya fedha zote zinazotoka Serikali Kuu shilingi bilioni 17.4 ni kwa ajili ya kulipa mishahara ya Watumishi wa Halmashauri ambayo ni sawa na asilimia 63 ya bajeti yote inayotoka serikali Kuu, ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya matumizi ya kawaida (OC) ni Shilingi Bilioni 1.35 sawa na asilimia 5, na miradi ya maendeleo ni Shilingi Bilioni 8.8 sawa na asilimia 32.

Ameongeza kuwa,  hatua hiyo inaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma bado ni tegemezi kwa serikali Kuu kwa asilimia 92. Huku Halmashauri hiyo imetenga jumla ya Shilingi milioni 390, 938, 600 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Amesema, changamoto ambazo halmashauri imekutana nazo katika kutekeleza mpango na Bajeti ya mwaka uliopita ni pamoja na fedha inayotarajiwa kupatikana kutoka Serikali Kuu kama ilivyopitishwa na Bunge kutotolewa kwa wakati au kutotolewa kabisa pia uchakavu na uhaba wa magari na boti kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za maendeleo.

Pia, uhaba wa watumishi katika sekta ya afya, elimu, ujenzi, ardhi na utawala na mahitaji halisi ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Wananchi pamoja na mahitaji halisi ya utoaji huduma kwa Wananchi kuwa mkubwa kuliko fedha inayopatikana ndani ya mwaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Msongela Palela kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato yatokanayo ya sekta ya uvuvi ambayo ndiyo muhimili wa mapato ya halmashauri hiyo.

Magoma amesema sekta ya uvuvi ikisimamiwa kikamilifu itasaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza mapato kwani hivi dasa mapato yanayokusanywa kutokana na uvuvi ni kidogo na hayaendani na uhalisia uliopo.

"Mkurugenzi simamia ukusanyaji wa mapato yanayotokana na uvuvi, Afisa uvuvi haisaidii kabisa Halmashauri hii. mapato mengi yanapotea na wakati Halmashauri yetu tunategemea ziwa Victoria ni kata tatu tu ambazo hazina ziwa Kati ya kata 21 ya Halmashauri yetu. Pia vyanzo vingine vipya vibuniwe kuongeza mapato ya ndani Jambo hili lifanye kwa ufanisi ili miradi ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa Wananchi wetu," amesema Magoma.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Musoma,  Msongela Palela amesema atahakikisha anasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato yatokanayo na sekta ya uvuvi pamoja na kuimarisha ukusanyaji katika vyanzo vingine. Huku akiwaomba Madiwani kuendelea kushirikiana na kuwa na umoja ambao utachangia kusukuma mbele maendeleo ya Halmashauri hiyo.
Msongela amesema kuwa, iwapo watashikamana na kushirikiana baina ya Watumishi wa Halmashauri hiyo na Madiwani Wananchi watapata maendeleo. Huku akiahidi kuhakikisha kwamba kwamba mipango yote ya maendeleo waliyoipanga wanajitahidi kutekeleza kulingana na upatikanaji wa fedha..

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news